Mkoa wa Iringa waomba wadau zaidi kujitokeza kusaidia waathirika wa mafuriko Pawaga.
Serikali mkoani Iringa imewaomba wasamalia wema kote nchini kuendelea kushirikiana na mkoa huo kuwasaidia wananchi waliokumbwa na mafurika katika kata mbili za tarafa ya Pawaga na kata moja ya Idodi katika tarafa ya Idodi wilayani Iringa zilikumbwa na maafa hayo ambapo zaidi ya kaya 200 zimeachwa bila makazi na kuhifadhiwa kwenye kambi za muda za Itunundu Kimande na shule ya msingi Idodi.
Mkuu wa mkoa wa Iringa Bi.Amina Masenza ametoa ombi hilo wakati akipokea msaada wa kusaidia waathirika wa mafuriko ya Pawaga kutoka kampuni ya Tigo Tanzania waliojitolea vifaa mbalimbali yakiwemo Mabranketi, Mabati na Magodoro vyote kwapamoja vikiwa na thamani ya shilingi milioni kumi.
Mkurugenzi wa Tigo kanda ya nyanda za juu kusini Jackson Kiswaga amesema kampuni hiyo imekuswa na kadhia ya mafuriko iliyowapata wananchi wa pawaga hivyo inashiriki pamoja nao katika kupunguza makali ya maisha ya waathirika hao kwa kujitolea vifaa hivyo ambavyo vitasaidia watu hao wapatao zaidi ya mia tano wakati huu ambapo hawajaweza kujitegemea.
Pamoja na mafuriko hayo eneo hilo la Pawaga limekumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu mwanzoni mwa mwezi huu ambapo zaidi ya watu mia mbili wamekwisharipotiwa kuugua ugonjwa huo huku kukiwa na vifo viwili vilivyosababishwa na ugonjwa huo baada ya mgonjwa mwingine kufariki tarehe 17 Februari.