Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Nzega leo hii imemhukumu Masanja Mwinamila (44), mkazi wa Kitongoji cha Kona Nne, Kijiji cha Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala, Tarafa ya Puge wilayani Nzega katika Mkoa wa Tabora kwenda jela miaka 10 kwa kosa la kuteka mtoto mwenye albinism, Margreth Hamisi (6).
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Saraphine Nsana, alitoa hukumu hiyo baada ya mshtakiwa kusomewa shtaka na kukiri kutenda kosa hilo.
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba, mnamo Juni 15, 2015 majira ya saa 3:00 usiku katika Kijiji cha Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala wilayani Nzega, mtuhumiwa alimteka binti huyo kwa lengo la kwenda ‘kumuuza’ ili ajipatie fedha (kiasi kimehifadhiwa).
Hii ni mara ya kwanza kwa kesi inayohusisha utekaji nyara, kujeruhi na mauaji dhidi ya watu wenye albinism kuchukua muda mfupi zaidi, kwani ndiyo kwanza kesi hiyo ya Jinai Namba 116/2015 imefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kutolewa hukumu.
Jitihada za Polisi
Mafanikio ya kukamatwa kwa Masanja Mwinamila akiwa katika harakati za kutaka kumuuza mtoto Margreth Hamisi, ambaye ni mpwa wake, yametokana na umakini wa Jeshi la Polisi nchini ambapo maofisa wake wa Kikosi Kazi cha Taifa waliweka mtego na kufanikiwa kumnasa mtuhumiwa kabla hajamdhuru mateka wake.
Tukio hilo limefanikisha kuubomoa mtandao hatari wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwani ni takriban wiki tatu tu tangu maofisa usalama walipofanikiwa kuwanasa watu wengine sita wakiwa katika harakati za kuuza mifupa inayodhaniwa kuwa ya binadamu (albino) mjini Kahama Mei 22, 2015 ambapo tayari wamekwishafikishwa mahakamani pamoja na wengine watatu waliokamatwa baadaye.
Matukio hayo mawili makubwa yaliyotokea katika kipindi hicho yamedhihirisha namna serikali kupitia jeshi hilo na vyombo vingine vya usalama inavyoshughulikia mitandao hiyo hatari usiku na mchana ili kuhakikisha Watanzania wote wanaishi kwa amani na usalama.