SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limeingia mkataba na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wa mauzo ya sehemu ya eneo la ofisi katika mradi wake wa Morocco Square ulioko Kinondoni, Dar es Salaam.
Mkataba huo ulitiwa saini jana na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu na Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Moremi Marwa.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, Mchechu alisema mkataba huo utagharimu sh. bilioni 3.3 na kwamba malipo yatafanyika kwa awamu nne katika kipindi cha miaka mitatu.
Mchechu alisema mradi wa Morocco Square una ukubwa wa mita za mraba 105,000, na utakamilika katika kipindi cha miaka mitatu.
Alisema mradi huo umebuniwa kulingana na mahitaji ya majengo ya sasa na ya baadaye ambapo utakuwa na huduma zote muhimu na utaboresha mazingira ya biashara katika jiji la Dar es Salaam.
Alisema makubaliano waliyofikia yatatoa fursa kwa DSE na mawakala wake wa soko la mitaji kutumia jengo hilo. Mchechu aliwataka wanaohitaji maeneo ya ofisi, biashara na nyumba za kuishi katika mradi huo wafike ofisi za NHC kwa ajili ya kukamilisha taratibu za manunuzi.
Kwa upande wake, Marwa alisema lengo la DSE ni kuziwezesha kampuni kupata mitaji. Alisema soko hilo litanunua sehemu ya mradi wa Morocco ambapo wataweka ofisi zao.
Marwa aliongeza kuwa DSE inaendelea kuboresha shughuli zake na mwaka huu, kampuni tano zitasajiliwa.