Wanafunzi Kibangile watumia vyoo hatarishi na wakabiliwa na uhaba wa madawati.
Wanafunzi wa shule ya msingi Kibangile tarafa ya Matombo wilayani Morogoro wako hatarini ikiwemo kuugua magonjwa ya mlipuko kutokana na kutumia vyoo hatarishi na vichafu vilivyojengwa kwa udongo na miti na kuezekwa kwa nyasi, huku wakikabiliwa pia na tatizo la uhaba wa madawati na uchakavu wa majengo hali inayotishia pia kushuka kwa kiwango cha ufaulu.
Afisa elimu wa wilaya ya Morogoro,Donald Pambe,amekiri changamoto hiyo kuzikabili shule mbalibali za wilaya hiyo,ingawa kwa Kibangile hali ni mbaya zaidi na hivi karibuni ugonjwa wa kipindupindu uliibuka shuleni hapo, lakini wako kwenye mkakati kuhakikisha mazingira yanaboreshwa na hali inakuwa nzuri, huku lile la madawati akisema tayari wameomba kibali kwa halmashauri ili waweze kukata miti kwaajili ya kutengeneza madawati.
Kutokana na changamoto ya madawati, kampuni ya simu za mkononi ya Tigo Tanzania imetoa madawati 400 kwa shule 10 za msingi katika wilaya ya Morogoro ikiwemo kibangile, ambapo mkurugenzi wa Tigo kanda ya Pwani,Goodluck Charles amesema wamefanya hivyo ili kuungana na jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano kuboresha maisha ya watanzania, huku mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya halmashauri ya wilaya ya Morogoro,Robert Selasela,akiwataka wanajumuiya wa shule mbalimbali za wilaya hiyo kutunza madawati hayo na kuwa na utayari wa kuchangia mahitaji mbalimbali yanayohusu elimu.