Kisheria yapo mazingira ambapo mtu aliyeuza ardhi anaweza kuidai tena ardhi ileile aliyouza kutoka kwa mnunuzi na akaipata. Na hapa haijalishi kama mnunuzi ameiendeleza ardhi kwa kiasi gani au amebadilisha hati na kuingia jina lake na vitu vingine kama hivyo.
Sheria imetoa haki hii kwa muuzaji hasa iwapo masharti katika mkataba wa mauziano yamevunjwa. Kwa kawaida kila mkataba wa mauziano ya ardhi huwa na masharti ambayo hupaswa kutekelezwa na kila upande. Masharti haya huwa ni ya msingi na hupaswa kutekelezwa vilevile kama ilivyokubaliwa.
Kuvunjwa/kukiukwa kwake hutoa haki kwa muuzaji kuchukua tena kilicho chake yaani kujirejeshea umiliki wa ardhi. Na hii mara nyingi husababishwa na kuingia mikataba kiholela bila kupata ushauri au kusimamiwa na wanasheria ambao hupanga masharti haya kwa ufundi usio na madhara. Hapa chini tutaona jambo hili hufanyikaje kisheria.
1.MUUZAJI KUJIMILIKISHA TENA ARDHI BAADA YA KUUZA.
Sehemu ndogo ya tatu, kifungu cha 73 – 76 cha Sheria ya Ardhi ndivyo vifungu katika sheria ya ardhi vinavyoeleza kwa urefu namna ya kujimilikisha tena ardhi baada ya kuiuza.
Kifungu cha 73 kinaanza kwa kusema kuwa. mkataba wa mauziano ya ardhi unapokuwa umekamilika na mnunuzi ameshakuwa mmiliki wa ardhi aliyonunua, muuzaji anaweza kujitoa katika mkataba huo pale ambapo mnunuzi atakiuka au kwenda kinyume na masharti au makubaliano katika mkataba huo. Maana iliyo katika kifungu hiki ni kuwa tayari mkataba umekamilika, na mnunuzi amemiliki lile eneo iwe nyumba, shamba au kiwanja .
Na amemiliki kwa kiwango kuwa mpaka hati/leseni ya makazi/ofa n.k tayari ina jina lake, lakini kuna mambo aliahidiana na yule aliyemuuzia na bado hajayatekeleza mpaka sasa. Basi huyu aliyemuuzia ana haki ya kudai umiliki au kuchukua tena ile ardhi. Anachukuaje ile ardhi tutaona hapa chini.
2. SABABU ZA KUJIREJESHEA UMILIKI BAADA YA KUUZA.
Sababu kubwa za kisheria za muuzaji kujitoa katika mkataba na kujirejeshea umiliki ni kutokufuatwa kwa masharti au makubaliano yaliyo katika mkataba wa mauzo( sale agreement).
Kwa mfano kutomaliziwa kwa hela . Unakuta mnunuzi ameahidi kuwa atamalizia kiwango cha hela kilichobaki ndani ya miezi mitatu tangu siku ya kusainiwa kwa mkataba. Muda huo unafika mpaka unapita mnunuzi hataki kulipa hela na tayari anamiliki eneo. Au ni ardhi ya kijiji na ameahidi kuiendeleza ndani ya muda fulani lakini bado hajafanya hivyo na muda umepita sasa. Haya ndio mazingira na kwa ufupi hii huhusisha kutotekelezwa kwa yale aliyoahidi mnunuzi katika mkataba wa mauzo si lazima yawe hayo tu niliyotaja.