Wanawake wanaokunywa pombe kupita kiwango kinachokubalika wapo katika hatari ya kuathirika maini mapema kuliko wanaume.
Mkurugenzi wa kliniki ya kimataifa ya afya ya uzazi kwa mama, baba, mtoto na vijana, Dk. Ali Mzige, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na NIPASHE.
Alisema hali hiyo inatokana na mfumo wa mwili wa mtu kutofautiana na wa mwingine na pia kutegemeana na aina ya pombe na kiasi anachokunywa.
Dk. Mzige alisema kitaalamu mwanamke anapaswa kunywa chupa moja ya bia kwa siku na mwanaume chupa mbili.
Hata hivyo, alisema hivi sasa wanawake wamekuwa wakinywa kupita kiasi mijini na vijijini, kitu ambacho ni hatari kiafya.
"Wanywaji wa pombe wa muda mrefu, ambao tunaweza kuwapa jina la ‘chapombe' wanaanza kuwa na dalili za afya zao kuyumba na kutetereka wanapofikia umri wa miaka 30-40," alisema Dk. Mzige.
Alizitaja athari wanazopata wanywaji wengi wa pombe kuwa ni pamoja na sukari mwilini kushuka, protini mbalimbali na za kiwango tofauti kushuka, shinikizo la damu, nguvu za kiume na za kike kupungua, kumbukumbu kupungua na baadaye kupotea kabisa.
Alisema pia mtu yeyote ambaye ini lake limeharibiwa na pombe, maumivu makali, homa, kukosa hamu ya kula chakula na kichefuchefu.