Featured

    Featured Posts

    Social Icons


Loading...

HIKI NDICHO ALICHOKISEMA ZITTO KABWE HUKO MTWARA

Naomba nikushirikishe na wewe pia kwamba kuna mambo mengi na mazuri ndapi ya picha iliyopo hapo chini ibofye uone.

hotuba ya kufunga mwaka ya Mhe: Zitto Kabwe (Mb), wakati wa mkutano wa pamoja wa hadhara na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, mjini Mtwara (31/12/2014).

Ndugu Profesa Ibrahimu Lipumba
Mwenyekiti wa Taifa wa CUF,
Ndugu Viongozi mbalimbali mliopo hapa leo,
Ndugu Wananchi
Mtwara Hakiii
Mtwara kuchele? Mtwara kumekucha?
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, nashukuru sana kwa mwaliko wako kuja kuzungumza na watu wa Mtwara na kujumuika nao katika kufurahia mafanikio makubwa waliyoyapata katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Nakushukuru kwa kipekee kwa upendo wako kwangu. Umekuwa mlezi wangu kisiasa na kimaisha. Hata pale nilipopitia mikiki mikiki na mihemko ya kisiasa, kamwe hukunikatia hukumu, bali uliona namna bora zaidi ya kunijenga kiuongozi. Wakati baadhi ya watu wakiandikia tanzia yangu ya kisiasa, uliniita na kufuturu nawe nyumbani kwako ukiwa katika moja ya sunna zako unazofunga kila wiki. Nakushukuru sana sana, na ninaomba uendelee kunilea katika maisha yangu ya kisiasa, kifamilia, kijamii na hata kitaaluma. Ukiwa mbobezi wa kimataifa katika taaluma ya uchumi nami nafuata nyayo zako, nataka nipite humohumo ulimopita na inshallah na hata zaidi.

Ndugu wananchi,
Ni kwa sababu ya upendo wa Profesa Lipumba kwangu nilishindwa kukataa kukubali mwaliko wake kuja hapa kujumuika nanyi katika siku hii muhimu sana. Hakuna namna bora zaidi ya kushukuru zaidi ya kuendelea kufanya kazi pamoja katika kuwatetea Watanzania na Tanzania yetu. Umoja wa upinzani ndio silaha dhidi ya mabwenyenye wa kiuchumi na kisiasa hapa nchini. Najua huko waliko inawauma sana wanapoona wapinzani wanaungana bila kujali tofauti ndogondogo zinazojitokeza miongoni mwao. Tutaendelea kushirikiana kwa maslahi mapana ya nchi yetu na katika kuhakikisha kwamba utawala wa Chama cha Mapinduzi ambacho sasa ni chama cha mabwenyenye unakoma katika nchi yetu mapema iwezekanavyo.

Nimekuja pia Mtwara kwa sababu huu ni Mkoa wa kipekee katika historia ya nchi yetu. Mtwara ni Mkoa ambao kwa miaka zaidi ya miaka 25 baada ya nchi yetu kupata uhuru ulibaki kuwa ngome imara dhidi ya mabeberu wa Kireno na waasi wa nchi jirani ya Msumbiji. Wakati mikoa mingine ikisonga mbele katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Mikoa ya Mtwara na Lindi ilibaki nyuma kwa sababu ya kulinda heshima ya mipaka ya nchi yetu. Hii ni historia muhimu sana ambayo vijana wetu inabidi waijue na waithamini.

Katika miaka ya hivi karibuni Mkoa wa Mtwara umechukua sura mpya kabisa kitaifa kufuatia kugunduliwa kwa gesi. Na katika hili wananchi wa Mtwara mmeonyesha kwamba watanzania wanaweza kupigania maslahi ya Taifa wakiamua. Mmesimama kidete kuhakikisha kwamba utajiri huu hauporwi na kwamba haturudii makosa yaliyofanyika Kanda ya Ziwa pale tuliporuhusu madini kuporwa na mabeberu wa kimagharibi kwa msaada wa mabwenyenye uchwara nchini mwetu. Nyie wananchi wa Mtwara mmesimama kidete katika kulinda maliasiali hii iliyogunduliwa kwa niaba ya wananchi wenzenu nchi nzima ya Tanzania.

Najua bado mnalia kuhusu Bomba la kupeleka Gesi Asili Dar es Salaam. Machozi yenu yatafutika tu kwani tayari habari za ufisadi mkubwa katika ujenzi wa Bomba hili zimeanza kuchomoza. Kiongozi wa Upinzani Bungeni ametamka mara kadhaa kuwa atatoa hoja kuhusu ufisadi katika ujenzi wa Bomba la Gesi. Sisi wengine, pale atakapohitaji msaada wetu, tutamsaidia kwani tunaamini gharama za mradi huu zimezidishwa mara mbili na inawezakana kabisa kuwa zaidi ya dola za Marekani 600 milioni

zimegawanywa kwa watu kama rushwa kuanzia Uchina mpaka hapa Tanzania. Machozi yenu wana Mtwara yatafutwa tu, kwa uwezo wa mola.
Kwa hiyo kwangu mimi Mtwara ni alama ya harakati za kupigania haki za wananchi kumiliki, kuendesha na kufaidika na mali asili za Taifa. Tutaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha kwamba utajiri unaoendelea kugunduliwa hapa Mtwara na Tanzania kwa ujumla unasaidia wananchi katika kuboresha maisha yao, elimu zao na kumaliza umaskini.

Mimi kama mwana michezo na ambaye napigania maendeleo na mafanikio ya timu za hapa nyumbani Tanzania, niwapongeze pia wana Mtwara kwa sababu ya timu yenu ya mpira ya Ndanda FC ambayo imeleta changamoto sana kwenye maendeleo ya soka nchini kwetu. Napenda kuitakia kheri timu yenu ya Ndanda FC katika mashindano ya Ligi Kuu ya Tanzania yanaendelea hivi sasa.

Ndugu Wananchi,
Imekuwa baraka na neema sana kufunga mwaka huu hapa Mtwara, ikiwa ni alama ya harakati za mapambano dhidi ya mabeberu na vibaraka wao popote walipo. Mtwara ni uwanja wa mapambano ya uwajibikaji na demokrasia. Ndio maana nasema imekuwa neema na baraka kufungia mwaka huu hapa. Kama Mwalimu Nyerere alivyotanagza Azimio la Arusha mwaka 1967 katika kujenga Nchi ya kijamaa, wana mabadiliko wote nchini wanapaswa kutangaza Azimio la Mtwara la Uwajibikaji katika Uvunaji wa Maliasili ya Nchi yetu.

Mwaka huu tunaouaga leo ulianza kwa matumaini makubwa sana kwa Taifa letu katika kupata Katiba Mpya ilitayozamiwa kuweka misingi imara zaidi ya Uwajibikaji wa Serikali kwa Wananchi. Bahati mbaya mwaka umemalizika kwa kubwaga chini mioyo ya Watanzania wengi sana baada ya kupata Katiba Inayopendekezwa yenye mambo yale yale yaliyotufikisha hapa tulipo zaidi ya nusu karne tangia tupate Uhuru. Hatutakubali nchi yetu irudi nyuma katika maendeleo ya demokrasia na kuruhusu watu wachache wapore uhuru wa wananchi kwa maslahi yao na vyama vyao vilivyogeuka mapango ya uporaji wa mali asili zetu kupitia mabeberu wa kimagharibi na vibaraka wao. Hatutakubali katiba mpya kwa jina. Hatutakubali mvinyo huohuo katika chupa mpya na muda ukifika tutawaambia namna ya kuikataa katiba hii inayopendekezwa. Busara inataka kura ya maoni ifanyike baada ya Uchaguzi Mkuu, lakini wakiileta tukusanye nguvu zetu zote kuikataa Katiba Inayopendekezwa.

Ndugu Wananchi,
Mwaka 2014 unaisha kwa hasira. Tumeshuhudia Bunge letu likijadili moja ya kashfa kubwa kabisa kupata kutokea katika nchi yetu. Zaidi ya shilingi Bilioni mia tatu zimechotwa na kugawaiwa kama njugu tena na watu wenye mamlaka na waliopewa heshima kubwa na umma. Hakuna kashfa kubwa kama wizi uliofanyika kupitia Akaunti ya Tegeta Esrow. Ni wizi mkubwa na tumewakamata wezi mchana kweupe kabisa. Nawakikishieni kwamba juhudi zinazoendelea kufanywa na baadhi ya wezi wa fedha hizi na vibaraka wao zitashindwa vibaya kwa sababu ukweli haujawahi

kushindwa. Watashindwa kwa aibu. Na mimi nawashauri wanyamaze na wakubali yaishe kwa sababu wataumbuka zaidi wakiendelea na ujasiriamali wao wa kupika uwongo barabarani. Kilichofanyika bungeni katika Mkutano wa 16 na 17 uliomalizika mwezi Novemba mwaka 2014 kimeonyesha namna ambavyo umoja ni nguvu. Wabunge wote bila kujali itikadi za vyama vyao walisimama kidete katika kuhakikisha kwamba maazimio yaliyopendekezwa na Kamati ya PAC yanatekelezwa kikamilifu.

