Siku kama ya leo mwaka 1996, ilikuwa ni vilio kila kona ya nchi, lakini Kanda ya Ziwa iliathirika zaidi na kuzama kwa meli ya Mv Bukoba na kuteketeza mamia ya wananchi. Kuzama kwa Mv Bukoba inaelezwa ni kutokana na kuwa ubovu.
Tukio hilo ambalo haliwezi kufutika vichwani mwa wakazi wa Kanda ya Ziwa, lakini kilio chao cha kupatiwa meli mpya licha ya Rais Jakaya Kikwete kuahidi Serikali kununua mwaka 2010, haijanunuliwa hadi sasa.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa ujenzi wa meli hiyo mpya iliyoahidiwa na Rais Kikwete kwa Ziwa Victoria unatarajia kukamilika mwaka 2016. Akizungumza ofisini kwake wiki hii, Ofisa Masoko wa Huduma za Meli Mwanza Obedi Nkongoki alisema mjenzi wa meli hiyo Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Denmark (Danida) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
“Ujenzi huu unahusisha meli nne ingawa Rais aliahidi tatu; Ziwa Victoria moja, mbili Ziwa Tanganyika na nyingine Ziwa Nyasa ambazo zinatarajiwa kukamilika 2018, huku ya Ziwa Victoria ikitarajiwa kukamilika 2016,” alisema Nkongoki.
Alisema meli mpya itakuwa na kasi kwa kutumia saa tano kwenda Bukoba na kurudi Mwanza, itakuwa ikifanya kazi mchana badala ya usiku pekee, ikibeba wastani wa abiria ni 500 na tani 56 za mizigo.
Gharama hazitakuwa kubwa zaidi na haitakuwa tofauti na mabasi ila zitazingatia soko na bei ya mafuta,” alisema Nkongoki na kuongeza:“2016 itapatikana meli mpya, hapo tutaanza ukarabati wa meli za Serengeti na Victoria, baadaye tutaifanyia ukarabati meli ya Umoja, ambao utaziweka katika hali nzuri na zitakazokwenda na wakati.
Tunalenga kujiimarisha kiuchumi kwa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo, Uganda, Zambia, Rwanda na Malawi.”Alisema meli zinazohudumu zilitengenzwa mwaka 1938 na kwamba, ambayo inaonekana mpya ni ya mwaka 1988, hivyo wamekuwa na uzoefu wa mabadiliko ya meli kulingana na hali ya hewa.
“Hivyo tuna uhakika wa kuepuka ajali, kwani tunajitahidi kufanya ukaguzi mara kwa mara. Pia, tunaajiri wataalamu wenye taaluma ili kuimarisha usalama wa abiria na mali zao,” alisema.Victoria hivi sasa inabeba abiria 1,200 na tani 200 za mizigo, huku Serengeti ikibeba abiria 593 na tani 350 za mizigo.
Hivyo ujio wa meli mpya na ukarabati wa meli zilizopo unatazamiwa kuwa ni mkombozi kwa usafiri Ziwa Victoria.