SEHEMU YA PILI
Safari ya Dar ilianza kwa taratibu huku Aisha akiwa na matumaini makubwa ya kuonana na mpenzi wake. Hakujua ukubwa wa jiji hili ni tofauti na vijiji vyao. Pia hakujua kuwa mioyo ya watu wa huku pia ni tofauti na watu wa huko kutokana na mchanganyiko mkubwa wa makabila na tabia pia.
Masaa matano baadae toka alipotoka kwao, alifika Dar kwa mara ya kwanza. Alishangaa sana kuona maghorofa na wingi wa watu waliokuwa wakishuka na kuingia kwenye jiji hili. Akiwa na begi lake la nguo, alianza kuhagaika huku na huko na kuuliza watu juu ya Zakaria.
“namtafuta mpenzi wangu anaitwa Zakaria Kamonalelo. Sijui unamjua?” aliuliza Aisha baada ya kutembea mwendo mrefu bila kumuona mpenzi wake. “wewe dada umechanganyikiwa?.. huyo mpenzi wako sura yake ipo kwenye shilingi mpaka kila mtu amfahamu?... una wazimu wewe.” Aliongea dada mmoja aliyekuwa na rafiki yake na kusababisha kicheko kati yao.
Aisha alizunguka mpaka usiku bila ya mafanikio. Usiku ulipokuwa mkubwa, hakujua ni wapi anaweza kupata hifadhi, alitembea huku na huko na kukuta wakina dada wakiwa wamejipanga wakiuza miili yao maeneo ya shekilango.
Alistaajabu kuwaona madada wale waliokuwa wamevaa nusu uchi, aliamua kufungua mkoba wake na kutoa khanga kadhaa na kuwapelekea.
“wewe dada una wazimu nini??... wewe wa wapi wewe?..hebu tutolee takataka zako hapa. Muangalieni huyu jamani amekuja kutufunga hela.” Aliongea dada poa mmoja baada ya kumuona Aisha amekuja kuwapa khanga. “we mwenyewe si unamuona alivyo, ametoka Kimbiji leo hii.” Alongea dada poa mwingine na kuwafanya wenzake kuangua kicheko.
Aisha aliamua kurudisha khanga zake kwenye begi lake na kwenda kukaa pembeni kabisa. Kutokana na kuzunguka muda mrefu, uchovu aliokuwa nao uliishinda njaa na kupitiwa na usingizi mzito pale pale alipokaa. Kwa kudra za Mwenyezi Mungu palikucha salama.
Aisha aliamka asubuhi hiyo huku akiwa hana dira yoyote ya kuelekea. Aliamka na njaa ya ajabu sana, lakini akiangalia salio lake halikumuwezesha kununua chochote hapa mjini. Aliamua kutembea huku na huko bila kuchoka kumuulizia mpenzi wake huyo ambaye hakupata majibu yaliyomridhisha.
Zaidi alipata majibu ya kumkatisha tamaa. Mpaka mchana uliingia bila ya Aisha kutia kitu chochote kinywani mwake. Mpaka kichwa pamoja na tumbo vilianza kumuuma kutokana na njaa aliyokuwa nayo. Aliamua kukaa chini na kujiinamia huku akiugulia maumivu aliyokuwa nayo.
“umepatwa na nini dada?” Ilisikika sauti ya kiume iliyomfanya Aisha anyanyue kichwa chake pale alipojiinamia na kumtazama mtu aliyemsemesha kwa tabu kutokana na maumivu aliyokuwa anayasikia muda huo. “kichwa kinaniuma na tumbo pia, ila vyote hivyo vimesababishwa na njaa kaka yangu.”
Aliongea Aisha na kumuangalia yule mtu aliyekuja kumuangalia. “pole sana.” Aliongea yule kaka na kuingiza mkono mfukoni na kutoa waleti yake na kutoa noti moja ya shilingi elfu tano na kumkabidhi Aisha. Ilikuwa kama ndoto kwa aisha kutokana na kuijua thamani ya hela aliyopewa. “ahsante sana kaka yangu.” Alishukuru Aisha.
“usijali,” aliongea yule kaka na kuondoka zake. Hatua tano tu alizopiga yule kaka toka aondoke pale alipokuwa amekaa Aisha, alishtushwa na kishindo kikubwa kilichotokea nyuma yake. Aligeuka haraka na alichokiona hakukitarajia. Alimkuta Aisha ameanguka chini na kuzimia.