Somo moja tunalojifunza ni kwamba tukishirikiana hakuna linaloweza kushindikana katika kupigania maslahi ya taifa letu pendwa la Tanzania. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni ushahidi tosha wa faida za kushirikiana. Wananchi pia wameonyesha hasira zao dhidi ya Wizi wa fedha za Umma kupitia uchaguzi huu.

Katika shilingi bilioni 306 zilizokuwa na zilizopaswa kuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow kuna fedha za Umma. Serikali inasema hazikuwa 306 bilioni bali 202 bilioni! Hii sio hoja ya msingi. Hoja ya msingi ni kwamba hata zingekuwa bilioni moja, bado ndani yake kuna fedha za umma na ilipaswa utekelezaji wa hukumu ya kupunguza kiwango cha tozo ya uwekezaji kufanyika ili kujua kiasi cha fedha za umma.

Tapeli Harbinder Singh Seth alilipwa hizo zilizokuwemo katika akaunti na akaendelea kulipwa bakaa na TANESCO kiasi kwamba shirika hili linalofilisika linamlipa kila siku bwana huyu shilingi milioni 400. Kila siku inayokwenda kwa mungu tunamlipa mtu ambaye hajawekeza hata senti tano nchini mwetu. Alikuja na briefcase tu. Kule Kigoma kuna neno jipya siku hizi, linaitwa umazwazwa. Ni kama ujuha hivi. Huu ni umazwazwa ambao wananchi hawapaswi kuukubali.

Watu watatu tu ambao ni raia wa kigeni walichora wizi huu kwa miaka mitatu. Mtu mmoja anaitwa Bwana Baharuddin kutoka Malaysia, Bwana Issa Ruwaih kutoka Oman na Bwana Singh kutoka Kenya na anaishi Afrika Kusini.
Walidanganya nyaraka za kuuziana makampuni, bwana Baharuddin akauza hisa za IPTL kutoka Mechmar kwenda kwa Bwana Issa wa kampuni ya PiperLink na Bwana Issa naye akauza hisa hizo zikiwa zimezuiwa na Mahakama kwa Bwana Seth wa kampuni PAP.

Mabwana hawa wanajua Watanzania ni mazwazwa na hawafanyi uchunguzi wa kina, yaani ‘due diligence’ kwani hata kwenye EPA fedha ziliibiwa kwa kutofanya due diligence na kwa kutumia kitu kinaitwa ‘deed of assignment’.
Mabwana hawa wanajua kuwa Watanzania wenye ofisi za umma wana njaa na watawahonga kidogo tu na kupitisha kila kitu. Ndivyo ilivyofanyika.
Kama viongozi wetu wangefanya ‘due diligence’ kwenye manunuzi ya makampuni haya kama Sheria ya Kodi ya Mapato inavyowataka, tusingekuwa na skandali ya Tegeta Escrow.

Mfumo uliganzishwa kwa rushwa. Ukitazama miamala ya malipo kutoka akaunti ya Bwana Seth katika akaunti ya StanBic utaona fedha zimekwenda benki za UAE na baadaye Oman na Malaysia. Fedha hizo zilikwenda kuwalipa mabwana Baharuddin na Issa.

Serikali lazima ichukue hatua mara moja kuhakikisha fedha zilizokuwamo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zinarudi, uamuzi wa mahakama ya kimataifa unatekelezwa na fedha za umma zinarejeshwa TANESCO na zile za binafsi zinalipwa kwa wamiliki halali. Tanzania haiwezi kuwa nchi ya kubariki utapeli wa kimataifa na kuchafua sura ya nchi yetu mbele ya jamii ya kimataifa.

Baraza la Taifa yaani Bunge, kupitia wawakilishi wa wananchi, tayari wameamua na kupitisha maazimio. Kilichobakia ni maazimio hayo kutekelezwa na Serikali. Hakuna mjadala katika maazimio ya Bunge, maana katika maazimio hayo Serikali nayo imo; ilishiriki kikamilifu katika kuyandaa na hatimaye kupitishwa na Bunge. Hakuna namna ya kukwepa kutekeleza maazimio ya Bunge kwa ukamilifu wake; nasema hakuna, ni utekelezaji tu.

