Baada ya vifo vya wakimbizi kutoka Burundi kufikia 40, Serikali imelazimika kuongeza idadi ya kambi za wakimbizi ili kupunguza msongamano Nyarugusu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Isaac Nantanga alisema jana kuwa hali iliyopo kwenye Kambi ya Nyarugusu siyo ya kuridhisha, maana mpaka sasa wagonjwa wa kipindupindu wanafikia 7429 na watoto wenye utapiamro idadi yao ikizidi kuongezeka.
Alisema wakimbizi waliopo kambini ni 29,145 na ambao hawajaingia wakiwa katika uwanja wa Lake Tanganyika ni 4,729
Nantanga alisema Serikali imelazimika kuongeza kambi moja katika eneo hilo litakaloitwa Nyarugusu 2.
Alisema wameshaanza kuwahamisha wakimbizi kutoka kwenye uwanja huo chini ya uangalizi mkali.
“Tumebaini wakimbizi wanabanana sana kwenye kambi moja, kuna wengine wajawazito, wagonjwa wa kipindupindu, hivyo tumelazimika kuongeza kambi ya pili,” alisema Nantanga.
Alisema Serikali inashirikiana na Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) kuhakikisha huduma za chakula na matibabu zinapatikana.
Nantanga alisema kuhusu suala la ulinzi, Serikali imejipanga kuhakikisha hakuna uhalifu wowote utakaotokea kambini hapo.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Steven Kebwe alisema wanashirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhakikisha wanapeleka timu ya wataalamu maeneo ya Kagunga na Nyarugusu kufanya tathmini na kutoa elimu ya afya.