Serikali mkoani Tanga imewaondoa hofu wananchi wa jiji la Tanga kuwa vikundi vya uhalifu vilivyojikita katika mapango ya Amboni na kujihusisha na vitendo vya uporaji kisha kupoteza maisha ya baadhi ya watu ni wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakitumia nafasi ya kujificha katika mapango hayo.
Akizungumza ofisini kwake baada ya hali ya sintofahamu kujitokeza katika mapango ya Amboni huku askari polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wakiimarisha ulinzi usiku na mchana katika eneo hilo,Mkuu wa mkoa wa Tanga Martin Shegela amesema wahamiaji hao wamehusika na vitendo vya uporaji katika duka la kuuza mikate la Central Baker ambapo walifanya mauaji ya watu wanne kwa kutumia silaha za moto kisha kupora fedha na kukimbilia mapangoni.
Hata hivyo baadhi ya wakazi wanaojihusisha na kilimo jirani na mapango ya Amboni,wakizunguzmia hali hiyo wamedai kuwa wameagizwa mwisho wa kufanya shughuli za kilimo iwe saa 10 jioni kwa sababu ya usalama wao kufuatia kuibuka kwa hali ya sintofahamu katika mapango ya Amboni.
Kufuatia hatua hiyo,baadhi ya wakulima wameiomba serikali kuwamegea mashamba waliyoomba tangu mwaka 2010 ili kusafisha mapori yaliyopo jirani na mapango ya Amboni mleni maji moto ambayo yamekuwa maficho ya wahalifu
hasa baada ya kampuni ya Amboni plastic kusitisha uzalishaji miaka 15 iliyopita kisha eneo hilo kuchukua mwekezaji ambaye inadaiwa kuwa hajaendeleza eneo hilo.