Morogoro. Mwanamke aliyetambuliwa kuwa ni Mariamu Said mkazi wa Kiwanja cha Ndege, Morogoro juzi alishushiwa kipigo na wananchi kutokana na kumficha mtoto wa marehemu mdogo wake kwenye boksi kwa miaka minne.
Tukio hilo lilitokea juzi saa nne asubuhi baada ya majirani zake kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Dia Zongo kuhusu mtoto huyo, Nasra Rashid, kufichwa ndani ya boksi tangu akiwa na umri wa miezi tisa.
Zongo alisema majirani hao walimweleza pia kuwa jirani yao huyo hamfanyii usafi mtoto huyo wala kumtoa nje.Baada ya kupata taarifa hizo, Zongo alimtafuta Mwenyekiti wa Mtaa huo, Tatu Mgagala na kuongozana naye hadi kwenye nyumba hiyo na kumhoji mwanamke huyo ambaye alikuwa akijibu kwa kubabaika.
Moja ya maswali aliyoulizwa ni idadi ya watoto wake na akajibu kuwa ana wawili lakini wakati akiendelea kujibu maswali, ghafla mtoto huyo alipiga chafya na kuanza kukohoa, hivyo kuwapa wasiwasi na kuamua kuingia chumbani kwa mwanamke huyo kwa nguvu na kumkuta mtoto Nasra akiwa ndani ya boksi.
Ofisa mtendaji huyo alisema wakati wakimtoa mtoto huyo ndani ya nyumba, kundi kubwa la watu waliokuwa na fimbo na mawe walianza kumshambulia mwanamke huyo na kumlazimu mtendaji kutoa taarifa polisi.
Alisema muda mfupi baadaye, polisi waliwasili na kumkamata Mariam na kumpeleka katika ofisi ya kata ambako aliwekwa chini ya ulinzi.Baadaye aliwekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi, Morogoro na mtoto alipelekwa Ofisi za Ustawi wa Jamii.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alisema wanaendelea kukusanya taarifa za tukio hilo ikiwamo matokeo ya vipimo vya madaktari kuhusu afya ya mtoto huyo kabla ya kuchukua hatua zaidi.Kamanda Paulo alisema watuhumiwa hao wanashikiliwa kwa kosa la kumfanyiwa mtoto vitendo vya kikatili.Hata hivyo, kamanda huyo alisema polisi wanakadiria kwamba mtoto huyo alianza kufichwa kwenye boksi hilo akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu.
Akijibu maswali ya polisi, mwanamke huyo alikiri kuanza kumlea mtoto huyo tangu akiwa na umri wa miezi tisa baada ya mama wa mtoto huyo kufariki dunia mwaka 2010.
Pia mtuhumiwa alikiri kwamba mtoto huyo hajawahi kupewa chanjo yoyote wala kupelekwa kliniki. Alikuwa akitoa maelezo hayo huku akiwa amemshikilia mtoto huyo aliyetapakaa uchafu ikiwamo haja kubwa na ndogo alizokuwa akitoa ndani ya boksi na kusema kwamba mara ya mwisho alimwogesha Julai mwaka jana.
Pia alisema alikuwa akimwekea chakula na maji ndani ya boksi lililokuwa nyuma ya mlango wa chumba. Mume wa mwanamke huyo, Mtonga Ramadhani anayefanya biashara katika Soko la Mawenzi, Morogoro ambaye pia anashikiliwa na polisi, alidai kuwa hakuona sababu ya kutoa taarifa za kufichwa kwa mtoto huyo kwa sababu hamhusu na wajibu wake ni kutafuta chakula.
AlivyonaswaBaadhi ya majirani wa mwanamke huyo ambao hawakutaka kutajwa majina, walisema Mariam alihamia katika nyumba hiyo mwaka 2010 na hawajawahi kumwona mtoto huyo akitolewa nje wala kufanyiwa usafi.
Walisema mtoto huyo alibainika baada ya kusikika akikohoa na kulia nyakati za usiku, jambo lililozua wasiwasi kuwa huenda mtuhumiwa alikuwa mshirikina anayefuga misukule.Baba wa mtotoBaba mzazi wa mtoto huyo, Rashid Mvungi alisema hakujua kama mwanaye alikuwa analelewa katika mazingira hatarishi.
Akihojiwa na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu, Mvungi alisema alimzaa mtoto huyo nje ya ndoa na amekuwa akituma fedha za matumizi kwa mama yake mkubwa.
Mvungi ambaye ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, alisema baada ya mzazi mwenzake kufariki dunia alishindwa kumchukua mtoto wake kwa sababu tayari alishakuwa na mke.
Alisema hata hivyo, alikubaliana na upande wa familia ya marehemu kuwa mtoto huyo alelewe na mama yake mkubwa. Mtoto azungumzaWakati Mvungi akihojiwa, baadhi ya watu waliofurika katika Ofisi za Ustawi wa Jamii walianza kuangua kilio baada ya mtoto huyo anayeonekana mlemavu kuanza kujibu maswali aliyokuwa akiulizwa na maofisa wa Ustawi wa Jamii.
Swali: Unaitwa nani:
Jibu: Naitwa Nasra
Jibu: Naitwa Nasra
Swali: Ulikuwa unapewa chakula gani?
Jibu: Ubwabwa na maharage
Swali: Una umri wa miaka mingapi?
Jibu: Miaka minne
Swali: Baba yako yuko wapi?
Jibu: (anamwonyesha kwa kidole)Ngungamtitu alisema huenda ulemavu wa mtoto huyo umetokana na kuishi kwenye boksi au kukosa lishe yakiwamo maziwa ya mama, hewa safi na upendo.
Alisema si ajabu mtoto huyo kushambuliwa na magonjwa mbalimbali kama minyoo, pneumonia, utapiamlo na malaria, ndio maana aliagiza apelekwe katika Hospitali ya Mkoa kwa uchunguzi, chanjo na tiba.
Ofisa huyo alisema matibabu mengine atakayopatiwa ni pamoja na kunyooshwa viungo, mikono na miguu iliyolemaa.Ngungamtitu aliwaomba wasamaria wema, mashirika ya dini na wadau mbalimbali kutoa misaada ya nguo, lishe, matibabu na mahitaji mengine kwa mtoto huyo.