Featured

    Featured Posts

    Social Icons


Loading...

HADITHI HII INAFAHAMIKA KWA JINA LA DAMU YANGU

I.s.k & M.o.j.w. Campany limited press Tanzania,
Hostel ubungo,
S.L.P 1014,
Dar-es-salaam.

© Mutalemwa O. Juvenary 2010 na Aisha. S. Kiumwa

Mkaguzi: Rajabu.Hiteshi
ISBN 6375 7 10718

             
Toleo la kwanza 2011
MTUNZI:
 AISHA SAIDI KIUMWA
               
Haki zote za kunakili zime hifadhiwa.Hairuhusiwi ama kuiga, kunakili,
  kutafsiri, kupiga chapa au kukitoa kitabu hiki kwa jinsi yoyote ile bila hidhini ya  
I.s.k & M.o.j.w. Campany limited.

                                              ENEO LA TUKIO:
                Kitabu hiki kimetungwa katika mazingira ya shule ya.
                                VICTORY SECONDARY SCHOOL.
                                          P.O.BOX 19777,
                                         DAR-ES-SALAAM,
                                             TANZANIA.
                             MAHALI: MWANDEGE-VIKINDU,
                    WILAYA YA MKURANGA, MKOA WA PWANI.
                               (Kalibu na barabara ya Kilwa)
         Mawazo, pamoja na mtililiko wa matukio ndipo ulipo anzia.


                        TAREHE: 13/05/2011, Muda:  09:28:59 Asubuhi

Kitabu hiki kimetungwa nami AISHA SAIDY KIUMWA.Kijana kutoka, kitongoji Mjimwema, wilaya ya Kigoma mjini, Kata ya Bangwe mkoani Kigoma. Japo kwa sasa naishi Kilungule kata ya Mwandege mkoa wa Pwani.



UTANGULIZI:

Jina langu kamili naitwa AISHA SAIDY KIUMWA.ni mtoto wa tano katika familia ya watoto watano,Baba yangu ni mwanajeshi msitaafu,afande SAIDI SEIF KIUMWA.Na mama yangu ni
SALMA PILI MUSA KANDA.ni mfanya biashara ndogo ndogo.

Nimependa kutunga kitabu hiki ambacho ni cha kwanza kwangu.Lakini mimi bado ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya VICTORY SECONDARY SCHOOL. Kwa mwaka (2011).
Kitabu cha Damu yangu, ni kitabu ambacho kimebeba hadithi mbili. Ambazo kati ya izombili mojawapo ndio imekuwa jina la kitabu.Nilikuwa na wakati mgumu sana katika uandaaji wa kitabu hiki.Kwa sababu muda mwingi nilikuwa nadili na mambo ya shule,na pia pindi nirudipo nyumbani kutoka shule  ilinipasa kusaidia kazi za nyumbani.Kwaiyo nilikuwa na muda mchache sana,ila namshukuru Mungu nimeweza kukamilisha zoezi hili.Na kuweza kufikisha ujumbe kwa jamii zetu. 
Kutokana na kusoma hadithi mbali mbali, nilipata ufahanu wa kutosha na pia nikapata ujasiri wa kuweza kutunga hadithi yangu kulingana na mtililiko wa matukio.katika hadithi mbalimbali nilizo jaribu kuzisoma.
Baada ya kuwa tayali nimeisha pata uzoefu wa kutosha, nilianza mara moja kuandika hadithi hii ya Damu yangu, na pia niliweza kupata msaada wa kimawazo, ushauli kutoka kwa watu mbali mbali na sehemu tofauti tofauti ndani na nje ya nchi.Napenda nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa wote walio shiriki kwa namna moja ama nyingine katika kukamilisha zoezi hili la uandishi wa kitabu hiki kilichobeba hadithi zenye kusisimua.

Natumai utafurahia sana kama utasoma kitabu hiki.Napia samahani kwa usumbufu utakao kuwepo katika kitabu hiki.Ndugu msomaji wangu.
                                        
            SHUKRANI ZA PEKEE:
      Kwa mama yangu mzazi Salma Pili Musa Kanda.
*      Kwa baba yangu mzazi Saidi Seif Kiumwa.
   Kwa rafiki yangu wa karibu sana Mutalemwa .O.Juvenary
*      Kwa rafiki yangu Asha Alli

*      Kwa marafikizangu kama vile,Rahma,Rahma Yasini,
*      Tatu, Adolla Adriani, Christina Baltazali, Khinuzya

*      Pia kwa Amadi Chome,Rajabu Shabani,Petro Juma,

*  Pamoja na wale watunzi wa hadithi wasikunyingi, ambao ndio wamenifanya mpaka niweze kutengeneza kitabu hiki.




AKNOWLDGEMENT FOR

Kwa wote walioshiliki katika kunisaidia kwenye ukamilishaji wa kitabu hiki,kwa upande huu wa mazingira ya shule pamoja na mazingira ya nyumbani.Nawapongeza sana,na Mungu awabaliki sana. Pia nitoe shukrani zangu za dhati kwa mkuu wa shule ya Victory secondary school kwa msaada wake mkubwa alioutoa kwangu Mr.Dionez Kongwa. 
                                                                      


HAYA NDIYO MAPENZI YA KWELI YA KUFA NA KUZIKANA.

SEHEMU YA TANO
Baada ya kukumbatiana kwa muda wa dakika mbili hivi, waliachiana na kuangaliana kwa chati. Kila mmoja alikua haamini macho yake kwa kile alichokiona. “karibu ndani.” Aliongea Zakaria na kumuangalia Aisha ambaye hakuwa na usemi zaidi ya kumfuata Zakaria aingiapo.


Waliingia mpaka ndani na kwa bahati mbaya umeme haukuwepo pale nyumbani. “tutafute sehemu nyingine tulivu, hapa hapafai tena.” Aliongea Zakaria na kumuangalia Aisha ambaye alikuwa hana usemi wowote kwa wakati huo.

