Hii ni tofauti na wenzetu wazungu ambao hujishughulisha na kujua mambo ya msingi katika shughuli zao mbalimbali wanazoziendesha. Kutokana na hili nimekuwa nikieleza mara kwa mara baadhi ya mambo ya msingi kuhusu kampuni. Nakumbuka nimewahi kueleza namna ya kuunda kampuni, maana ya neno limited, namna ya kuandaa mahesabu ya kampuni, jinsi ya kununua na kuuza hisa, na mengine mengi. Kwa anayetaka kuyaona haya atembelee SHERIA YAKUB BLOG. Leo tena naeleza kitu kingine ambacho ni, Maana ya hisa na aina zake ( shares) .
1.NINI MAANA YA HISA.
Hisa ni maslahi ya kila mwanahisa aliyonayo katika kampuni fulani. Yaani wewe kama ni mwanahisa katika kampuni fulani basi yale maslahi yako au kiwango chako cha uwekezaji ulichowekeza katika ile kampuni ndio hisa zako. Kama mko watu kumi katika kampuni basi kila mtu ana maslahi au kiwango kadhaa cha uwekezaji ambapo ukikusanya uwekezaji huo kwa pamoja ndio utaitwa hisa za kampuni. Uwekezaji au maslahi katika kampuni hutofautiana kutokana na uwezo wa kila mwanahisa.
Tofauti hutokana na kiwango cha kila mtu alichowekeza. Kuna mwenye hisa kumi, kuna mwenye ishirini, kuna mwenye hisa mia n.k. Hisa siku zote hupimwa kwa kiwango cha pesa. Yawezekana uwekezaji wa mtu kwenye kampuni ni magari yaani amepata hisa kwa kuchangia magari. Mwingine amepata hisa kwa kuchangia ofisi. Na mwingine amepata hisa kwa kuchangia vifaa vyote vya ofisi. Katika kuhesabu hisa michango hii yote itawekwa katika viwango vya pesa na itasemwa kuwa fulani ana hisa za shilingi kadhaa na sio ana hisa za magari au vifaa kadhaa. Kwa hiyo hisa huhesabiwa kwa mtindo/viwango vya fedha.
2. AINA ZA HISA.
Hisa sio hisa kama wengi tunavyojua isipokuwa hisa zina aina zake. Sio kila mwenye hisa ana hisa isipokuwa ana hisa gani au za aina gani. Aina za hisa za mtu katika kampuni ndio humwezesha kujua ana haki gani katika kampuni, ana wajibu gani na anawajibikaje likitokea tatizo. Kwa hiyo haki, wajibu(duty) na uwajibikaji(liability) katika kampuni hutofautiana kutoka mwanahisa mmoja hadi mwingine kutokana na aina za hisa anazomiliki. Wanahisa wote hawana haki sawa, hawana wajibu sawa na hawawajibika sawa pamoja na kuwa katika kampuni moja. Hapa chini tutaona aina za hisa.
( a ) HISA ZA WAMILIKI ( EQUITY SHARES).
Hizi ni aina za hisa ambazo huwa ndio nyingi katika kampuni. Wale wanaomiliki hisa nyingi katika kampuni hisa zao huitwa hisa za wamiliki. Huitwa hisa za wamiliki kwakuwa hawa huhesabika kama ndio kampuni yenyewe na hivyo wenye hisa hizo ndio wamiliki wa kampuni. Nimesema hapo juu kuwa wanahisa hawana haki sawa, wajibu pamoja na uwajibikaji. Wenye hisa hizi wana haki kubwa ya kimaamuzi katika shughuli zote za uendeshaji wa kampuni kwakuwa wao kila hisa moja huwa ni kura moja na kwahiyo kila kitu hupitishwa kwa kura zao. Pia wana haki ya kupata mgao mkubwa kuliko wengine. Hata hivyo wanawajibika zaidi linapotokea tatizo kwa mfano inapotokea hasara wao ndio hupoteza zaidi. Kwa jina jingine hisa za hawa huitwa HISA ZA SIMBA( LIONS SHARE). Hii ni kwasababu huko mwituni simba hupata mgao mkubwa wa nyama kati ya wanyama wote.
( b ) HISA ZA KAWAIDA.
Hizi ni zile hisa ambazo humilikiwa na watu wengine wa kawaida katika kampuni. Mara nyingi hawa ndio huwa wengi japo kila mtu huwa na hisa kidogo kidogo. Mgao wao wa faida hutokana na asilimia ya kile mtu anachomiliki. Maamuzi yao katika kampuni huwa ni madogo ukilinganisha na wenye zile hisa za umiliki( equity shares). Hata hivyo uwajibikaji wao nao ni mdogo pia kwani hupata hasara kidogo pale kampuni inapopata hasara. Pamoja na hayo sheria imewapa kipaumbele cha kupewa mgao wa faida kabla ya kundi jingine lolote.
( c ) HISA ZA WAANZILISHI ( DEFERRED SHARES).
Hizi ni hisa ambazo hutolewa kama zawadi kwa waanzilishi wa kampuni. Mgao wa faida wa hisa hizi huwa sio wa moja kwa moja isipokuwa hutegemea na faida inayozidi. Kawaida mgao wa faida kwa wanahisa wengine hutoka katika faida ya kawaida lakini hawa hawapewi mgao kutoka faida ya kawaida isipokuwa hupata pale faida inapozidi au kuvuka kiwango ilichotegemewa.
( d ) HISA ZA KAMPUNI( CORPORATE SHARES).
Zote nilizotaja juu ni hisa za kampuni lakini bado jina hili hupewa hisa hizi kutokana na kuwa ni hisa maalum ambazo hutolewa kwa waajiriwa/wafanyakazi katika kampuni husika. Waajiriwa hutengewa hisa zao na mwenye uwezo huweza kuchukua hisa hizo kwa kiwango cha uwezo wake. Mwajiriwa huendelea kuwa na hisa hizo hata baada ya utumishi wake kukoma . Kwa ufupi sana niseme tu kuwa hisa sio hisa ila hisa ni una hisa za aina gani Usikose kuangalia Movies mbalimbali kutoka kila kona ya dunia, bofya kwenye picha iliyopo hapo chini kuona izo muvies