Wanasiasa wametakiwa kutotumia changamoto za Muungano kama mtaji katika majukwaa yao. Hata hivyo, watu wanaopinga Muungano wametakiwa kusoma historia yake na kufahamu sababu za kuanzishwa kwa kuwa wengi wao wanakosa hoja za msingi.
Pia, serikali imepongezwa kwa kupiga hatua katika ujenzi wa maabara za sayansi katika shule za sekondari. Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Uhuru baadhi ya wasomi waliipongeza serikali kwa kupiga hatua za kimaendeleo katika kipindi cha miaka 51 ya Muungano.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mohammed Bakari, aliwaasa wanasiasa kudumisha Muungano kwa kuwa unafaida kubwa kwa taifa. Alisema changamoto za Muungano zilizopo zisitumike vibaya kutaka kuuvunja bali uimarishwe kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
Bakari alisema mwarobaini wa kutatua changamoto za muungano ni kupitishwa kwa katiba inayopendekezwa kwa sababu inatoa muongozo mzuri. Hata hivyo, alitoa rai kwa viongozi walioko madarakani kuhakikisha wanawaongoza vizuri wananchi ili dhamira ya waasisi wa Muungano iweze kufikiwa.
“Wanaopinga Muungano wanatakiwa kusoma historia na watoe maelezo kwa nini waasisi wa taifa waliamua kuleta Muungano na wasiwasemee watu kuwa hawautaki wakati hayo ni maoni yao,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Hoseah Kayumbo, aliipongeza serikali kwa kupiga hatua katika kuboresha sekta ya elimu hususan ujenzi wa maabara. Alisema wakati wakisherehekea maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano wananchi hasa wanasayansi wanapaswa kujivunia hatua iliyofikiwa.
“Wanasayansi tunajivunia muamko wa serikali kujenga maabara ambazo zitawezesha kizazi kijacho kuendesha uchumi wa kisayansi,” alisema. Alisema nchi inawajibu wa kuendelea muungano hata kama uongozi utabadilika na wenye kulalamika wataendelea kuwepo licha ya kuyaona mafanikio yaliyofikiwa.
Naye Mwenyekiti wa UPDP, Fahm Dovutwa, alisema Muungano ni mzuri na unatakiwa kuenziwa kwa sababu matatizo yaliyoko yanazungumzika.