Ndugu Wananchi,
Nataka niwambie watanzania kupitia mkutano huu muhimu wa Mtwara kwamba yaliyotokea Bungeni ni mwanzo na si mwisho. Ni mwanzo wa safari ndefu wa kujenga utamaduni wa uwajibikaji katika nchi yetu.

Dhana ya Uwajibikaji ni dhana inayotaka kila kiongozi kuwajibika kwa matendo yake katika utekelezaji wa shughuli za umma. Ni dhana ambayo ni lazima kuienzi kama tunataka nchi yetu ibakie salama na yenye utulivu kwani kukosekana kwa uwajibikaji kunaleta rushwa na ufisadi. Tusikubali watu wachache kwa maslahi yao binafsi waendelea kuharibu heshima ya nchi yetu. Tusikubali kamwe.

Ufisadi unarudisha nyuma maendeleo, unaleta umasikini, unaleta vita na umwagaji damu. Ndio maana ni lazima kuimarisha taasisi za uwajibikaji katika nchi yetu. Kufukuza mawaziri wanaposhindwa kutekeleza wajibu, japo haitoshi, sio udhaifu bali ni mchakato wa kuimarisha taasisi za Uwajibikaji na kukuza demokrasia kwa ujumla. Mwalimu Nyerere alituasa kwamba cheo ni dhamana. Ukipewa heshima ya kuongoza lazima ujiheshimu, ukishindwa kujiheshimu lazima uondoke, kwa hiari au kwa kulazimishwa.

Waziri Mkuu mstaafu, Mzee wangu, Jaji Joseph Warioba, alipata kunihadithia alivyojiuzulu wadhifa wake huo mwezi Machi mwaka 1990. Rais Mwinyi alihutubia Taifa kuingia mwaka mpya wa 1990 kwamba rushwa imeshamiri ‘mpaka muuza njugu anaombwa rushwa’. Wizara takribani nane zikahusishwa na rushwa ikiwamo Wizara ya Sheria (mahakama), Wizara ya Mambo ya Ndani (uhamiaji na polisi) na Wizara ya Ardhi.

Mawaziri hawa nane walipaswa kuwajibika kwa kujiuzulu, lakini Mzee Warioba aliona hiyo ni takribani nusu ya Serikali akamwomba Rais ajiuzulu yeye ili Serikali mpya iundwe. Baada ya majadiliano marefu Mzee Mwinyi akakubali na akalitaka Baraza zima la Mawaziri kujiuzulu. Lote kabisa.

Akaunda upya Serikali, akamrejesha Warioba kama Waziri Mkuu lakini akaondoa baadhi ya mawaziri. Mwaka 1990 ulikuwa mwaka wa Uchaguzi, lakini Mzee Mwinyi hakusita kuunda upya Serikali. Maamuzi hayo ndio yaliyomwingiza kwenye Baraza la Mawaziri ( kama Waziri Kamili) Meja (wakati huo) Jakaya Mrisho Kikwete ambaye sasa ni Rais wa Jamhuri yetu. Hivyo Rais akifanya leo sio jambo jipya. Uwaziri sio usultani, ni dhamana tu ya kuongoza sehemu ya idara za Serikali.

Ndugu Wananchi,
Ni katika nchi ya Tanzania pekee ambapo waziri anaweza kutukana wananchi waziwazi mchana kweupe na kuwaambia kwamba ni wajinga na wapumbavu na akabaki katika ofisi ya Umma. Ni Tanzania tu ndipo Katibu Mkuu wa Wizara anaweza kutukana wabunge kuwa ni washenzi akaachwa bila kuchukuliwa hatua za kinidhamu. Huwezi kuwa na Taifa lisiloheshimu wananchi na wawakilishi wao. Uwajibikaji ni suluhisho. Uwajibikaji unaweka nidhamu. Uwajibikaji unatoa matumaini kwa watu kuwa viongozi wao wanawajali.

Mwenyezi Mungu ameweka utajiri wa nchi yetu wa mafuta na gesi asilia kwenye mikoa ya Pwani na Kusini. Mikoa mingine pia mungu amejaalia utajiri. Kanda ya Ziwa kuna dhahabu na almasi, nyanda za juu makaa ya mawe, Kaskazini Mlima Kilimanjaro na Tanzanite na kadhalika. Hata hivyo katika dhahabu yote iliyochimbwa na kuuzwa nje ya thamani ya dola za kimarekani bilioni 13 kati ya mwaka 1998 na mwaka 2013, yaani miaka 15, nchi yetu ilipata mapato ya dola za Kimarekani 650 milioni tu, sawa na asilimia tano.

