Maafisa wa polisi nchini Kenya wanasema wamemnasa mshukiwa mkuu wa Al-Shabaab mjini Nairobi. Mshukiwa huyo alikuwa nchini Kenya kutafuta matibabu. Duru zingine zinasema kuwa alikuwa mwanahabari zamani na anashukuwa kujihuhusisha na mauaji ya waandishi wa habari wa Somali huko Mogadishu.
Ni nadra kunasa washukiwa kama hawa wanaoingia nchi jirani ya Kenya kupitia mipaka yake ambayo bado haina ulinzi wa kutosha. Mshukiwa huyo anadhaniwa kuwa Hassan Hanafi na amekuwa akizuru Kenya mara kwa mara.
Maafisa wa polisi wameambia BBC kuwa alitiwa nguvuni siku chache zilizopita na anahojiwa na maafisa wa kitengo maalum cha polisi kinachoshughulikia maswala ya ugaidi.
Maafisa wa Usalama wa Somali wamesema kuwa ushirikiano kati ya majasusi wa Kenya na Somali ndiko kulipelekea au kuwezesha kukamatwa kwa mshukiwa huyo ambaye anadai ameshikwa kimakosa na kufananishwa na mtu mwingine.
Hanafi anashukiwa kutekeleza au kufadhili mauaji ya wanahabari mjini Mogadishu. Zaidi ya wanahabari 20 wameuwawa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita nchini Somalia. Inaaminika kuwa Hanafi alijiunga na Al-Shabaab mwaka 2006, baada ya Ethiopia kuondoa mamlakani muungano wa mahakama za kiislamu.
Baadaye Hanafi alifanya kazi katika kituo cha Redio cha Andalus, ambacho hutumiwa kama ni kipaza sauti cha al-Shabaab nchini Somalia, na hatimaye kujiunga na mrengo wa Al-Shabaab unaotumia silaha hatari.
Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi.