Kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Omar Simon (30) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kwa tuhuma ya kumlawiti mwanafunzi wa darasa la pili (9), anayesoma katika Shule ya Msingi Kitangili, Manispaa ya Shinyanga, kisha kumtoboa macho kwa kutumia kitu chenye ncha kali na kumuacha porini, akisota kwa muda wa siku mbili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangalla alisema tukio hilo lilitokea Aprili 20, mwaka huu majira ya saa 10;00 jioni katika kitongoji cha Bugweto, nje kidogo ya Mji. Alisema mwanafunzi huyo aliokotwa na wanawake wawili.Kamanda Mangalla alisema siku ya tukio, mwanafunzi huyo ambaye anaishi na bibi yake Kata ya Ibinzamata alipewa Sh 500 na bibi huyo ili apande baiskeli kwenda kwa mama yake mkubwa anayeishi Kata ya Ngokolo.
Mangalla alidai mwanafunzi huyo alipofika katika kituo cha baiskeli, zinazofanya biashara ya kusafirisha abiria, maarufu kama daladala au bodaboda, alikutana na mtuhumiwa Simon, mwendesha daladala ya baiskeli, ambaye alimpeleka katika pori dogo lililoko katika Kitongoji cha Bugweto na kumlawiti na kisha kumtoboa macho kwa kitu chenye ncha kali na kumtelekeza katika eneo hilo bila ya msaada.
“Tangu mwanafunzi huyo atoweke kwao Aprili 20, alikuja kuokotwa Aprili 22, mwaka huu majira ya saa 4;00 asubuhi na wanawake wawili na kumpeleka katika Kituo cha Polisi ambao walimpeleka Hospitali ya Mkoa hadi sasa anaendelea kupata matibabu,“ alisema Mangalla.
Kamanda Mangalla alisema mtuhumiwa tayari amekwishakamatwa na Jeshi la Polisi, na atafikishwa mahakamani wakati wowote kuhusiana na tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, bibi wa mwanafunzi huyo alisema amefungua kesi katika Kituo Kikuu cha Polisi jalada lenye kumbukumbu Namba SHY/ RB/2098/2014 baada ya kuhisi mjukuu wake, amefanyiwa kitendo hicho, kutokana na hali aliyonayo.