Walitoka na kwenda sehemu tulivu kwa ajili ya kuongea mawili matatu. “unajua mpaka muda huu siamini macho yangu kuwa ni wewe ndiye ninayeongea nawe!” aliongea Zakaria baada ya kutulia kwa muda mahali hapo walipoweka kambi ya muda mfupi. “kwanini?” aliuliza Aisha huku uso wake ukiwa umejawa tabasamu.

“unajua nilienda mpaka Morogoro kukutafuta lakini nikakukosa. Nikaambiwa kuwa toka mama yako wa hiyari afariki tu na wewe ukatoweka pale” aliongea Zakaria na kumuangalia Aisha ambaye alikua makini kumsikiliza. “ni kweli zakaria, niliamua kuja huku mjini kukutafuta wewe mpenzi wangu.” 

Alifunguka Aisha bila kujali kuwa kwa sasa alikua na mtu mwingine ambaye siku za ndoa yao zilikua zinahesabika. “kusema ukweli mpaka hivi sasa bado sijachukua uamuzi wa kuwa na mwanamke mwingine japokuwa nilishakata tamaa ya kukutana na wewe tena.

Sijui wewe mwenzangu umeshanitoa moyoni?” aliuliza Zakaria huku akijaribu kuonyesha hisia zake juu ya mpenzi wake huyo waliyepotezana muda mrefu sana. Aisha alipatwa na kitu cha ajabu kilichosoma ubongoni haraka na kumpa maamuzi ya kuivua pete ya uchumba aliyovalishwa na Jack kwa siri hali iliyofanya tukio hilo lisionekane na Zakaria ambaye hakuwa makini sana kumchunguza.

“hata mimi, nimekutafuta bila mafanikio kwa muda mrefu. Japokuwa nilikata tamaa kukutana na wewe tena, ila moyo wangu umekuwa mgumu sana kumkubali mwanaume yeyeto zaidi yako wewe Zakaria” Alijikuta Aisha anaongea maneno hayo bila kujali kuwa anatengeneza tukio litakalomuumiza mtu asiyekuwa na hatia katika tasnia ya mapenzi.

Aliongea maneno hayo na kumtazama Zakaria ambaye muda huo alikuwa ametabasamu huku akoionyesha wazi kuyafurahia maneno yake. “woooooh… ahsante Mungu.” Aliongea maneno hayo Zakaria na kunyanyuka. Akamfuata Aisha alipokaa na kumyanyua.

Bila kuchelewa akamkumbatia na kuanza kumpa mabusu yasiyokuwa na idadi. Masaa yalisogea kwa kasi hadi kufikia saa tatu usiku bila ya Aisha kuonekana katika macho ya Jack. Hali ya wasi wasi iliwatanda Mack na kaka yake kwa kuhofia usalama wa Aisha. Kwa mara kadhaa walipiga simu ya Aisha na haikupokelewa.

Na baadae haikupatikana kabisa. Hali hiyo ilizidi kuwachanganya sana. Hawakuwa na raha muda wote walipokuwa wamejipanga sebuleni kumsubiri Aisha. “kwani alivyokuaga kuwa anaenda saloon, hakusema kuwa atapitia sehemu yoyote?” aliuliza Jack huku akionyesha ishara zote za kuchanganyikiwa kutokana na tukio hilo ambalo ni mara ya kwanza kutokea. 

“hakuniambia kua atapitia mahali popote, zaidi ya kuniambia kuwa anaenda saluni kuseti nywele zake.” Alijibu Mack “wewe unapajua huko saloon?” aliuliza Jack huku akiwa hatulii sehemu moja. Alikuwa anatembea tembea huku akikizunguka kile kiti alichokalia Mack na kutafuta kitu cha maana alichokuwa anakifuatilia.

Kila dakika alitupa macho yake kwenye saa ya ukutani ambayo ilikuwa inajitahidi kumuhesabia sekunde na dakika ambazo zilimsomea kuwa mpaka wakati huo saa nne juu ya alama ilikuwa imeshagota. “mambo ya wanawake brother mi nitayajulia wapi?

sijui ni wapi atakuwa ameenda.” Aliongea mdogo wake Jack na kumfanya kaka yake akae kwenye ngazi ya kuelekea chumbani badala ya kwenye sofa. Tai aliiona inamkaba, aliilegeza kidogo na kuamua kusubiri muda atakaorudi Aisha. 

Honi za gari zilizokuwa zikilia muda huo getini ndizo zilizomshtua na kumuamsha Jack pale alipokaa na kwenda nje na kufungua geti. Aliiona gari ya Aisha ikiwa nje, alifungua geti na Aisha aliingiza gari ndani na kwenda kupaki mahala pake. 

Baada ya hapo, alishuka na kuingia ndani, alimsalimia shemeji yake na kupitiliza chumbani kwake. Jack alimfuata Aisha chumbani na kumkuta anasaula nguo kwa ajili ya kulala. “kimekupata nini mke wangu mpaka unarudi muda huu?” aliuliza Jack baada ya kuingia tu ndani. 

“kuna sehemu nilienda, so foleni na ukijumlisha sikuenda muda mrefu ndio maana nimechelewa kurudi.” Alijibu Aisha kwa kujiamini na kuonyesha wazi kuwa haoni kama alikua ana kosa. “ndio hata kupiga simu angalau kutujulisha basi kwamba utachelewa?” aliongea Jack baada ya kutoridhishwa na jibu la Aisha. 

“simu yangu ilikata chaji.” Alijibu Aisha huku akiendelea kuvua nguo zake. “mbona nilipokupigia simu kwa mara kadhaa ilikua inaita bila ya wewe kuipokea?” bado Jack aliendelea kumbana Aisha kwa maswali yalimgusa Aisha kwa wakati huo. “naomba tulale Jack, maana fikira zako zinafikiria mbali sana.
Kwani huniamini?” Aisha alikwepa kujibu lile swali na kumgeuzia kibao Jack na kumuuliza yeye. “kukuamini nakuamini, tena sana tu. Ila kitendo ulichokifanya leo sijakifurahia.” Aliongea Jack kwa sauti ya upole kama yeye mwenyewe na muonekano wake ulivyo. “basi, nisamehe mume wangu.

