Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mwalimu Izekiel Oluoch, akichangia mjadala wa Sura ya Kwanza na ya Pili za Rasimu ya Pili ya Katiba, wakati wa mjadala wa vifungu hivyo, bungeni mjini Dodoma.
WALIMU wa Manispaa ya Kigoma /Ujiji, ambao siyo wanachama wa Chama cha Walimu(CWT), baada ya kupigania haki zao na hatimaye kuondoka kwenye chama hicho na kusitishwa makato ya mishahara yao asilimia mbili, wamemtaka Naibu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiel Oluoch, kuacha kuwasemea walimu bila kuwauliza.
Hayo yamo katika waraka wao ulioandikwa Mei 30, mwaka huu na kusambazwa kwa vyombo mbalimbali nchini, wakipinga kumtuma Oluoch, kuwasemea katika Bunge maalum la Katiba lililoahirishwa hivi karibuni.
Katika waraka huo ambao Mtandao wa kalulunga media umepata nakala yake na kuthibitishwa na Mwalimu T. Nyamkunga, ambaye ni Katibu wa sekretarieti ya walimu hao, wamesema kuwa, Naibu Katibu Mkuu huyo wa CWT, hajawahi kuendesha mchakato wa kura ya maoni kwa walimu, ili kujua walimu wanahitaji muundo wa serikali ngapi, tofauti na alivyochangia kuwa wanataka Serikali tatu.
“Tumefanya hivyo ili kuondoa tabia za baadhi ya viongozi wa kada mbalimbali ikiwemo CWT, kuwasemea watu bila idhini yao na hasa mambo yanayohusu misimamo ya kikatiba” umeeleza waraka huo.
Mwalimu Nyamkunga alisema, wao kama walimu, wanasubiri utaratibu wa Serikali wa kila mwananchi kupiga kura baada ya marekebisho ya rasimu hiyo katika Bunge la Katiba na kwamba kwasasa hawajamtuma mtu yeyote Bungeni kuwasemea muundo wa serikali wautakao, iwe serikali moja, mbili au tatu.
Walisema kauli za Oluoch Bungeni, zichukuliwe kama kauli za wanasiasa wengine, maana huo ni msimamo wake binafsi na wala siyo msimamo wa walimu wote nchini na kwamba huko ni kupora uhuru wa mawazo ya walimu, waliopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuwa huru kimawazo.