AMREF yazindua mradi wa kupambana na ukeketaji watoto wa kike mkoani Mara.
Wilaya ya Serengeti mkoani Mara imetajwa kuongoza kwa kiasi kikubwa kwa vitendo vya ukeketaji watoto wa kike hatua ambayo imeelezwa kuwa mbali na kusababisha idadi kubwa ya watoto wa kike kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu kutokana na kuolewa muda mfupi tu baada ya kukeketwa lakini pia vitendo hivyo vimetajwa pia kuchangia ukatili mkubwa kwa watoto wa kike.
Kufuatia ongezeko kubwa la kiwango cha ukeketaji kwa watoto wa kikemkoani Mara hasa katika wilaya ya Serengeti, shirika la afya barani Afrika AMREF kwa kushirikiana na kituo cha sheria na haki za binadam LHRC wamezindua mradi wa tokomeza ukeketaji ambao unalenga kupambana na vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike katika wilayani ya Serengeti mkoani Mara.
Meneja wa mradi huo wa tokomeza ukeketaji wilayani Serengeti, Bw Phinias Johnstone, akizungumza wakati wa uzinduzi huo ambao umefanyika katika viwanja vya mbuzi mjini mugumu wilayani Serengeti, amesema mradi huo unalenga kupunguza vitendo vya ukeketaji katika wilaya hiyo hasa kwa mwaka huu ambapo tayari baadhi ya jamii imeanza kufanya maandalizi makubwa ya kukeketa watoto wa kike.
Akisoma hotuba ya mkuu wa wilaya ya Serengeti wakati wa uzinduzi wa mradi huo tokomeza ukeketaji wilayani Serengeti, katibu tawala wilaya wa wilaya hiyo Bw Qamara Cosmas, amesema mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupambana na vitendo vya ukeketaji ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya serikali katika kupambana na vitendo hivyo vya ukatili.