Serikali imesema kuwa iliamua kununua ndege mbili za abiria aina ya Bombadier Q400 kutoka nchini Canada kutokana na uhitaji wa huduma ya usafiri wa anga kwa safari za ndani ya nchi na mazingira halisi ya viwanja vya ndege vilivyopo nchini.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakufunzi wa marubani katika chuo cha Taifa cha usafirishaji(NIT).
Mbarawa alisema kuwa Serikali haikukurupuka katika kufanya maamuzi ya aina ya ndege za kununua badala yake imezingatia vigezo na malengo mahsusi ya kuhudumia usafiri wa ndani na kuboresha usafiri wa anga kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
“Serikali imeamua kununua aina hii ya ndege za Bombadier Q400 kutokana na hali halisi ya Viwanja vya ndege nchini kuwa vya Changarawe na lami kwa baadhi, huku lengo ni kutoa huduma za usafiri wa ndani” Alisema Profesa Mbarawa.