Habari za leo wapendwa. Ninaamini mnaendelea vizuri kabisa na masomo yenu kuelekea mwisho wa mwaka, ambao una mambo mengi kwelikweli. Mimi nasonga kama kawaida, siku zinaenda na sasa namba zinabadilika.
Mtakumbuka wiki jana tulijadili hapa jinsi gani baadhi yetu tulibadili tabia kutokana na kupenda kujihusisha na mambo ya disco wakati tukiwa shule, ambako tulikutana na vishawishi vilivyosababisha wengi wetu kujikuta tuki-copy na ku-paste mambo ya mtaani, ambayo kwa kiasi kikubwa yalisaidia sana kutuondolea umakini katika mambo ya shule.
Siku kadhaa nyuma niliwahi kuandika hapa kuhusu tabia ya baadhi ya madenti, hasa jijini Dar es Salaam ambao hujikuta katika ugomvi usioisha baina yao na makondakta wa mabasi ya abiria, ambayo ni maarufu kama daladala. Ugomvi huu, ambao hufanywa na wanafunzi wa kiume hasa wa sekondari, huwasababishia wenzao wakati mwingine kukataliwa kupanda mabasi hayo.
Sina uhakika kama somo lile liliwaingia vizuri maana juzi kati nimekutana tena na kisanga kingine katika gari wakati nikirudi nyumbani kutoka kibaruani. Siku zile nilisema kwamba kutokana na vitendo vya kihuni vinavyofanywa na wanafunzi wakiwa ndani ya daladala, huwafanya makondakta na madereva kutosimama katika vituo ambavyo wanafunzi wanakuwa wengi.
Hii, pamoja na wakati mwingine kwa kuona kwamba wanafunzi hao wanalipa hela ndogo, lakini pia ni kutokana na usumbufu wao garini, wengine hukataa kulipa nauli na kibaya zaidi, wanaweza hata kuwatukana makondakta.
Sasa ndiyo juzikati, nipo zangu na abiria wengine tunarejea nyumbani baada ya mihangaiko ya mchana kutwa, gari imefika kituo kimoja hivi ikawabeba abiria, wakiwemo vijana kama watano hivi walioonekana wametoka mazoezini, kwa sababu walikuwa wamevaa mavazi ya kimichezo, traksuti na jezi.
Gari likaendelea na safari yake, kama kawaida konda anaulizia kama kuna watu wanashuka kituo kinachofuata, wakisema wapo, anawaita wasogee mlangoni na yeye anachukua nauli yake. Ndo mmoja kati ya wale vijana akasema anashuka kituo kinachofuata.
Konda akamwambia asogee na alipodai nauli yake, yule kijana akatoa nauli za wanafunzi, yaani shilingi mia mbili. Jamaa akifahamu kwamba ni mwanafunzi, akamtaka aonyeshe kitambulisho chake kama sheria zinavyotaka. Hapo ndipo utata ulipoanza. Dogo akasema, tena kwa sauti, kitambulisho cha nini, kwani huoni hii jezi?
Watu wakapigwa na mshangao, kitambulisho tokea lini kiwe jezi? Konda akakataa na dogo akakomaa, ikawa toa, sitoi, abiria tumekodoa macho kuona nini kitatokea. Gari kufika kituoni, denti akamsukuma konda, wote wakatoka nje, wamekabana mashati, niachie, sikuachii hadi mtu mmoja akajitolea kumlipia nauli kijana huyo.
Wakati wamekabana, bwana mdogo anamtisha konda, nitakupiga vichwa wewe mjinga! Na kweli, kwa kuwatazama, dogo alionekana mkakamavu kuliko kondakta. Baada ya songombingo lile kumalizika, watu wakaanza kumjadili yule bwana mdogo, wakimuona ndiye mkosefu, kwani konda alikuwa na haki.
Na tatizo pale wala halikuwa hela, ni kauli tu. Bwana mdogo angeweza kusema kwa lugha laini tu kuwa hakuwa au alisahau kitambulisho. Konda angemuelewa kwa sababu kwa kumtazama, alionekana bado kijana mdogo na wenzake aliopanda nao, walikuwa wamevaa sare.
Lakini kutokana na kauli zake, hata wenzake walibakia wameduwaa wasiweze kumtetea. Ninachotaka kusisitiza tena kwa madenti, hakuna kitu muhimu kwenu kama nidhamu, hasa mnapokuwa nje ya maeneo ya shule.
Maana pale watu wakaanza kusema mzazi wa yule denti wanapoteza fedha zao bure, kwa sababu kwa tabia ile, ni wazi kuwa hata anapokuwa shuleni, hakuna tofauti.
Mnafanya mambo hayo kwa kujiona ni wajanja, labda kwa vile mnaamini hamtafanywa kitu kwa vile nyinyi ni madenti, ukweli ni kwamba mnajidanganya. Mtu mwenye nidhamu mbaya, hutoa ishara kuwa hata kichwani mwake hamna kitu!
Kwa habari za Matukio Kitaifa, Kimataifa, Michezo na Burudani, Ungana nami kupitia Link zifuatazo.
FACEBOOK >>> TWITTER >>> MATUKIO >> MUSIC MPYA