Mwekezaji afunga njia ya kuingia katika mashamba ya wananchi mkoani Iringa.
Wananchi wa vijiji vya Makota na Kaning’ombe kata ya Mseke mkoani Iringa wamemlalamikia mwekezaji wa moja ya mashamba makubwa kijijini Makota anayemiliki jumla ya hekari 973 kufunga njia ya asili inayoingia kwenye mashamba ya wanavijiji hao na kuwasababishia hasara kubwa kutoka na baadhi ya mazao yao ya mbogamboga kuharibika baada ya magari kushindwa kuingia kwenye mashamba hayo.
Wakitoa kilio chao mbele ya mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela aliyefika kwenye shamba hilo kujionea hali hiyo baadhi ya wananchi wamesema mwekezaji huyo anayejulikana kwa jina la Bethania licha ya kufunga njia hiyo lakini pia ametelekeza shamba hilo kwa miaka mingi lakini wameshangaa ujio wake wa mwaka huu akifika na kuwangia njia hiyo.
Diwani wa kata ya Mseke Mathias Nganyagwa amesema mgogoro huo ni wa muda mrefu ambapo mwekezaji huyo amekuwa akikaidi vikao na wito wa serikali jambo ambalo limewakasirisha wananchi hao na kuamua kujichukulia sheria mikononi lakini uongozi wa kata hiyo uliwaomba kuvuta subira ili kuipa serikali nafasi kushughulikia mgogoro huo kwa njia za amani.
Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela amemuagiza mwekezaji huyo kufungua njia mara moja ili wananchi kuendelea na shughuli za kilimo kama kawaida huku afisa ardhi wa halmashauri ya iringa vijiji Geofrey Kaluwa akisema kuwa serikali ipo katika mchakato wa kufuta mashamba pori likiwemo shamba hilo ili kuyatoa kwa watu wanaoweza kuyaendeleza ama kuyabadilisha matumizi.
Usikose kuangalia Movies mbalimbali kutoka kila kona ya dunia, bofya kwenye picha iliyopo hapo chini kuona izo muvies