Aliruda pale na kuamua kukodisha taksi iliyowapeleka kwenye hospitali ya magomeni usalama. Huko alipokelewa na manesi waliokuwa nje na kumuwekea dripu ya maji. Nusu saa baadae, Aisha alirejewa na fahamu na kuanza kuangaza huku na huko na kumkuta kijana aliyemuokata akiwa pale.
Yule kijana alipomuna Aisha anamuangalia, alimuita daktari ambaye alifika pale na kumkagua. Baada ya hapo alipewa chakula ambacho alikishambulia kwa kasi na kukimaliza haraka. Baada ya daktari kuridhika na hali ya mgonjwa, Aisha aliruhusiwa kurudi nyumbani.
“wewe ni mkazi wa wapi hapa Dar?” aliuliza yule kaka ambaye alimsaidia Aisha. “mi nimkazi wa Morogoro, hapa Dar nimekuja kumtafuta mpenzi wangu tu.” Aliongea Aisha na kumuangalia yule kaka. “amekupa anuani yake au namba ya simu?” aliuliza yule kaka. “sina anuani wala namba yake.” Aliongea Aisha na kumfanya yule kaka aliyemsaidia kupigwa na butwaa.
“sasa utampataje huyo mpenzi wako?” aliuliza yule kaka na kumfanya Aisha kujiinamia kwa muda. “ni imani tu ndio niliyojiwekea kuwa nitampata.” Aliongea Aisha na kumfanya yule kaka aelewe kwa kina kitu kilichomsukuma binti huyo kutoka kijijini kwao na kuja huku Dar bila kuangalia madhara yatakayompata.
“bila shaka huna maali pa kufikia hapa mjini?” aliuliza swali yule kaka ili mradi ahakikishe kitu alichokiwaza kutokana na maelezo ya Aisha. “ndio.” Alijibu Aisha. “sawa, mi nitakupa hifadhi nyumbani kwangu. Hapo utakaa mpaka utakapofanikiwa kumpata huyo mpenzi wako.” Aliongea yule kaka na kumfanya Aisha afurahi.
Yule kaka aliyemsaidia Aisha alikodi taksi na kupelekwa nyumbani kwake maeneo ya magomeni moroco ndogo. Huko Aisha alikutana na mdogo wake wa kiume na huyo kaka ambaye walikuwa wanaishi wawili tu humo ndani. “nimeongeza familia mdogo wangu Mack. Huyu ni dada yetu wa hiyari, atajitambulisha mwenyewe.
Nimemleta hapa ili tusaidiane maswala ya hapa ndani, si unajua nyumba bila mwanamke haijakamilika?” aliongea yule kaka kwa utani na kufanya kicheko kilichodumu kwa sekunde kadhaa kutokea baina yao. “sawa kaka Jack. Ehee, dada unaitwa nani?” aliuliza mdogo wake na Jackson ambaye alionekana machachari kuliko kaka yake.
“naitwa Aisha.” Alijibu Aisha kwa aibu kidogo. “wooooh..Aisha, Mack, Jack sasa ni familia moja. Karibu sana dada yangu.” Aliongea Mack na kufanya wacheke tena. “mzoee tu mdogo wangu. Anaongea sana huyu.” Aliongea Jack na kunyanyuka alipokaa. “Aisha, hapa ndio nyumbani. Jisikie huru sana. Twende nikakuonyeshe chumba utakachokuwa unalala.
Ili kama unajisikia uchovu uende ukalale hata muda huu.” Aliongea Jack na Aisha alimfuata na kupewa chumba ambacho kilikuwa na kitanda pamoja na kabati la nguo tu. “nitachonga Dressing Table kwa ajili yako. Jisikie huru Aisha.” Aliongea kaka huyo na kumuacha Aisha mule ndani. Alikaa Aisha kwenye kitanda hicho na kushangaa kwa jinsi kilivyokuwa kinabonyea.
Alipojaribu kulala, alikuta kinadinya ndinya na kumpa raha ya kulala. Alijikuta anatabasamu peke yake na kumshukuru Mungu kwa kusaidiwa na kijana yule alionyesha kuwa na nia nzuri kwake Aisha.
ITAENDELEA SEHEMU YA TATU…………….
Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi.
FACEBOOK >>> TWITTER >>> MATUKIO KWA NJIA YA SAUTI