Willy Sagnol moja kwa moja kidole chake kilitua kwa Lionel Messi.
Beki huyo wa zamani wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa, amesema Messi ndiye aliyewafungisha Barcelona na kusababisha watolewe na Atletico Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano iliyopita.
Malalamiko ya Mfaransa huyo kwa Messi ni kwamba kwenye mchezo huo aliwafanya wenzake na watu waliokuwa wakimtazama wakitarajia kupata kitu tofauti kuwa ni wajinga.
Sagnol anasema Messi alikuwa anatembea tu uwanjani.
Amzidi kipa tu uwanjaniKwenye mchezo huo uliomalizika kwa Barcelona kuchapwa bao 1-0 na hivyo kutupwa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 2-1, Messi alikimbia kwa kilomita 6.8 uwanjani Vicente Calderon na kuonekana kuwa ndiye mchezaji wa ndani aliyekimbia umbali mdogo zaidi wakati wa mchezo.
Kwa takwimu za mchezaji mmoja mmoja na jinsi walivyoshiriki mechi hiyo, Messi amemzidi kipa tu wa Barcelona, Jose Pinto kwa kilomita 1.4 ikiwa ndiyo tofauti yao kitu ambacho kimetia wasiwasi kutokana na kipa kukimbia kwenye eneo dogo lakini bado hakuzidiwa kwa tofauti kubwa na mchezaji huyo wa ndani, ambaye miaka yote amezoeleka akihaha uwanja mzima.
Kutokana na hilo, staa huyo wa zamani wa Ufaransa, Sagnol anasema Messi alikosa nidhamu kwenye mchezo huo na kucheza kwa kuwategea wenzake kitu ambacho kiliwagharimu sana na kupoteza mechi.
Azidiwa na mfungajiKiungo Mhispaniola Koke ndiye aliamua matokeo ya mchezo huo baada ya kufunga bao maridadi kabisa kwenye mchezo huo, Koke alistahili kuipa timu yake ushindi kutokana na kujituma zaidi uwanjani na kukimbia kwa zaidi ya maili nane ikiwa ni mara mbili ya umbali aliokimbia Messi uwanjani.
Udhaifu wa Messi ndani ya uwanja limedaiwa kuwa ni jambo ambalo kocha Gerardo Martino alishindwa kulipatia ufumbuzi mapema na kuendelea kumwacha staa huyo uwanjani wakati hachezi kwa kujituma na alikuwa mzigo mkubwa ambao hakika umeigharimu sana timu hiyo.
Messi ameripotiwa kuporomoka kiwango chake tangu aliporejea uwanjani kutoka kuwa majeruhi, lakini mfumo wa kocha Martino unadaiwa kuwa tatizo pia kwa staa huyo kuweza kuonyesha makali yake ndani ya uwanja.
Awa butu kwa Atletico
Messi ameshindwa kufunga bao dhidi ya Atletico kwenye mechi tano alizomenyana na timu hiyo na Jumatano iliyopita uwanjani Calderon alikosa nafasi za wazi za kuipatia ushindi timu yao. Hakika Muargentina huyo alikuwa tatizo kwa Barcelona.
Sawa, kwa sasa Barcelona inahitaji kujijenga upya kwenye safu ya ulinzi na kipa, lakini bado Messi alikuwa na kila sababu kuhakikisha anaibeba timu yake akiwa kama staa tegemeo wa kikosi hicho.
Kwa hali ilivyo, kitu ambacho kitaweza kuiokoa Barcelona ni nyota wake kupandisha viwango vyao kufuatia kukabiliwa na adhabu ya kuzuiwa kusajili kwa mwaka mzima.
Mashabiki tayari wameanza presha na chokochoko ya kutaka aletwe kocha mpya huku mchakato huo ukitarajia kushika mvuto zaidi katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa kumpata rais mpya kwenye klabu hiyo.
Barca yachemsha kwa Atletico Kwa msimu huu.