Njoo tulale basi.” Aliongea Aisha na kumfuata Jack alipo na kuanza kumvua shati na tai. Siku ya pili yake, Jack alienda kazini kama kawaida, huko alipata kazi ambayo ita mlazimu kuchelewa kurudi nyumbani. Alichukua simu yake na kumpa Taarifa hiyo Aisha. Mishale ya saa mbili usiku, mlio wa simu ya Aisha ulimshtua alipokuwa jikoni anapika na kwenda kuipokea ile simu.

“niambie mpenzi wangu.” Iliongea sauti upande wapili baada ya simu yake kupokelewa. “safi tu. Mzima wewe?” aliongea Aisha huku akiangaza huku na huko ili ahakikishe usalama kwa kua mdogo wake Jack aliokua nyumbani. “njoo basi jamani, maana nahisi kitanda kimekuwa kikubwa sana usiku huu.” 

Aliongea mtu huyo maneno yaliyomshtua kidogo Aisha. “mpenzi wangu Zakaria, unanipa mtihani mwenzako. Sijawahi hata siku moja kulala nje ya nyumba hii. Unafikiri watanifikiriaje?” aliongea Aisha kwa sauti ndogo lakini iliyosikika vizuri kwenye masikio ya Zakaria. “we waambie tu ndugu zako kuwa leo unaenda kwa mumeo.

Na wakitaka kuniona hata kesho nikiwa nakurudisha wataniona. Kwani kuna tatizo hapo. Njoo bwana.” Aliongea Zakaria na kumfanya Aisha ashushe pumzi. “ngoja nijaribu.. sijui lakini.” Aliongea Aisha huku akionyesha kutokuwa na jibu sahihi. “nakuaminia, kama kweli unanipenda na nguvu yetu ya mapenzi bado ipo, basi utakuja kwakua tumefanya mengi makubwa na ya kushangaza kuliko hili.

”Aliongea Zakaria. “sawa, nikukute kituoni basi, maana leo sichukui gari.” Aliongea Aisha na kuonyesha kuwa alikua tayari kufanya hivyo. “poa, nakuja muda huu. Nipe dakika ishirini tu.” Aliongea zakaria na kukata simu. Aisha aliipua chakula ambacho kilikuwa tayari kimeshaiva. 

Akaingia bafuni na kuoga. Kwa haraka alichagua nguo zilizomkaa vizuri na kutinga. Wakati anajipamba kwenye dressing table, simu yake ikaita tena. “nimeshafika tayari.” Aliongea Zakaria baada ya simu yake kupokelewa. “nakuja, nipe dakika tano tu.” 

Alijibu Aisha na kuongeza spidi katika kujipamba kwake. Alitoka sebuleni kwa kunyata. Alifurahi kutomuona shemeji yake sebuleni. Huku akiwa ameshika viatu vyake, aliufikia mlango kwa style hiyo ya kunyata na kuanza kuufungua mlango huo taratibu. Hamadi! Alichokiona mbele yake hakuamini, alikua Jack yupo mlangoni kama vile alikua anamsubiria yeye amfungulie mlango.

 “UNAENDA WAPI USIKU HUU??” Aisha alikutana na swali hilo ambalo alishindwa kulijibu zaidi ya kutumbua tu macho kama mjusi aliyebanwa na mlango.

ITAENDELEA SEHEMU YA SITA....……….


Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi. 

        FACEBOOK >>> TWITTER  >>> MATUKIO KWA NJIA YA SAUTI

HAYA NDIYO MAPENZI YA KWELI YA KUFA NA KUZIKANA.

SEHEMU YA NNE
Miezi ya mateso na manyanyaso iliendelea kwa kasi kubwa bila mzee wao kuamua lolote iliendelea kwa shida na ukosaji wa haki za msingi kwa watoto hao wawili.

Muda mwingine baba yao aliwaongezea mateso pindi waliposhitakiwa, makosa yao hata kama hawakufanya kweli. Miezi sita baadae baba yao alifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha. Yule mama yao alirithi mali nyingi za mzee wao kwakua ziliandikwa kwa jina lake, kasoro nyumba moja tu ambayo ilikua na jina la marehemu mama yao.

Mungu akamjaalia Jack baada ya kusoma kwa bidii masomo yake ya biashara na kufanikiwa kuchukua stashahada. Akapata ajira katika benki ya CRDB ambayo anafanya kazi mpaka sasa hivi. Toka hapo Jackson aliapa kutojihusisha na maswala ya mapenzi kutokana na aliyoyashuhudia kutoka kwa marehemu baba yake.

Baada ya kumuhadithia Aisha stori yake iliyomfanya asimuamini mtu anayeitwa mwanamke katika maisha yake, alinyamaza na kusikiliza mawazo yatakayotolewa na dada yake huyo wa hiyari.

“pole sana, ila si kwamba wanawake wote wapo hivyo. Ni baadhi tu na hasa wanaopenda mteremko kama huyo mama yako wa kambo.” Aliongea Aisha na kumfariji Jack ambaye alikua na hali ya huzuni wakati huo.

Siku hiyo ilipita huku kila mmoja akijua maisha aliyoishi nyuma mwenzake. Upendo uliopo ndani ulikua mkubwa kila mmoja kumuamini na kumjali mwenzake. Safari za kwenda matembezi kila weekend waliongozana wote watatu.

Na hata Jack alipokuwa anaenda shooping kwa ajili ya kununua nguo, basi hakumtenga Aisha na wote walitoka ng`aring`ari kila walipotupia mapigo hayo yaliyokwenda na wakati. Ni zaidi ya nguvu ya sumaku iliyoshinikizwa na umahiri mkubwa wa Mack katika uchochezi wa hisia za watu.

