Mtu mmoja amefariki dunia na wengine watatu kunusurika baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kutoka kwenye mashamba ya mwani kupigwa na mawimbi na kuzama baharini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Shekhan Mohammed Shekhan amemtaja aliyekufa kuwa ni Mariam Makame Hassan (50) mkazi wa Tumbe, Wilaya ya Micheweni Pemba.
Kamanda Shekhan amewataja walionusurika kuwa ni Salama Hamad, Rehema Abdallah Ali na Haji Faki Haji.Alisema tukio hilo lililotokea mchana katika eneo la bahari karibu na Mto Kiwawali.
Tulipata taarifa za mtu mmoja kufariki dunia kutokana na mtumbwi kuzama,” alisema Shekhan na kuongeza
:“Tulikwenda eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
”Kamanda Shekhan amewataka wananchi hasa wakulima kuchukua vifaa vya uokozi wakati wanapokwenda kwenye shughuli za kilimo.
“Ajali hii itufundishe kuwa makini, lazima tubebe vifaa vya kutusadia wakati yanapotokea matatizo au hatari ya kuzama kwa vyombo vya usafiri baharini,” alisema Kamanda Shekhan.
Amesema kuwa kutokana na shughuli za kilimo cha mwani kufanywa zaidi na wanawake, ni vizuri kuchukua vifaa vya uokozi na kufuatana na wanaume.
“Nawaomba wakulima kuchukua vifaa vya uokozi wanapokwenda kwenye shughuli zao ikiwa ni pamoja na kufuatana na akinababa ili kusaidia inapotokea hatari,” alisisitiza Shekhan.
Aliwataka wanaume kushirikiana na wanawake wanapokwenda shambani ili kutoa msaada wa haraka linapotokea tatizo.Mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi Hospitali ya Micheweni na kubainika kifo chake kilitokana na kunywa maji mengi.
Baadhi ya wananchi wa Tumbe wameziomba kampuni zinazonunua zao la mwani kuwasaidia vifaa vya uokozi.