Vijiji 50 vyanufaika na matumizi bora ya ardhi mkoani Kigoma.
Taasisi ya uhifadhi ya Jane Goodall Tanzania kupitia mradi wa uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii wa Gombe Masito Ugala, imefanikiwa kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji zaidi ya 50 katika mikoa ya Kigoma na Katavi mpango ambao unalenga kuboresha maisha ya jamii na kupunguza migogoro isiyo ya lazima katika makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo wakulima na wafugaji.
Mratibu wa zoezi la kupanga matumizi bora ya ardhi katika mradi wa Gombe Masito Ugala unaotekelezwa na taasisi ya Jane Goodall kwenye mikoa ya Kigoma na Katavi, Fadhili Mlacha ameiambia Mutalemwa Blog kuwa mchakato huo wa kupima vijiji na kuviwekea mipango ya matumzi bora ya ardhi umewawezesha wananchi wengi katika vijiji hivyo 50 kutumia vizuri ardhi ya maeneo yao ambayo sasa inakidhi mahitaji ya kilimo, mifugo, makazi na misitu ya hifadhi za vijiji.
Nao baadhi ya wananchi wanaotekeleza mradi huo wamesema umesaidia kuboresha maisha kwani kila eneo limepangiwa matumzi yake na umeongeza kipato kwa jamii kutokana na mazao ya misitu ikiwemo Uyoga na ufugaji wa Nyuki.
Kwa upande wao baadhi ya wataalam wa mazingira na wanahabari kutoka taasisi ya Jane Goodall nchini Marekani Shawn Sweeney na Bill Wallaueer walioko mkoani Kigoma kuangalia shughuli za jamii zinazotekelezwa na JGI Tanzania wamezungumzia kuhusu miradi inayotekelezwa na taasisi hiyo kwa wananchi wa vijijini na pia wamesisitiza kuhusu umuhimu wa vyombo vya habari katika kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, misitu na wanyamapori kwenye maeneo mbalimbali nchini.