Kufumba na kufumbua Jack na Aisha wakajikuta wapo ndani ya uzio wa mapenzi. Aisha alikubali kumtua Zakaria baada ya kumtafuta muda mrefu bila mafanikio. Akaamua kumpa moyo Jack ambaye hajawahi kupenda kabla ila amejawa na uoga na hisia za maumivu kwa vitendo alivyofanyiwa baba yake. 

Mapenzi hayo yaliyoanza kwa kasi ya Rocket yalizidi kukua na kupanuka siku hadi siku. Hali hiyo ilimfanya JACK kuandaa part ndogo ya kumvisha pete ya uchumba mpenzi wake huyo wa kwanza aliyemkubali ukubwani kwa kua hakuhitaji kabisa swala la mapenzi hapo kabla. 

Sherehe hiyo ilifaa sana, na Aisha alifarijika. Japokuwa hakua na ndugu katika umati wote uliohudhuria pale, ila alijiona yupo juu kwa muitiko wa watu waliohudhuria sherehe yake. Baada ya zoezi hilo kukamilika, zoezi jingine la kufunga ndoa kabisa ndio likawekwa mezani kwa muda huo.

Mchango uliotolewa na benk anayofanyia kazi na wafanya kazi wenzake ulitosha kabisa kufanya harusi kubwa. Hivyo tarehe ilipangwa na baada ya mwezi mmoja tu basi ndoa ilitakiwa kupita. Siku zilisogea kwa kasi huku kila mmoja akiwa na hamu ya kuingojea hiyo siku kwa nguvu. Shooping kwa ajili ya harusi hiyo ilianza mara moja kwa bibi harusi ambaye ndio Aisha kupewa fungu lake la hela kwa ajili ya kununua shela na vitu vingine alivyoviona ni muhimu kwake. 

Siku hiyo Aisha alitoka mapema na kuchukua funguo ya gari ndogo mpya aliyopewa kama zawadi na bosi wa benk ya CRDB katika sherehe ya kuvalishwa pete. Alitia gia na kwenda maeneo ya msasani katika maduka makubwa ya Boutique kwa ajili ya kupata shela nzuri kwa ajili ya harusi yake.

Alizunguka sana na baadae alirudi jioni bila kununua chochote. “vipi mke wangu mtarajiwa?.. hujaliona au nikakuchagulie mimi?” aliuliza Mack kiutani akijaribu kumtania shemeji yake. “sijaona toleo jipya kabisa yaani, naona yote muundo ule ule tuu.. mi nataka siku hiyo watu macho yawatoke nikipita tu.” Aliongea Aisha na kumuangalia Jack ambaye muda wote alikua anatabasamu tu.

“sasa watu wakitoka macho si itakuwa vurugu hiyo badala ya sherehe?” aliongea Mack na kumfanya Aisha aanze kumkimbiza huku akichukua mito midogo iliyopo pale sebuleni na kuanza kumrushia shemeji yake aliyekua ana vituko visivyoisha. “acha utani bwana, ninachoongea ni ukweli mtupu.

Kama vipi niagizie kutoka nje mume wangu.” Aliongea Aisha kwa kudeka baada ya kucheza kwa dakika kadhaa na Mack. “sawa, nitaongea na rafiki yangu Awena yupo Uingereza. Atanitumia picha za mashela na bei zake kwenye E-mail yangu halafu utachagua mwenyewe.” Aliongea Jack na kumuangalia Aisha aliyekua na shauku kubwa.

Alimtafuta rafiki yake huyo hewani na baabade akampata na kumuelezea shida yake kupitia e- mail walizokuwa wanatumiana. Kwa haraka Awena alimtumia rifiki yake huyo picha za mashela kadhaa yaliyomvutia Aisha na kuchagua moja wapo.

Harakati za kuhakikisha kuwa shela hilo linafika nchini zilifanywa na Awena na kupokelewa salama salimini katika mikono ya Aisha na kuwekwa kabatiki ikisubiriwa tarehe tu. Vitu vidogo viliyobakia viliandaliwa kwa haraka wakishirikiana wote watatu.

Siku moja Aisha alikua saloon maeneo ya sinza. Wakati anasetiwa nywele, kwa mbali alimuona mtu aliyemfananisha sana. “shoga hebu nitoe hili dryer,.. kuna mtu nimemfananisha.” Aliongea Aisha na yule shoga yake akafanya hivyo kama alivyoagizwa. Aisha alitoka na kumfuatilia yule kaka, alipomuangalia vizuri aligundua kuwa ni yeye kabisa.

Mara akamuona anapanda kwenye gari ndogo aina ya starlet na kuondoka. “HAIWEZEKANI” Aliongea Aisha na kuchukua funguo ya gari yake na kuanza kuifuatilia ile gari. Aliifuatilia mpaka maeneo ya sayansi kijitonyama. Gari ilipaki kwenye moja ya geti katika nyumba za pale na yule mtu akashuka. Ndipo Aisha alipomuona vizuri.

“ZAKARIAAA!!!!!” Aliita Aisha kwa sauti kubwa huku akishuka kwenye gari yake. Yule mtu naye baada ya kuisikia ile sauti aligeuka nyuma na kukutana na huyo dada aliyemuita. “AISHA!!!!!!” Yule kaka nae akalitaja hilo jina ili kuhakikisha kuwa ndiye mwenyewe au alimfananisha. Bila kusubiri, Aisha alijikuta anamkimbilia mwanaume huyo na kumkumbatia.

ITAENDELEA SEHEMU YA TANO...……..

Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi. 

        FACEBOOK >>> TWITTER  >>> MATUKIO KWA NJIA YA SAUTI

HAYA NDIYO MAPENZI YA KWELI YA KUFA NA KUZIKANA

SEHEMU YA TATU

Usingizi ulimchukua na kulala kwa masaa kadhaa. Alshtushwa na mtu aliyekuja kumuita kwa ajili ya kula chakula cha usiku. “ulichoka sana eeh.. maana umelala muda mrefu!” aliuliza Jack walipokuwa kwenye meza ya chakula.

