Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuzungumza na kusema yupo salama, mke wake, Josephine Mushumbusi
amekanusha tuhuma zilizozagaa kuwa ndiye aliyemshauri kiongozi huyo wa
Chadema kujiuzulu na kumzuia kushiriki vikao muhimu vya chama.
Tetesi hizo zilivuma kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari
baada ya Dk Slaa kutoonekana katika vikao muhimu vya Chadema na Ukawa,
kuwa Mushumbusi hakupendezwa na kitendo cha Lowassa kupitishwa kuwania
urais chini ya mwavuli wa Ukawa na badala yake alitaka Dk Slaa ndiye awe
mpeperusha bendera.
Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo Mushumbusi amezikanusha, aliamua
alimfungia ndani Dk Slaa kama moja ya mbinu za kumzuia asishiriki
shughuli za kichama, tuhuma ambazo amezikanusha.
“Bosi wako akija kukuomba ushauri utamsaidia, lakini akija akakuambia ameshafanya maamuzi unaweza kupingana naye?” alihoji Mushumbusi akianza kutoa maelezo yake na kuendelea: “Wakati wa vikao nilikuwa
namwona (Dk Slaa) anachelewa kurudi kila siku, siku moja akaja
akaniambia uamuzi aliouchukua na mimi sikuwa na la kusema, nikachukua
shuka nikajifunika.”
Katika mahojiano yake ya kwanza na Mwananchi baada ya kuzagaa kwa
tetesi hizo, Mushumbusi pia alikana kumfungia Dk Slaa ndani ya nyumba,
akisema wakati maneno hayo yalipokuwa yanazagaa, alikuwa nje ya nchi na
wala hakujua kinachoendelea.
“Mwenyewe najiuliza nini
kinaendelea, siwezi kufanya kitu kama hicho. Nyumba yangu ina milango
miwili, nawezaje kumfungia mtu, tena mwanamume, hata watoto siwezi
kuwafungia. Kuna mambo mengine mwanamke huwezi kuyafanya kwa mwanamume.
Mwanamume ni mwanamume tu,” alisema.
Alisema viongozi wa Chadema, ndugu, jamaa na marafiki walikuwa
wanafika nyumbani kwake na walikutana na Dk Slaa na kuzungumza naye… “Kama ningekuwa nimemfungia wangezungumza naye vipi?”
Mushumbusi alisema mwanamke anaweza kufanya chochote lakini kuna baadhi ya mambo ambayo mwanamume akiamua ni vigumu kumzuia. Akifafanua tuhuma za kumshinikiza Dk Slaa kujiuzulu Chadema,
Mushumbusi alisema kiongozi huyo wa Chadema ana uamuzi wake na yeye ni
msaidizi tu ambaye hana uamuzi wa mwisho kwenye familia.
Hata hivyo, alisema endapo angeamua kumshawishi, uwezo wa kufanya
hivyo anao lakini yeye ni mwanamke mwadilifu anayependa mafanikio ya
mumewe.
“Kwani unanionaje? Mimi ni ‘strong’ (nina nguvu), ningetaka ningefanya hivyo, nisingeshindwa,” alisema.
Pamoja na hayo, Mushumbusi alilalamika kuwa tuhuma hizo dhidi yake zimesababisha asisikilizwe kama ilivyokuwa awali. Bila kufafanua kwa undani, alisema kuna kundi linalounda propaganda
hizo ili abadili mtazamo kuhusu mumewe lakini jambo hilo haliwezi
kutokea.
“Nilisema nitampenda kama
alivyo, sitajali chochote wala akiwa katika hali gani au chama gani.
Kazi yangu ni kumtia moyo ili kile atakachofanya kifanikiwe,” alisema. Mbali na kukanusha vikali tuhuma hizo, Mushumbusi alisema
alikwishajitoa kwenye masuala ya siasa kwa miaka miwili sasa na badala
yake ameamua kufanya biashara ya kuuza mkaa.
Usikose kuangalia Movies mbalimbali kutoka kila kona ya dunia, bofya kwenye picha iliyopo hapo chini kuona izo muvies