Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeibua tuhuma mpya dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
kikisema kimebaini shahada zaidi ya milioni mbili za kupigia kura
zinazotarajiwa kuingizwa kinyemela katika Daftari la Wapiga Kura na
kugawiwa kwa wana CCM ambao hawakujiandikisha.
Chama hicho kimedai kwamba, mbali na shahada hizo pia wakimbizi zaidi
ya 70,000 mkoani Kigoma wameandikishwa katika daftari hilo kwa ajili ya
kupiga kura.
Tuhuma hizo zilitolewa jijini Dar es Salaam jana mbela ya waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chadema (BAWACHA), Halima Mdee na kada wa chama hicho, Saed Kubenea.
Akizungumza katika mkutano huo, Kubenea aliwaonyesha takribani
shahada 100 alizosema ndizo zitakazoingizwa kwenye dafatari hilo kinyume
cha taratibu.
Shahada hizo hazina jina la mpiga kura, picha, tarehe ya kuzaliwa,
sehemu na eneo alilojiandikisha pamoja na taarifa nyingine muhumu
zinazowekwa kwenye shahada halali.
“Chadema tumebaini kuwepo kwa
mpango wa kuingizwa kwa shahada za kupigia kura zaidi ya milioni mbili,
ambazo zinatarajiwa kutumiwa na wana CCM ambao walikuwa
hawakujiandikisha katika daftari la kupigia kura,” Kubenea.
“Inawezekana kabisa NEC kwa
kushirikiana na CCM wamepanga kuingiza majina yao katika shahada hizi,
na ndiyo maana hata kuna baadhi ya watu walikamatwa wakiwa na mashine
nyumbani kwa watu,” alisema.
Kubenea alisema vitambulisho hivyo vimetengenezwa ili kuongeza kura
za CCM kwa wanachama wake ambao hawakupata nafasi ya kujiandikisha.
“Nchi yenye idadi hiyo ya watu
haiwezi kuwa na wapiga kura milioni 23, kwa mujibu wa takwimu za Tume
ya Takwimu ya Taifa wanasema asilimia 60 ya Watanzania wako chini ya
miaka 18, hivyo ukichukua nusu ya Watanzania milioni 45 itakuwa ni
milioni 22.5 kama wote wangeingia kwenye sensa hivyo kwa tathmini hiyo
nyongeza hiyo ni wizi,” alisema.
Kubenea alitoa wito kwa NEC kufanyakazi kwa uaminifu na uadilifu ili
kuondokana na mipango ya kuongezwa kwa kura za watu ambao
hawakujiandikisha katika daftari la wapiga kura.
Kwa upande wake Halima Mdee alisema kuwa chama hicho kimepata taarifa
kutoka kwa wafanyakazi wa Tume wakisema kuwa kuna wakimbizi 70,000
walioandikishwa kutoka mkoani Kigoma.
“Kuna wafanyakazi wa tume ambao
ni wasamaria wema wametupatia taarifa za ndani zinazosema kuwa katika
kuhakikisha ushindi unapatikana wamewaandikishwa wakimbizi 70,000 kutoka
mikoa ya kigoma,” alisema.
Mdee alisema kuwa ujanja wa kutafuta kura za kupata bao la mkono
imekuwa sababu ya NEC, kuchelewa kufanya uhakiki wa daftari la kupigia
kura kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Usikose kuangalia Movies mbalimbali kutoka kila kona ya dunia, bofya kwenye picha iliyopo hapo chini kuona izo muvies