“ni kweli. Nilikuwa na uchovu wa maana. Yaani sijui hata kama nitapata usingizi usiku huu kwa jinsi nilivyolala muda mrefu.” Aliongea Aisha na wote wakamuangalia dada huyo kwa pamoja. “unaonaje kama ukituhadithia ilivyokuwa mpaka ukaja huku Dar kumtafuta huyo mpenzi wako.” Aliongea Mack baada ya kumaliza kula.

“mimi mzawa wa morogoro. Ni mpogoro halisi kutoka kwa baba na mama yangu ambao wote kwa sasa ni marehemu.” Alianza kuhadithia Aisha huku wote wakiwa makini kumsikiliza. “pole sana.” Kipengele hicho cha kufiwa na wazazi wote wawili kiliwagusa moyoni na wote wakajikuta wanongea maneno hayo kwa pamoja.

“baada ya kifo cha baba yangu mpenzi, hapo ndipo nilichukuliwa na baba yangu mkubwa na kuanza kuishi nae pale nyumbani kwetu kama mlezi wangu na mali zangu. Mwanzo wa mateso ulianzia hapo. Kazi zote nilizifanya mimi. Niliteswa na kupigwa mara kwa mara hata wakati mwingine niliunguzwa na moto na mama yangu mkubwa.

Uzalendo ulinishinda na kuamua kutoroka pale nyumbani. Nilikimbilia kijiji cha pili, huko nilikutana na mama mmoja aliyekuwa mkulima. Hakika namshukuru sana kwa kukubali kunipokea na kunilea kama mwanae wa kumzaa. Mpaka na fika kwa huyo mama, sikuwahi kuwa na mpenzi kabla, ila baadae nilipokuwa najitambua, nilikuwa na mvulana ambaye tulikua tunapendana sana.

Hakuna ambaye alikuwa hatujui pale kijijini kuwa sisi tulikuwa wapenzi. Kwa bahati nzuri au mbaya, mpenzi wangu aliitwa na kaka yake anayeishi huku Dar, alikuwa amemtafutia kazi huku mjini na ndipo mpenzi wangu aliponiaga na kuja huku kwa huyo kaka yake. Nilivumilia sana kwakua nilikua namuamini kupita maelezo, ila mwaka mmoja baadae yule mama aliyekuwa ananilea aliaga dunia na kuniacha mimi mpweke nisiye na msaada wowote pale kijijini kwao.

Ndipo nilipoamua kuja huku Dar kwa ajili ya kumtafuta mpenzi wangu.” Aisha aliwahadithia stori ya maisha yake na kusababisha wamuonee huruma kwa msoto alioupitia. Baada ya kusikiliza stori hiyo, kila mtu aliingia chumbani kwake na kulala.

Asubuhi Jack aliamka na kumpatia Aisha kiasi cha shilingi elfu kumi kwa ajili ya nauli ya kuzunguka hapa mjini kwa ajili ya kazi yake ya kumtafuta huyo mpenzi wake aliyemteka hisia na aliyekuwa na ndoto naye nyingi kuliko mwanaume yeyote hapa duniani. Alitoka asubuhi Aisha kwa msaada wa Mack aliyekuwa anampeleka kila sehemu anayotaka kwenda na kumsaidia kumuulizia mtu huyo ambaye hawakuwa na hata picha yake.

Walirudi jioni bila mafanikio. Jack aliwapa moyo na kuwaambia watafanikiwa tu kwakua Mungu yupo na atawakutanisha tu. Zoezi la kuenda pamoja na Mack lilichukua muda wa mwezi mmoja na baadae Aisha alianza kwenda mwenyewe kwa sababu alishalizoea jiji na kila sehemu alipajua kwa muda mfupi.

Zoezi hilo lilichukua muda wa mwaka mzima bila kuonana na Zakaria. Aliheshimiwa mule ndani kama dada yao wa tumbo moja. Mpaka kupita muda huo tayari Aisha alishachoka kumtafuta mpenzi wake huyo. Aliamini kuwa ukubwa wa jiji hili, kuna uwezekano asionane nae kabisa katika maisha yake. 

“vipi dada, mbona siku hizi huendi kumtafuta shemeji, wiki ya pili leo hii hujatoka kabisa?” aliuliza Mack baada ya kumuona Aisha kila siku wakishinda wote, na hata kama akitoka basi humkuta akirudi. “ah!.. nimechoka kumtafuta Mack.” Aliongea Aisha na kumuangalia Mack ambaye walizoeana sana kuliko kaka yake ambaye alikua yupo bize na kazi kwa muda mwingi.

Na akirudi huwa amechoka hivyo kutumia mud mfupi sana kuwa karibu nay eye. Muonekano wa Asha ulibadilika sana kutokana na kukaa mjini kwa kipindi kirefu. Licha ya uzuri halisi wa mrembo huyo, lakini aina ya nguo za kisasa, kucha za bandia, kope na ma wigi ya Brazil ndio ulioubadilisha kabisa muonekano wake na kuwa wakuvutia zaidi.

Alipendeza sana kutokana na shooping za mara kwa mara alizokuwa anapigwa na Jack. Hata mule ndani walikubali kuwa uzuri wa yule dada yao wa hiyari ulifunikwa na shida tu, ila kiukweli alikuwa mzuri sema alikosa tu huduma. 

Kadri siku zinavyozidi kwenda, Aisha aliendelea kuvutia sana na kuwafanya wanaume wengi aliokuwa anakutana nao njiani au popote kutupa ndoano zao ili wajaribu bahati zao kwake. Hakuna aliyefanikiwa kwa binti huyo aliyejiwekea msimamo mkali kwa kutokubali kuvua nguo yake ya ndani kwa mvulana yoyote mpaka afunge naye ndoa.

