NEMC yalalamikiwa kushindwa kudhibiti uharibifu wa mazingira katika mto Nyakasangwe Bunju.
Baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira NEMC na halmashauri ya manispaa ya Kinondoni wamelalamikiwa kwa kushindwa kudhibiti uharibifu wa mazingira unaofanywa kwa maksudi na kikundi cha watu kwa kuchimba mchanga katika mto Nyakasangwe eneo la Boko Dovya kata ya Bunju jijini Dar es Salaam huku wakijeruhi na kuwatishia watu wanaowazuia kuchimba na kusomba mchanga katika mto huo.
Mbali na viongozi wa eneo hilo kutishiwa na watu hao wanaochimba mchanga na kusomba na malori katika mto nyakasangwe, baadhi ya viongozi wa mtaa wa Dovya kata ya Bunju
wamesema mmoja wa wajumbe alishawahi kutekwa na wachimba mchanga hao na taarifa ikapelekwa kituo cha polisi wazo lakini mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa
huku baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira-NEMC na manispaa ya Kinondoni wakionekana kushindwa kudhibiti hali hiyo na kikundi hicho kinaendelea kutamba.
Licha ya ITV kutofanikiwa kuzungumza na mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni kuhusu uharibifu wa mto huo baada ya kujulishwa kwamba yupo nje ya ofisi kikazi, camera ya ITV ikafika katika ofisi ya baraza la taifa la hifadhi ya mazingira ambao wamekiri kupata taarifa ya mto huo na kuahidi kushirikiana na jeshi la polisi kudhibiti watu hao.