Mafia ni moja ya wilaya zilizoko mkoani wa Pwani. Shughuli nyingi za kiuchumi katika wilaya hiyo zinategemea uvuvi, kilimo cha nazi pamoja na utalii. Hata hivyo shughuli hizo hazijaweza kuondoa hali duni ya maisha ya watu wake.Mafia ina wakazi wapatao 46,000, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.
Wakazi wa wilaya hiyo walio wengi wanakula mlo mmoja kwa siku, hii inatokana na wengi wao kutegemea uvuvi wa samaki pekee, ambao kwa bahati sasa ni vigumu kuwavua kutokana na kuwepo kwa sheria mbalimbali zinazowazuia wageni kuvua wanavyotaka kama ilivyokuwa zamani.
Baadhi ya wakazi wanasema zamani kulikuwa hakuna ulazima wa kuomba kibali, lakini sasa mvuvi anapaswa kuomba kibali, huku pia kukiwa na sheria kali za kumwongoza mvuvi wapi pa kuvua au wapi pa kutovua.
Kwa sasa wilaya hiyo ina kiwanda kimoja cha minofu ya samaki. Wakati kinajengwa, wananchi wengi wanamini kwamba wangepata ajira, hata hivyo ukweli ni tofauti, kiwanda kina uwezo mdogo sana wa kutoa ajira.Mkurugenzi wa Wilaya ya Mafia, Fransic Namaumbo anasema kiwanda hicho cha Tanpesca kinachangia Sh8.4 milioni kwa mwezi katika wilaya hiyo kwa mwaka kama kodi.
Shughuli za uvuviNa maumbo anasema uvuvi wa samaki kwa ujumla unachangia pato kwa wilaya hiyo Sh129 milioni.Kulingana na kiongozi huyo wastani wa kipato cha mkazi wa Mafia kwa siku ni Sh1,350, kiasi ambacho baadhi ya wananchi wanapingana nacho wakisema kuwa kwa namna wanavyoona, wananchi wengi wana kipato kidogo zaidi ya hicho.
Wananchi wengi wanalalamika kwamba viongozi wa wilaya hiyo hawasimamii vizuri rasilimali zilizopo. Wanadai kuwa wanashindwa kuwaongoza vema wananchi kuelekea kwenye mafanikio.
Miundombinu mingi ni duni, huduma nyingi za afya si bora, kiasi kwamba wilaya nzima inategemea hospitali moja tu kubwa ambayo nayo imekuwa ikilalamikiwa kutokuwa na vifaa vya kutosha katika kuhudumia wananchi.
Huduma za afya, elimu, maji safi na salama na barabara ni mojawapo ya kero kubwa zilizoko katika Wilaya ya Mafia, huku wenye madaraka wakilaumiwa kutoa ahadi nyingi zaidi kuliko vitendo. Baadhi ya wafanyakazi wanaopangwa kufanya kazi Mafia kutoka mikoa mingine, hukimbia, kutokana na miundo mbinumingi kuwa duni.