Ndege ya kubeba abiria imetua kwa dharura katika uwanja wa ndege mjini Mogadishu, Somalia ikiwa na shimo kubwa kwenye kiunzi chake.
Shimo hilo kwenye ndege hiyo lilitoboka muda mfupi baada ya ndege hiyo kupaa kutoka Mogadishu, ikiwa futi 10,000 (3,048m) juu angani, jamaa wa mmoja wa abiria ameambia BBC.
Haijabainika ni nini kilichotoboa shimbo hilo. Maafisa wanasema abiria wawili waliumia.
Ndege hiyo ya shirika la ndege la Daallo, iliyokuwa ikielekea Djibouti, ilikuwa imebeba watu karibu 60, afisa wa polisi ameambia shirika la habari la Bloomberg.
Baadhi ya ripoti zinasema ndege hiyo ilishika moto muda mfupi baada ya kupaa.
Darren Howe, ambaye mwenzake alikuwa ameabiri ndege hiyo, alipiga picha inayoonyesha shimo hilo muda mfupi baada ya ndege hiyo kutua.
"Hakukutokea mlipuko. Ni kiunzi cha ndege kilichopata hitilafu ndege ikiwa futi 10,000 angani,” ameambia BBC.
Ndege za shirika la Daallo husafiri mara kwa mara kati ya Dubai, Somalia na Djibouti.