Kipindi chote alichokuwa anaishi pale, Aisha hakuwahi hata siku moja kumuona msichana wa Jack wala kusikia stori juu ya mvulana huyo kuwa na mpenzi. Mack hakujificha, alikuwa anakuja nae mpaka pale na muda mwingine walikuwa wanakula chakula pamoja au huwa anaingia jikoni kabisa na kupika.

Swali hilo lilimuumiza kichwa kwa muda huku akihofia kumuuliza Jack. Siku hiyo aliamua kujifunga mkanda na kuamua kumvaa Jack na kuamua kumuuliza swali hilo. Jack alimuangalia Aisha kwa sekunde kadhaa kisha akamjibu. “ni story ndefu sana, ndio maana mpaka hivi sasa sihitaji kuyashobokea mapenzi.

” Aliongea Jack kwa upole na kumuangalia Aisha ambaye walikuwa wote sebuleni wakiangalia movie kutokana na kuwa siku hiyo ilikuwa ni mwisho wa wiki. “Nina muda wa kutosha wa kukusikiliza, usijali kwa hilo.” Aliongea Aisha na kumuangalia Jack ambaye muda huo alikua kama anajifikiria kumuelezea.
Baada ya sekunde kadhaa alimuangalia Aisha na kuanza kumpa stori ya maisha yake.

Jackson Peter alizaliwa hapa Dar-es-salaam katika familia yenye kipato cha juu kiasi. Alimpoteza mama yake baada ya kujifungua tu mdogo wake Mack. Huzuni ilitawala kwao. Baada ya miaka sita baadae, baba yake aliamua kuoa mwanamke mwingine ili amsaidie ulezi wa watoto wake wale wa kiume ambaye mmoja alikua ana miaka kumi na moja ambaye ndio Jack na mwingine akiwa na miaka sita peke yake ambaye ndio Mack. 

Walishi kwa furaha kwa kipindi kifupi kutoka kwa mama yao huyo wa kambo waliyeletewa na baba yao. Baada ya miezi kadhaa kupita, visa na manyanyaso vilianza kutokea kutoka kwa mama yao huyo. Walivumilia kwa muda na baadae wakaamua kufikisha malalamiko yao kwa baba yao.

Walilalamika sana bila ya mafanikio. Sanasana waliishia kufokewa na kupigwa wakati mwingine na baba yao wakishitaki chochote wanachofanyiwa na mama yao huyo aliyekuja kupoteza furaha na amani kwao.

ITAENDELEA SEHEMU YA NNE...……….



Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi. 

        FACEBOOK >>> TWITTER  >>> MATUKIO KWA NJIA YA SAUTI

HAYA NDIYO MAPENZI YA KWELI YA KUFA NA KUZIKANA

SEHEMU YA PILI
Safari ya Dar ilianza kwa taratibu huku Aisha akiwa na matumaini makubwa ya kuonana na mpenzi wake. Hakujua ukubwa wa jiji hili ni tofauti na vijiji vyao. Pia hakujua kuwa mioyo ya watu wa huku pia ni tofauti na watu wa huko kutokana na mchanganyiko mkubwa wa makabila na tabia pia.


Masaa matano baadae toka alipotoka kwao, alifika Dar kwa mara ya kwanza. Alishangaa sana kuona maghorofa na wingi wa watu waliokuwa wakishuka na kuingia kwenye jiji hili. Akiwa na begi lake la nguo, alianza kuhagaika huku na huko na kuuliza watu juu ya Zakaria. 

“namtafuta mpenzi wangu anaitwa Zakaria Kamonalelo. Sijui unamjua?” aliuliza Aisha baada ya kutembea mwendo mrefu bila kumuona mpenzi wake. “wewe dada umechanganyikiwa?.. huyo mpenzi wako sura yake ipo kwenye shilingi mpaka kila mtu amfahamu?... una wazimu wewe.” Aliongea dada mmoja aliyekuwa na rafiki yake na kusababisha kicheko kati yao.

Aisha alizunguka mpaka usiku bila ya mafanikio. Usiku ulipokuwa mkubwa, hakujua ni wapi anaweza kupata hifadhi, alitembea huku na huko na kukuta wakina dada wakiwa wamejipanga wakiuza miili yao maeneo ya shekilango.

 Alistaajabu kuwaona madada wale waliokuwa wamevaa nusu uchi, aliamua kufungua mkoba wake na kutoa khanga kadhaa na kuwapelekea.

“wewe dada una wazimu nini??... wewe wa wapi wewe?..hebu tutolee takataka zako hapa. Muangalieni huyu jamani amekuja kutufunga hela.” Aliongea dada poa mmoja baada ya kumuona Aisha amekuja kuwapa khanga. “we mwenyewe si unamuona alivyo, ametoka Kimbiji leo hii.” Alongea dada poa mwingine na kuwafanya wenzake kuangua kicheko. 

Aisha aliamua kurudisha khanga zake kwenye begi lake na kwenda kukaa pembeni kabisa. Kutokana na kuzunguka muda mrefu, uchovu aliokuwa nao uliishinda njaa na kupitiwa na usingizi mzito pale pale alipokaa. Kwa kudra za Mwenyezi Mungu palikucha salama. 

Aisha aliamka asubuhi hiyo huku akiwa hana dira yoyote ya kuelekea. Aliamka na njaa ya ajabu sana, lakini akiangalia salio lake halikumuwezesha kununua chochote hapa mjini. Aliamua kutembea huku na huko bila kuchoka kumuulizia mpenzi wake huyo ambaye hakupata majibu yaliyomridhisha.

Zaidi alipata majibu ya kumkatisha tamaa. Mpaka mchana uliingia bila ya Aisha kutia kitu chochote kinywani mwake. Mpaka kichwa pamoja na tumbo vilianza kumuuma kutokana na njaa aliyokuwa nayo. Aliamua kukaa chini na kujiinamia huku akiugulia maumivu aliyokuwa nayo.

