Watu wawili akiwamo mwanafunzi wa kidato cha tatu wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na kundi la watu wanne waliokuwa wakitumia silaha aina ya SMG na SAR katika Kijiji cha Alidonyowassu, Tarafa ya Loliondo, wilayani Ngorongoro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4:30 asubuhi wakati wananchi hao wakitoka Kijiji cha Digodigo kuelekea Loliondo wakiwa kwenye gari aina ya Land Rover, lililokuwa likiendeshwa na Emmanuel Shayo, mkazi wa Kilimanjaro.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Ibrahim John (15), mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Digodigo aliyepigwa risasi ya shingo, Athuman Hamad (25) mkazi wa Loliondo ambaye alikuwa utingo wa gari hilo.
Waliojeruhiwa ni Janeth Samwel, Ester Paulo, Aden Sindoya na Pendo Loyi. Wengine ni Pendo Ezekiel na Emmanuel Ter.
Kamanda huyo alisema chanzo cha tukio hilo hakijajulikana kwani hakuna kitu chochote kilichoporwa na kwamba polisi inaendelea na msako ili kuwakamata waliohusika na tukio hilo, ambapo miili ya waliofariki imehifadhiwa kwenye Hospitali ya Wasson na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
Wakati huo huo, watu wawili wenye asili ya Kiasia, Mavan Patel (20) na Nisha Patel (26) wakazi wa Metropole jijini Arusha wamekamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin Aprili 9, mwaka huu.
Watu hao walikamatwa na kete 170 na kete 300 za bangi zikiwa zimehifadhiwa kwenye mfuko mweusi, huku gramu 150 za heroine zikiwa zimehifadhiwa kwenye mpira wa kiume (kondomu) ndani ya gari aina ya Nissan.Watuhumiwa hao wapo chini ya ulinzi wa polisi kwa ajili ya mahojiano na watafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika.