Operesheni kagua umeme nyumba kwa nyumba yabaini uharibifu mkubwa Kahama.
Wakaguzi kutoka katika shirika la ugavi wa umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Shinyanga wakishirikiana na jeshi la polisi wamefanya operesheni ya kukagua mita za umeme kwa wateja wa shirika hilo katika mji wa Kahama na kubaini idadi kubwa ya wateja walioharibu miundombinu na kuchezea mita huku wakitumia umeme bure kinyume na sheria na taratibu za shirika hilo.
Katika operesheni hiyo ya kushtukiza nyumba kwa nyumba maofisa wa Tanesco wamebaini idadi kubwa ya wateja wanaotumia umeme kinyume na taratibu kwa kuchezea mita na kuharibu miundombinu huku mteja mmoja aliyetambulika kwa jina la Issa Mvano anayemiliki duka na kituo cha afya mjini hapo akiwa ameharibu miundombinu na kuchezea mita katika biashara zake zote pamoja na nyumbani ambapo kwa mujibu wa taratibu za shirika mteja huyo amesitishiwa huduma na kuagizwa kufika katika ofisi za Tanesco kwa hatua zaidi za kisheria.
Aidha maofisa wa Tanesco walijaribu kumtafuta mteja huyo bila mafanikio na walipomtafuta kwa njia ya simu alidai kuwa yuko safarini hali iliyomlazimu mhandisi wa miundombinu ya Tanesco mkoa wa Shinyanga Bw.Tadei Kasiki kutoa tamko juu ya watu wanaohujumu miundombinu ya Tanesco.
Katika hatua nyingine meneja wa Tanesco wilaya ya kahama Bw.Sule Kabati amewalalamikia wasambazaji wa miundombinu ya Televisheni maarufu kama Cable Tv kwa kupitisha nyaya zao juu ya miundombinu ya Tanesco hali inayoathiri mfumo wa usambazaji umeme wa shirika na kuhatarisha maisha ya watu huku akitoa muda wa mwezi mmoja kuondoa nyaya zao na baada ya hapo shirika litachukua hatua kali za kisheria dhidi yao.