Wakati joto la uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu likizidi kupanda, Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeviagiza vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa kisheria, kutoendesha kampeni zao katika nyumba za ibada.
Rai hiyo imetolewa na Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega alipozungumza na waandishi wa habari jana katika Ofisi ya Tume hiyo mjini hapa. Alivitaka vyama hivyo kuzingatia maadili kama ilivyokubaliwa na vyama
vyote 22 na ambayo viongozi wake waliridhia na kusaini mbele ya Tume ya
Taifa ya Uchaguzi.
Mbali na nyumba za ibada, NEC pia imeviagiza vyama hivyo vya siasa,
kutoendesha kampeni zao katika taasisi za umma kama vile vyuo vikuu.
Kwitega alisema NEC ni chombo huru, ambacho hakifungamani na chama
chochote cha siasa na kwamba jukumu lake ni kusimamia kwa uadilifu wa
hali ya juu masuala ya Sheria za Uchaguzi nchini.
Mbali na nyumba za ibada na taasisi za Serikali, pia alivitaka vyama
vya siasa kuepuka kutumia lugha za matusi kejeli na kashfa wakati wa
kampeni, huku akivihimiza kunadi sera zake mbele ya wananchi pamoja na
yale ambayo chama husika kimetekeleza ama kinatarajia kutekeleza.
Alisema NEC itasimamia maadili ambayo yamekubaliwa na vyama vyote vya
kisiasa vyenye usajili wa kudumu. Aidha, Kwitega alivitaka vyama vya
siasa kutowatumia viongozi wa madhehebu ya dini, kuendesha kampeni zao
katika madhehebu yao.
Alisema kwamba maeneo ya ibada ni kwa ajili ya kuabudu, sio kuendesha
kampeni za kisiasa. Pazia la kampeni kwa vyama vyote, zinazotarajiwa
kufanyika kwa miezi miwili, linatarajiwa kufunguliwa Agosti 22.
Usikose kuangalia Movies mbalimbali kutoka kila kona ya dunia, bofya kwenye picha iliyopo hapo chini kuona izo muvies