Naomba kurudia. Kwa miaka 15 ambayo dhahabu yetu ilichimbwa na kuuzwa, Watanzania tumepata shilingi tano tu katika kila shilingi 100 ! Shilingi 95 zote zimekwenda kwa wageni. Kama sio umazwazwa ni nini?

Yote ni kwa sababu ya mikataba ya siri yenye makosa makubwa na yenye kupendelea wawekezaji. Tunataka mikataba ya gesi iwe wazi kabla ya uvunaji mkubwa kuanza ili kama kuna makosa turekebishe. Ndiyo maana Kamati yenu ya PAC iliamuru viongozi wa TPDC waswekwe ndani kwa kukataa kuweka mikataba hii wazi kwa wajumbe wa Kamati ili waitathimini kwa niaba ya wananchi.

Hatutaki viongozi ambao kazi yao ni kuombaomba kwa wawekezaji ili kuwasaidia katika miradi yao ya kisiasa. Tunataka, kwa mfano, mtu kama DANGOTE anapowekeza hapa Mtwara, watu wa Mtwara na Watanzania wafaidike na sio wanasiasa. Kuomba omba rushwa kunatia doa heshima yetu mbele ya mataifa ya ulimwengu.

Ndugu Wananchi,
Tunaingia mwaka 2015 kifua mbele katika vita dhidi ya ufisadi na katika kusimika uwajibikaji nchini. Tunataka Watanzania wote wenye uzalendo kwa nchi yao kuungana na vyama vya upinzani katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji nchini kwetu. Kwa upande wa Kamati ya PAC tunawahakikishia utendaji uliotukuka zaidi. Katika Bunge la mwezi Januari, mkutano wa 18 moja ya jambo tutakalolitolea taarifa ni ukwepaji mkubwa wa kodi katika mauzo ya Korosho nje ya nchi, uagizaji holela wa Sukari na nguo. Fuatilie Bunge hili kwa makini.

Tunautangaza Mwaka 2015 kuwa ni mwaka wa kuwajibishana. Uwajibikaji unahitajika zaidi mwaka 2015 kuliko wakati mwingine wowote katika miaka mitano iliyopita. Tuungane kuhakikisha Serikali inawajibika kwa wananchi badala ya kuweka mipango ya kuchakachua uchaguzi.

Lakini nimalizie kwa kusema wazi wazi kwamba kujaribu kuiajibisha serikali ya CCM kupitia Bunge ni kazi kubwa na ngumu mno. Hawa watu ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa. Hawasikii. Hawaoni. Hawaambiliki. Wameshazibwa mifumo ya fahamu. Hiyo ndiyo hatatari ya rushwa na ufisadi. Yote tunayoyafanya bungeni na nje ya Bunge kama wapinzani ni mambo ya muda mfupi. Suluhu ya kudumu ya uwajibikaji kwa serikali ya CCM mnayo ninyi wananchi. Nami nawaomba mtusaidie muda ukifika mwakani mchukue HATUA kupitia kura zetu.

Hakuna tena muda wa kuwachekea hawa CCM. Tuwaweke pembeni na hili linawezekana kwa sababu tayari mmeshaonyesha kwamba mnaweza kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa. Tunapouanza mwaka mpya, kila mwenye mapenzi ya kweli ya nchi hii aungane na kufanya kazi pamoja na kwa bidii katika kuijenga Tanzania bora kwa kila Mtanzania. Tanzania imara, yenye kujali haki na utu wa raia wake na yenye demokrasia na uwajibikaji inawezekana. Tuchukue hatua sasa!

Namshukuru tena ndugu yangu, mjomba wangu Profesa Ibrahimu Lipumba, msomi mwana mapinduzi, kwa fursa hii adimu.
Asanteni sana kwa kunisikiliza
… Hakiiii….



Kwa habari za Matukio Kitaifa, Kimataifa, Michezo na Burudani, Ungana nami kupitia Link zifuatazo hapo chini.

    
In order you follow me just click one of the Icon Button above.
Usikose kuangalia Movies mbalimbali kutoka kila kona ya dunia, bofya kwenye picha iliyopo hapo chini kuona izo muvies
Nobody is a total failure if he dares to try to do something worthwhile. Tough times never last, but tough people do. The place broke up with applause. Those thirty - five hundred farmers who had lost hope and had battled depression found that hope.

Share habari hii kadri uwezavyo.

Contact us on mutalemwa.oesmo@gmail.com. Powered by Blogger.
© Copyright Mutalemwa Blog
Back To Top