Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga, amesitisha shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu katika machimbo madogo ya Kaole yaliyopo Kata ya Lunguyu wilayani Msalala.
Alisema ameamua kusitisha kwa muda shughuli za uchimbaji kwa ajili ya kupisha timu ya watalamu kutoka mgodi wa dhahabu Bulyanhulu kuendelea na kazi ya kutafuta watu wengine waliofukiwa na kifusi.
Rufunga alitoa amri hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi katika machimbo ya Kalole, ambapo aliwapa pole kwa kupoteza ndugu waliofariki kwa kuangukiwa na kifusi cha udongo.
Alisema serikali imefikia uamuzi wa kufunga kwa muda shughuli za uchimbaji kutokana na watu 19 kupoteza maisha baada ya kufukiwa na kifusi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kalole, Khamis Misungwi, alisema zaidi ya wachimbaji wadogo 400, wanaendesha shughuli zao katika mgodi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, alisema maiti 18 zilitambuliwa na ndugu zao na mmoja bado hajatambuliwa.Hata hivyo, Rufunga aliwataka viongozi wa serikali ya kijiji kutoruhusu watu kuendelea na uchimbaji katika eneo hilo.