Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kina wagombea wawili wanaowania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Madai hayo mapya ya Profesa Lipumba yametolewa siku tatu baada ya
kujiuzulu uenyekiti CUF, akisema hiyo ni moja ya sababu za kuachia
nafasi yake kutokana na uamuzi uliofikiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuhusu mgombea urais.
Profesa Lipumba alisema dhamira yake ilikuwa
inamsuta kwa kuwaingiza ndani ya Ukawa watu kutoka CCM, waliokuwa
wanapingana na maoni ya wananchi kuhusu rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba
na kuwapa fursa ya kuwania urais.
Juzi usiku katika mahojiano aliyoyafanya na Azam TV kutoka Kigali
alikosema anafanya utafiti, Profesa Lipumba alisema kumpa nafasi waziri
mkuu mstaafu, Edward Lowassa kuwania urais kupitia Chadema ndani ya
Ukawa, ni sawa na CCM kusimamisha wagombea wawili (Lowassa) na Waziri wa
Ujenzi, Dk John Magufuli.
Katika mahojiano hayo ya simu, Profesa Lipumba ambaye wiki mbili
zilizopita alimpokea Lowassa akisema ni mtu safi na kwamba, ufisadi
ndani ya CCM ni mfumo alisema katika kujiuzulu kwake hakutumiwa na CCM
kuparaganyisha Ukawa, bali walikuwa tayari wameparaganyika.
“Ukweli ni kwamba
tumejiparaganyisha wenyewe ndani ya Ukawa. Kwa hiyo Watanzania watakuwa
na wanaCCM wawili wanaogombea urais wakati Ukawa tulikuwa na wagombea
watatu… mimi, Dk Willibrod Slaa, (Katibu Mkuu wa Chadema) pamoja na Dk
George Kahangwa (NCCR-Mageuzi) ambaye alikiri kuwapo makubaliano hayo.
“Tulikutana nyumbani kwangu tukakubaliana Dk Slaa apeperushe bendera ya Ukawa, lakini tumewekwa kando,” Prof. Lipumba.
Alisema yupo Rwanda kwa muda na anafanya utafiti kuona namna gani
Tanzania inaweza kujifunza mambo ya kiuchumi kutokana na nchi hiyo
kupiga hatua kubwa kiuchumi. Pia alisisitiza kuwa hajahama nchi na kwamba wiki hii anatarajia kurejea nchini.
Usikose kuangalia Movies mbalimbali kutoka kila kona ya dunia, bofya kwenye picha iliyopo hapo chini kuona izo muvies