Barcelona imekuwa dhaifu kwa Atletico Madrid. Miamba hiyo miwili imekutana mara tano, lakini mbaya zaidi kwa Barcelona timu ambayo ilizoeleka kuwa mbabe imeteswa sana na kikosi hicho cha kocha Diego Simeone.
Kocha Martino ameshindwa kutegua mtego wa Atletico Madrid. Kwenye mechi tano walizomenyana, Barcelona imeambulia mabao mawili tu na wameshindwa kuibuka na ushindi dhidi ya timu hiyo ya Simeone.
Mechi ijayo baina ya timu hizo itakuwa ya ligi ya ndani na Barcelona sasa itahitaji kushinda kama kweli inataka kutetea ubingwa wake wa La Liga, lakini mambo yanazidi kuwa mabaya kwao baada ya kuchapwa na Granada 1-0 juzi Jumamosi.
Matumaini pekee yaliyobaki kwa klabu hiyo ni kunyakua ubingwa wa Copa del Rey kwa kucheza fainali wiki iliyopita, lakini tayari wapo kwenye wakati mgumu kutokana na beki wao Gerard Pique na kipa wao namba moja Victor Valdes kuwa majeruhi, hivyo wataingia uwanjani wakiwa chamtoto.
Messi ataweza kuibeba Argentina? Kwa mara ya kwanza tangu 2011. Messi alicheza mechi nne bila ya kufunga bao, lakini mbaya zaidi ni ukubwa wa eneo alilokimbia uwanjani Vicente Calderon Jumatano iliyopita. Kuna vitu viwili tu vinaweza kuwa sababu ya kiwango hicho cha Messi, inawezekana alikosa moyo wa kupambana au tatizo la majeruhi limedhoofisha uwezo wake.
Wachambuzi wa masuala ya mpira wa miguu wanadai kwamba huenda Messi akawa anatunza nguvu kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika kuanzia Juni mwaka huu nchini Brazil.
Wachezaji waliofanya hivyoKinapofika kipindi cha Kombe la Dunia, wachezaji wengi wamekuwa wakicheza kwa tahadhari kubwa sana kujilinda ili kwenda kufanya vyema kwenye michuano hiyo.
Wakati Messi akionekana hajitumi uwanjani kwa sasa kutunza nguvu zake kabla ya fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil, wachezaji wengine waliowahi kufanya hivyo ni gwiji la Brazil, Rivaldo, ambaye alicheza kwa kiwango cha chini sana kikosini Barcelona wakati fainali za Kombe la Dunia 2002 zilipokuwa zinakaribia.
Kiungo nguli wa Ufaransa, Zinedine Zidane alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa fainali za Kombe la Dunia 2006 zilizofanyika Ujerumani, likiwa ni tukio lililowashangaza wengi baada ya kucheza vibaya sana mechi za mwisho wa msimu katika klabu ya Real Madrid.
Messi hajawahi kuonyesha kiwango anachokionyesha Barcelona kwa sasa, hivyo jambo hilo linadaiwa huenda ukawa ujanja tu wa kutunza nguvu zake ili kwenda kung’ara kwenye michuano ya kimataifa.
Anaamini kujitoa sana kwenye Barcelona kutamfanya ashindwe kung’ara Brazil.
Avamia na mchumba kwa FabregasMambo hayaendi vizuri ndani ya uwanja kwa upande wa Barcelona kwa sasa, lakini hilo halikuwafanya wachezaji wa timu hiyo kufanya mambo yao.
Mastaa kadhaa wa Barcelona, walivamia nyumbani kwa kiungo Cesc Fabregas kusherehekea siku ya kuzaliwa ya binti wa mwanasoka huyo, Lia.
Kwenye sherehe hiyo, Gerard Pique alivamia na mkewe nyota wa pop, Shakira, wakati Lionel Messi alimchukua mchumba wake mrembo Anotella Roccuzzo na kwenda naye kusherehekea Ijumaa iliyopita. Nyota wengine wa Barcelona waliohudhuria sherehe hiyo ni Carles Puyol na Xavi.