Shirikisho la Soka (TFF) limedai linachunguza kitendo cha klabu ya Azam FC kumsajili kiungo Frank Domayo wakati akiwa kwenye kambi ya timu ya taifa mjini Mbeya.
TFF imedai imemuagiza Wakili Wilson Ogunde kuchunguza tukio hilo kwa kile kinachoelezwa kuwa kambi ya timu ya taifa ina miiko yake.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa shirikisho hilo linampa siku 14 wakili Ogunde awe ameshachunguza tukio hilo na kuwapa ushauri wa kisheria na hatua za kufuata.
“Wakili Ogunde ataangalia mlolongo mzima wa tukio na kanuni za maadili kuhusu suala hilo, kanuni za usajili zinasemaje na tutafanyia kazi bila kumuogopa mtu wala kumuonea mtu kwa kumchukulia hatua stahiki.
“Hakuna ‘Mungu Mtu’ kwenye mpira wala klabu, yeyote aliyehusika na tukio lile tutamchukulia hatua za kinidhamu.
Kambi ya timu ya taifa inatakiwa iheshimiwe, ina miiko yake na wahusika wote waliohusika kwenye tukio hilo tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria na ushauri utakaotolewa na wakili tuliyempa jukumu hilo, ndani ya siku 14 mtajua ni hatua gani tutazichukua,” alisisitiza.
Kwa kawaida, mchezaji anatakiwa achukuliwe hatua kwanza na uongozi wa timu na iwapo hautachukua hatua, basi suala lake linapelekwa kwenye kamati husika kwa hatua za kinidhamu.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, wakili wa TFF, Alex Mgongolwa alisema: “Kama Azam wamemsajili Domayo akiwa na mkataba na Yanga kama Domayo hana mkataba na Yanga, hakuna kesi, ila kuna kingine cha maadili ambacho kinaweza kutengua usajili wa Azam kulingana na kanuni inavyoeleza.”
Jiunge na mi kwa kubonyeza kwenye link zifuatazo chini ili kupata habari mpya zaidi.
FACEBOOK >>> TWITTER >>> MATUKIO KWA NJIA YA SAUTI