Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Tanzania Jakaya Kikwete
wamezindua mradi wa ujenzi wa barabara ya Taveta-Mwatate ambayo
inatarajiwa kurahisisha uchukuzi kati ya kataifa hayo mawili.
Barabara ya Arusha-Holili upande wa Tanzania pia inakarabatiwa.
Rais Kikwete yumo nchini Kenya kwa ziara rasmi ya siku tatu na Jumanne anatarajiwa kuhutubia kikao cha pamoja cha mabunge mawili ya Kenya.
Mradi wa ujenzi wa barabara hizo mbili umefadhiliwa kwa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika na serikali za Kenya na Tanzania.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa kanda hii wa AfDB Gabriel Negatu benki hiyo imetoa $218 milioni za kutumiwa kwenye mradi huo, Kenya ikipokea $116 milioni na Tanzania $102 milioni.
Huo ndio mradi wa pili wa barabara wa kuunganisha Kenya na Tanzania uliofadhiliwa na benki hiyo, wa kwanza ukiwa barabara za Arusha-Namanga/Namanga-Athi River.
Rais Kikwete alisema barabara hiyo ya Taveta-Mwatate hutumiwa na wakazi wa kaskazini na kaskazini-magharibi mwa Tanzania kusafirisha bidhaa hadi Mombasa.
“Huchukua saa 14 kutoka Arusha hadi Voi. Lakini ujenzi huu ukikamilika, itachukua saa mbili na nusu pekee, hivyo kuwa nafuu sana kwa wasafiri na wenye magari,” alisema.
Kiongozi huyo, anayetarajiwa kuondoka mamlakani karibuni baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, alisema barabara hiyo ina uwezo wa kuimarisha biashara kati ya Kenya na Tanzania kwa asilimia 10.