Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imeunga mkono hatua inayochukuliwa na Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam ya kutoruhusu waendesha pikipiki ‘bodaboda’ na pikipiki za magurudumu matatu kufika maeneo ya katikati ya jiji.
Mamlaka hiyo imefafanua kuwa imekasimu madaraka kwa Serikali za Mitaa katika kutoa leseni kwa watu wanaoendesha vyombo hivi kibiashara.
Ofisa Uhusiano wa Sumatra, David Mziray alisema wao kama mamlaka wanafanya kazi ya kuandaa kanuni ambazo zinatumika kama sheria, jeshi la polisi hufanya kazi ya kusimamia kanuni hizo na kuzitekeleza kama inavyotakiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki hivi karibuni aliagiza vyombo mbalimbali vya usalama kusimamia mpango wa kupiga marufuku bodaboda kuingia katikati ya jiji hatua iliyopokewa kwa hisia tofauti.
Hivi karibuni, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika aliitaka Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kusitisha zoezi hilo ili kutoa nafasi kwa serikali na wahusika wa bodaboda na bajaji kufanya mazungumzo.