“umepatwa na nini dada?” Ilisikika sauti ya kiume iliyomfanya Aisha anyanyue kichwa chake pale alipojiinamia na kumtazama mtu aliyemsemesha kwa tabu kutokana na maumivu aliyokuwa anayasikia muda huo. “kichwa kinaniuma na tumbo pia, ila vyote hivyo vimesababishwa na njaa kaka yangu.” 

Aliongea Aisha na kumuangalia yule mtu aliyekuja kumuangalia. “pole sana.” Aliongea yule kaka na kuingiza mkono mfukoni na kutoa waleti yake na kutoa noti moja ya shilingi elfu tano na kumkabidhi Aisha. Ilikuwa kama ndoto kwa aisha kutokana na kuijua thamani ya hela aliyopewa. “ahsante sana kaka yangu.” Alishukuru Aisha.

“usijali,” aliongea yule kaka na kuondoka zake. Hatua tano tu alizopiga yule kaka toka aondoke pale alipokuwa amekaa Aisha, alishtushwa na kishindo kikubwa kilichotokea nyuma yake. Aligeuka haraka na alichokiona hakukitarajia. Alimkuta Aisha ameanguka chini na kuzimia. 

Aliruda pale na kuamua kukodisha taksi iliyowapeleka kwenye hospitali ya magomeni usalama. Huko alipokelewa na manesi waliokuwa nje na kumuwekea dripu ya maji. Nusu saa baadae, Aisha alirejewa na fahamu na kuanza kuangaza huku na huko na kumkuta kijana aliyemuokata akiwa pale.

Yule kijana alipomuna Aisha anamuangalia, alimuita daktari ambaye alifika pale na kumkagua. Baada ya hapo alipewa chakula ambacho alikishambulia kwa kasi na kukimaliza haraka. Baada ya daktari kuridhika na hali ya mgonjwa, Aisha aliruhusiwa kurudi nyumbani. 

“wewe ni mkazi wa wapi hapa Dar?” aliuliza yule kaka ambaye alimsaidia Aisha. “mi nimkazi wa Morogoro, hapa Dar nimekuja kumtafuta mpenzi wangu tu.” Aliongea Aisha na kumuangalia yule kaka. “amekupa anuani yake au namba ya simu?” aliuliza yule kaka. “sina anuani wala namba yake.” Aliongea Aisha na kumfanya yule kaka aliyemsaidia kupigwa na butwaa.

“sasa utampataje huyo mpenzi wako?” aliuliza yule kaka na kumfanya Aisha kujiinamia kwa muda. “ni imani tu ndio niliyojiwekea kuwa nitampata.” Aliongea Aisha na kumfanya yule kaka aelewe kwa kina kitu kilichomsukuma binti huyo kutoka kijijini kwao na kuja huku Dar bila kuangalia madhara yatakayompata.

“bila shaka huna maali pa kufikia hapa mjini?” aliuliza swali yule kaka ili mradi ahakikishe kitu alichokiwaza kutokana na maelezo ya Aisha. “ndio.” Alijibu Aisha. “sawa, mi nitakupa hifadhi nyumbani kwangu. Hapo utakaa mpaka utakapofanikiwa kumpata huyo mpenzi wako.” Aliongea yule kaka na kumfanya Aisha afurahi.

Yule kaka aliyemsaidia Aisha alikodi taksi na kupelekwa nyumbani kwake maeneo ya magomeni moroco ndogo. Huko Aisha alikutana na mdogo wake wa kiume na huyo kaka ambaye walikuwa wanaishi wawili tu humo ndani. “nimeongeza familia mdogo wangu Mack. Huyu ni dada yetu wa hiyari, atajitambulisha mwenyewe.

Nimemleta hapa ili tusaidiane maswala ya hapa ndani, si unajua nyumba bila mwanamke haijakamilika?” aliongea yule kaka kwa utani na kufanya kicheko kilichodumu kwa sekunde kadhaa kutokea baina yao. “sawa kaka Jack. Ehee, dada unaitwa nani?” aliuliza mdogo wake na Jackson ambaye alionekana machachari kuliko kaka yake.

“naitwa Aisha.” Alijibu Aisha kwa aibu kidogo. “wooooh..Aisha, Mack, Jack sasa ni familia moja. Karibu sana dada yangu.” Aliongea Mack na kufanya wacheke tena. “mzoee tu mdogo wangu. Anaongea sana huyu.” Aliongea Jack na kunyanyuka alipokaa. “Aisha, hapa ndio nyumbani. Jisikie huru sana. Twende nikakuonyeshe chumba utakachokuwa unalala.

Ili kama unajisikia uchovu uende ukalale hata muda huu.” Aliongea Jack na Aisha alimfuata na kupewa chumba ambacho kilikuwa na kitanda pamoja na kabati la nguo tu. “nitachonga Dressing Table kwa ajili yako. Jisikie huru Aisha.” Aliongea kaka huyo na kumuacha Aisha mule ndani. Alikaa Aisha kwenye kitanda hicho na kushangaa kwa jinsi kilivyokuwa kinabonyea.

Alipojaribu kulala, alikuta kinadinya ndinya na kumpa raha ya kulala. Alijikuta anatabasamu peke yake na kumshukuru Mungu kwa kusaidiwa na kijana yule alionyesha kuwa na nia nzuri kwake Aisha. 

ITAENDELEA SEHEMU YA TATU…………….


Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi. 

        FACEBOOK >>> TWITTER  >>> MATUKIO KWA NJIA YA SAUTI

HAYA NDIYO MAPENZI YA KWELI YA KUFA NA KUZIKANA

SEHEMU YA KWANZA.

Mungu ameujaalia mkoa huu kwa kuwa na milima kila sehemu na miti yenye majani ya rangi ya kijani kibichi. Ameupa ardhi yenye rutuba iliyoweza kuzalisha mazao mbali mbali, pia amewapa mito japokuwa kasoro yao ni moja kubwa na ndio jina livumalo hususani ukiitaja kasoro hiyo.


