Huenda ikaonekana kama siyo muhimu, lakini tafiti zinaonyesha kwamba ni lazima kufahamu aina ya mwenzi unayetaka kuwa naye au tayari unaye.
Moja ya mambo ya msingi kuyajua ni kwamba uliyenaye, kwao ni mtoto wa ngapi? Ni muhimu kujua hilo kwani kitaalamu, kila mtoto ana staili yake ya kwenda naye. Kwa namna ilivyozoeleka, watoto hulelewa tofauti, kulingana na namna walivyozaliwa.
Mfano; kama ni mtoto wa kwanza au wa mwisho, wazazi wengi huwalea tofauti watoto hawa. Naamini tunakubaliana kwamba, mara nyingi watoto wa kwanza hulelewa kwa mapenzi makubwa zaidi, huku wa mwisho wakidekezwa zaidi.
Wale wa kati, mara nyingi hulelewa malezi ya kawaida. Ingawa siyo wote, asilimia kubwa ya watoto wa mwisho uhitaji mzazi kuwa mwangalifu zaidi kwa namna ya kuwalea.
Wakati mwingine hata kusema asante huwa hawawezi hata unaweza kujiuliza inakuwaje, mbona niko na mwenzi, lakini ni kama kila ninapofanya jambo haonyeshi kuridhika au hata kusema asante? Wengine hawezi hata kusema mpenzi au kubusu.
Hili kwa asilimia kubwa huchangiwa na malezi. Watoto wengi wa mwisho siyo wazuri katika makeke, ni vigumu kupendelea vitu kama busu na mambo kama hayo, badala yake wamekuwa ni watu wenye kupenda zaidi kutendewa mazuri.
Mbaya watoto wa mwisho mara nyingi siyo watu wa kujali sana hata uwatendee mazuri kwa sababu walishazoea kutendewa mazuri, kama ilivyozoeleka kwamba wengi huwa wanadekezwa.
Utafiti wa wataalamu mbalimbali unaonyesha kuwa ingawa hatuwezi kusema moja kwa moja kwamba watu waliozaliwa kama watoto wa kwanza au mwisho ndiyo pekee wazuri au la, msingi wa uzuri wa mtu wakati mwingine huchangiwa na wazazi. Kama wazazi hawajui mapenzi ni vigumu watoto kuyajua mapenzi.