Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) hatimaye wametaja mfanyabiashara ambaye alibainishwa na Rais John Magufuli katika hafla ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Ikulu Dar es Salaam juzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola alimtaja mfanyabiashara huyo kuwa ni Mohammed Mustafa Yusuf Ali anayetuhumiwa kuiibia Serikali matrilioni ya shilingi kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs) ambazo hazijasajiliwa na TRA na kutoa risiti bandia.
Alisema TRA kwa kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na uchunguzi ili kubaini makampuni yote yanayojihusisha na udanganyifu huu, ambapo hadi sasa jumla ya makampuni manne yamebainika kujihusisha na ukwepaji kodi kwa mtindo huu kuanzia mwaka 2010 hadi 2014; na jumla ya Sh 29,216,900,301.7 imebainika kutokulipwa serikalini na makampuni hayo kwa kipindi hicho.
Alisema kwa sasa wanaendelea na mahojiano naye zaidi ili kuwabaini wote wanaohusika na mfumo huo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa TRA, Alfayo Kidata aliyeambatana na Mlowola katika mkutano huo wa waandishi wa habari, makampuni hayo yamekuwa yakinunua risiti za manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki mashine za EFDs ambazo hazijasajiliwa.
Usikose kuangalia Movies mbalimbali kutoka kila kona ya dunia, bofya kwenye picha iliyopo hapo chini kuona izo muvies