Nauzungumzia mji kasoro bahari. Si mwengine na mji wa Morogoro. Huko aliishi mzee kambi na mtoto wake wa pekee Aisha. Hiyo ni kutokana na kumpoteza mke wake na kuamua kuishi hivyo huku akiridhika kumlea mtoto wake huyo wa kike aliyeachwa na mama yake akiwa na umri wa miaka sita tu.

Maisha sio mazuri kwa upande wa kipato, ila furaha ya familia hiyo ilizika mapengo yote ya umasikini walionao. Aisha alikua kwa kasi na kupelekwa shule na baba yake alipofikisha umri wa miaka saba. 

Kichwa cha msichana huyo kiliwafurahisha sana walimu wake kutokana na uwezo wa darasani aliokuwa nao. Alishika nafasi ya kwanza kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la sita ambapo aliachishwa shule na baba yake mkubwa baada ya baba yake mzazi kupooza viungo kuanzia kiunoni kushuka chini.

Walimu na wanafunzi wenzake walisikitishwa na hatua hiyo, lakini hawakuwa na la kuamua japokuwa waliamini kuwa angemaliza darasa la saba, basi lazima angefaulu tena kwa kiwango kikubwa.

Kazi ya kumuhudumuia baba yake aliachiwa peke yake. Hadi kuna vitu vingine kama kumsafisha pindi baba yake alipojisaidia aliifanya yeye mtoto wa kike huku ndugu zake wakiwa wanakuja kwa nadra sana kuwatembelea.

Mzee kambi alikua analia kila siku na kumuomba mungu amchukue ili mtoto wake asipate yale mateso aliyokuwa anayapata juu yake. Siku moja Shani alitumwa na baba yake aende akamtafutie ndulele kwa kua alikuwa anashida nazo.

Kwakua walikua wanaishi mbali kidogo na shamba lao, ilimchukua dakika ishirini kwenda na kurudi baadae baada ya dakika zipatazo arobaini na tano toka alipotoka pale.

“baba…babaaaaaaaaaaaaa’ Alilia kwa uchungu Aisha baada ya kumuona baba yake amekata roho baada ya kujichoma na kisu alichokua anakitumia kummenyea baba yake machungwa.

Kilio kilikua zaidi na majirani walikisikia kilio kile na kukusanyika eneo la tukio. Waliungana na yule mtoto na wengine wakimpooza mazito yaliyo mkuta. Baada ya mazishi ya mzee Kambi, baba mkubwa wa Aisha alichukua jukumu la kumlea mtoto huyo.

Ukurasa mpya wa mateso kutoka kwa mama yake mkubwa na baba yake huyo ulifunguliwa baada tu ya arobaini ya mzee kambi. Aligeuzwa mfanyakazi wa ndani kwenye nyumba ya marehemu wazazi wake, alichota maji, kufua nguo za watu wote mule ndani na kila kazi zenye uhusiano na ile familia, basi alizifanya yeye.

Maisha ya tabu,dhiki,mateso na msoto ndio uliomkuza Aisha. Ugumu wa maisha na kutafutiwa wanaume kwa ajili ya kuolewa kinguvu ndio vitu vilivyomchosha Aisha na kuamua kutoroka nyumbani kwao na kukimbilia kijiji cha pili.

Huko alipata hifadhi na mama mmoja baada ya kumuhadithia kila kitu kilichohusu maisha yake. Kwa imani ya yule mama, alimkaribisha na kuanza kuishi naye kama mtoto wake. Uzuri uliofunikwa na shida miaka mingi iliyopita, ulianza kuonekana taratibu kama kijua cha asubuhi kichomozapo. 

Hali iliyofanya vidume vya kijiji hicho kumtolea macho. Alinawiri vizuri kutokana na matunzo ya yule mama ambaye alifaidika naye kutokana na yeye alivyokuwa anajituma. Aisha alipotimiza miaka ishirini na moja, alifanikiwa kumpata ampendaye pale kijijini. 

Alianzisha uhusiano na mvulana huyo wa kwanza katika maisha yake kwa makubaliano ya kutofanya mapenzi mpaka ndoa. Kutokana na uelewa na mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo ZAKARIA, alikubaliana na Aisha na mapenzi yao yalinoga bila kushiriki kitendo hicho. Kila mahali walikuwa wote na walipendezana kwa hali yao.

Hakika walikuwa wakivutia kwa kila mahali wapitapo. Baada ya mwaka mmoja toka waanzishe uhusiano wa kimapenzi, Zakaria aliitwa na kaka yake Dar- es-salaam kwa ajili ya kufanya kazi kutokana na kupata nafasi aliyokuwa anamuahidi kila siku.

Kwa majonzi makubwa, Zakaria alimuambia kua anaenda kutafuta maisha na yakikaa sawa basi atakuja kumchukua. Wote walilia sana na kupeana ahadi ya kuishi pamoja tena kivyovyote vile. Zakaria aliondoka na kumuacha Aisha peke yake.

Baada ya miezi sita kupita, mama mlezi wa Aisha aligongwa na nyoka alipokuwa Shambani na kupoteza maisha. Lilikua ni zaidi ya pigo kwa Aisha ambaye hakuwa na mtegemezi mwingine pale kijijini zaidi ya yule mama peke yake.

Alilia sana na baadae uamuzi wa kwenda kumtafuta mpenzi wake mjini Dar-es-salaam ulimjia. Hela za pole alizozipata ndizo alizozitumia kwenda nazo Dar, bila kujua ni wapi afikiapo, atakapolala wala chakula atakachokula kwa siku zote atakazokuwa mjini. Yote hayo hakuyawaza zaidi ya kuamini kuwa akifika huko ataonana na mwanaume wa ndoto zake. ZAKARIA.

ITAENDELEA SEHEMU YA PILI.....……..

Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi. 

        FACEBOOK >>> TWITTER  >>> MATUKIO KWA NJIA YA SAUTI
Contact us on mutalemwa.oesmo@gmail.com. Powered by Blogger.
© Copyright Mutalemwa Blog
Back To Top