Rangi ya mdomo au ‘lipstick’ kama inavyofahamika kwa wengi ni urembo unaopendwa zaidi na wanawake.Ni ukweli usiopingika kuwa ‘lipstick’ imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza urembo wa mwanamke na kumfanya aonekane mwenye mvuto.
Wapo wanawake ambao wanaweza kupaka ‘lipstick’ mara moja na kukaa nayo kutwa nzima kisha kuifuta jioni kabla ya kulala. Vilevile wapo ambao hupaka hata zaidi ya mara tatu kwa siku kutokana na kufutika kwa sababu mbalimbali, lakini kubwa zaidi ni kujilamba.
Ni wachache ambao hupata muda wa kujiuliza maswali kuwa hiyo ‘lipstick’ inayofutika inakwenda wapi na ina madhara gani? Utafiti wa kisayansi uliofanywa na watalaamu kutoka School of Public Health na kuchapishwa katika Jarida la Environmental Health Perspective, Umeonyesha kuwa ‘lipstick’inatengenezwa na kemikali kadhaa zinazoweza kuwa na madhara ya kiafya kwa mtumiaji.
Hilo linasababishwa zaidi na ulambaji wa ‘lipstick’, hivyo kumweka mtumiaji kwenye hatari ya kupata maradhi kadhaa yakiwemo saratani. Kutokana na hali hiyo, tunapaswa kuwa makini wakati wa kupaka lipstick na kuhakikisha haturusu iingie mdomoni mara kwa mara.
Makala haya hayalengi kuwatisha au kuwafanya wanawake wakose raha wanapopaka ‘lipstick’ bali kuwasisitiza kuwa makini na kupunguza matumizi ya kupita kiasi ya kipodozi hicho.
Kwa mtu asiyeweza kukaa nayo kwa muda mrefu, hashauriwi kuirudia mara kwa mara. Ni vyema akatafuta njia nyingine ya kurembesha mdomo wake, hata kwa kupaka ‘lipshine’ zinazotengenezwa kwa matunda.