Featured

    Featured Posts

Loading...

UCHUNGUZI WABAINI WATOTO WA MIAKA 10-17 WATUMIKA KUUZA MADAWA YA KULEVYA

Naomba nikushirikishe na wewe pia kwamba kuna mambo mengi na mazuri ndapi ya picha iliyopo hapo chini ibofye uone.

Dar es Salaam. Je, unazijua safari zote za mtoto wako wa kiume? Je, siku za mwisho wa juma au mapumziko anakuwa kwenye mazingira yanayoeleweka? Je, hakuna wakati ameonekana kuwa na vitu kuliko uwezo wa familia?

Basi kama hujui, watoto wadogo wenye umri wa kati ya miaka 10 na 17 tena baadhi wakiwa ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, wamebainika kuwa wanatumiwa na wauzaji wa dawa za kulevya kusambaza dawa hizo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa miezi miwili sasa unaonyesha kwamba baadhi ya vijana walioanza kutumika kusambaza dawa hizo wakiwa wadogo sasa ni wafanyabiashara wanaojitegemea. Mbali ya kutumiwa kusambaza dawa hizo zinazoangamiza nguvu kazi ya taifa, wanatumia dawa hizo.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, wauzaji wa dawa za kulevya huwatumia watoto hao kusambaza dawa hizo kutoka eneo moja kwenda jingine kwa kuwa ni vigumu askari kuwatilia shaka na kuwakamata watoto, tofauti na ilivyo kwa watu wazima.

Malipo kwa watoto hao hutegemea umri wao na aina ya dawa wanazosambaza. Wanafunzi wa shule za sekondari wanaotumiwa katika usafirishaji huo hupewa malipo makubwa tofauti na watoto wa umri wa chini ya miaka 13. Malipo kwa ajili ya usafirishaji wa bangi ni kati ya Sh10, 000 na Sh15,000 na wanaosafirisha dawa za kulevya kama heroin na cocaine hulipwa kati ya Sh20,000 na 30,000.


Hata hivyo, imebainika kuwa watoto wadogo ambao wengi ni wa mtaani hawajui kama wanasambaza dawa hizo bali hudhani wanatumwa tu kupeleka mzigo na kupewa fedha.

Mmoja wa watoto waishio katika mazingira magumu (jina limehifadhiwa) ameleza kwamba amekuwa akitumwa na vijana wa eneo la Kinondoni kupeleka mzigo kwa watu, maeneo ya Kimara na Mbezi.  “Sisi tunapewaga mzigo na kaka (jina linahifadhiwa) tunaupeleka kwa kaka (jina linahifadhiwa), halafu tukirudi anatupa hela,” alisema mtoto huyo wa umri wa miaka 13, mkazi wa Kinondoni Mkwajuni.

Ushuhuda

Mmoja wa vijana hao (jina linahifadhiwa) ambaye alianza kuuza dawa za kulevya tangu mwaka 2001 alipokuwa na umri wa miaka 13, anasema kwamba mjomba wake ndiye alikuwa akimtuma maeneo tofauti kupeleka mzigo na baada ya kumaliza, alikuwa akipewa Sh10,000.

“Mwanzoni sikuwa nikijua natumwa nini, nikawa natumwa hadi nilipokuwa na miaka 15. Siku moja nikajua ninachopeleka baada ya kumsikia mmoja wa wateja wa mjomba akisema lazima afungue kwanza ndipo niondoke, ili ahakikishe kama kweli ni mali,” anaeleza.

“Basi alipofungua niliona kitu kama unga unga mweupe ambao aliunusa kisha akaniamuru niondoke. Sasa wakati naondoka nikamsikia akilalamika kuwa siku hizi anapewa ‘poda’ feki,” anafafanua kijana huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 28.

“Nilikuwa na ‘good time’ (maisha mazuri). Nilikuwa na simu, enzi hizo, hata watu wazima hawana simu. Nilikuwa na uwezo wa kununua kitu chochote, siri yangu ilikuwa ni kutumwa tu kupeleka mzigo hapa na pale,” anaeleza kijana huyo aliyehitimu elimu ya sekondari.

Baadaye niliamua kuhama nyumbani na kupanga nyumba, nikanunua gari na pikipiki kutokana tu na kusambaza unga, bado nilikuwa bega kwa bega na mjomba,” anasema kijana huyo ambaye kwa sasa anadai ameacha kazi hiyo.

Polisi

Kamishna wa Polisi Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa anasema kuwa wana usalama wake wamefanya uchunguzi na kubaini kuwa watoto na vijana wadogo wa rika tofauti wanatumikishwa kusambaza dawa za kulevya jijini Dar es Salaam.

“Tumegundua kuna watu wanawatumikisha hawa watoto, tulizunguka hapa jijini na kupata taarifa kuwa watoto wa rika tofauti wanafanyishwa kazi za kusambaza unga,” anasema Kamishna Nzowa na kuongeza kwamba watoto hao wa umri wa hadi miaka 10 hawafanyi kazi ya kusambaza tu, bali pia wananunua dawa za kulevya kwa ajili ya matumizi yao.

Machi 2013, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema kwamba wauzaji wa dawa za kulevya wanaweka dawa hizo kwenye mikate na barafu zinazouzwa kwenye shule.

Lukuvi ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika maadhimisho ya Siku ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya alisema Serikali itaanza kufuatilia biashara hizo shuleni.

“Sasa dawa hizi zinauzwa hadi kwenye vitu ambavyo watoto wanakula katika shule za msingi. Kwa mfano, hivi sasa dawa hizo zinawekwa kwenye maandazi, mikate na barafu. Ni lazima kufahamu watu gani wanauza vyakula vya aina hiyo na wana nia gani,” alisema Lukuvi.

Lukuvi alisema kuwa watu hao wamekuwa wakisababisha vijana wengi wa shule za msingi na hata sekondari kuwa na tabia za ajabu na alitaja baadhi ya matendo ya ajabu kuwa ni mtoto wa shule kuingia darasani akiwa na kiatu kimoja mguuni, mkufu wenye nyembe, kidani chenye nyembe kifuani, misumari mifukoni, hawafungi lisani za suruali zao na wengine kutembea vifua wazi.

Uchunguzi

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili jijini Dar es Salaam maeneo ya shule kwenye wilaya za Kinondoni, Temeke na Ilala, unaonyesha kwamba wasambazaji wa kawaida wa dawa za kulevya huitwa ‘mapusha’ wakati watoto wanaotumiwa kufanya kazi hiyo huitwa ‘masadal’. Masadal hupewa mzigo kuuza au wakati mwingine kuusambaza tu na kupewa fedha kwa ajili ya kazi ya usambazaji.

“Kwa siku unaweza kupewa mzigo wa Sh200, 000 au Sh300, 000, ukiumaliza unapewa malipo ya Sh 50,000, basi. Lakini si kila siku unaweza kupewa mzigo, inatokea siku na siku,” anasema mmoja wa wasambazaji hao mwenye miaka 16 eneo la Tabata.

Eneo la Kinondoni, Manyanya, Mwananyamala Komakoma kuna idadi kubwa ya vijana wadogo wanaotumiwa kusambaza ‘unga.’ Hata hivyo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura anasema kwamba khajawahi kupata taarifa za watoto wadogo kutumika kusambaza dawa za kulevya.

Baadhi ya walimu katika shule za msingi, waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, walisema baadhi ya wanafunzi katika shule zao wana tabia sawa na vijana mitaani wanaovuta bangi.

“Wewe unaona mwanafunzi wako anatembea na vijana wavuta bangi, kwa vyovyote naye atakuwa anashiriki,” anasema mwalimu wa shule moja wilayani Temeke.

Mwalimu Mkuu (jina linahifadhiwa) wa shule moja ya msingi eneo la Tabata alikiri kuwa wapo wanafunzi wenye mienendo inayotia shaka na hata baadhi ya wazazi anasema wamekuwa wakifika kushtaki kutokana na mabadiliko ya watoto wao.

“Unakuta mwanafunzi kwao familia ina kipato cha chini, lakini yeye anaishi maisha aghali sana hapa shuleni; ana simu ya gharama, anavaa mavazi ya gharama na wakati mwingine anawapa wanafunzi wenzake fedha. Hapo tunapata wasiwasi huenda ameingizwa kwenye mtandao huo,” alisema Mwalimu katika shule moja ya jeshi jijini.  Mwalimu mwingine wa shule binafsi katika Wilaya ya Temeke alisema kuwa wachezaji mpira wakiwa na timu za mitaani huvuta bangi kwa kile wanachodai kuondoa nishai na kwamba wapo wanaotumia dawa za kulevya.

“Mimi naijua shule hii… hata wanafunzi wake wengine tayari wanatumia dawa za kulevya,” alisema mwalimu huyo.

Ripoti ya hali ya dawa za kulevya inayotolewa na Tume ya Taifa ya Dawa za Kulevya kwa mwaka 2013 inaonyesha kuwa Wilaya ya Kinondoni ina watumiaji 2, 941 wa dawa za kulevya ambao wamesajiliwa na wameanza kupata tiba ya uraibu. Kati ya hao, wanaume ni 2, 162 na wanawake ni 879. Temeke ina watumiaji 2, 963 wakati Ilala ina watumiaji wanaume 453 na wanawake 23.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa Kitengo cha Uhalifu na Dawa za Kulevya (UNODC) kwa mwaka 2013, inaeleza kuwa kuna Watanzania 176 waliokamatwa nchini China kwa kesi za dawa za kulevya. Nako Brazil kuna wafungwa zaidi ya 103 na Hong Kong kuna Watanzania zaidi ya 200 wenye kesi za dawa za kulevya, ambapo kesi 130 zimeshatolewa hukumu na kesi 70 bado zinaendelea.
Usikose kuangalia Movies mbalimbali kutoka kila kona ya dunia, bofya kwenye picha iliyopo hapo chini kuona izo muvies
Nobody is a total failure if he dares to try to do something worthwhile. Tough times never last, but tough people do. The place broke up with applause. Those thirty - five hundred farmers who had lost hope and had battled depression found that hope.

Share habari hii kadri uwezavyo.

Contact us on mutalemwa.oesmo@gmail.com. Powered by Blogger.
© Copyright Mutalemwa Blog
Back To Top