Katika wiki iliyopita tulizungumzia kwa kirefu juu ya dhana ya mbadilishano wa haki(reciprocity of rights).
Tukasema kuwa maana ya dhana hii ni kuwa kila anaedai haki ajuwe kuwa haki ile ina wajibu lazima autekeleze,tukatowa mfano wa mke na mume,mume amepewa haki ya kuwa kiongozi wa familia lakini hakuachwa tu akapewa na jukumu la kuikimu familia yake kwa kila kitu.
Mke naye Uislamu umempa haki ya kutunzwa na mumewe kwa kila kitu hata kama yeye mke ni tajiri hahitajii, baada ya kupewa haki hii hakuachwa tu bali akapewa jukumu la kumtii na kumhudumia mumewe wakati wowote atakaomuhitajia.
Halikadhalika tunapozungumzia haki za mfanyakazi, mfanyakazi hana haki ya kudai haki fulani kama hajatekeleza wajibu wake kwa sababu yule mfanyiwa kazi naye ana haki zake, ni lazima wabadilishane haki na wajibu ndipo mambo yatakapokwenda sawa.
Kwa hakika Uislamu umemtukuza mfanyakazi na kumheshimu kwa sababu anatafuta riziki yake kwa njia ya halali, na ukatambua na kutetea haki za wafanyakazi kwa mara ya kwanza katika dunia wakati ambapo kwa kanuni za kizamani mfanyakazi alikuwa akihesabiwa kama mtumwa au kiumbe duni.
Kwa miaka hali iliendelea kuwa hivyo si katika nchi za kishenzi kama wanavyopenda kutuita bali kwa hao mabingwa wa haki za binadamu Ulaya na Marekani.
Kwa mfano mfanyakazi alikuwa hana haki ya kujadili kiasi gani alipwe, muda wa kazi na usalama kazini,mpaka karne ya kumi na tisa hadi mwanzo wa karne ya ishirini mfanyakazi alikuwa hana haki yoyote kazini.
Ndipo ikaja fikra ya kuunda vyama vya wafanyakazi (Labour Unions) kwa ajili ya kutetea haki zao, migomo na maandamano ikatokea mpaka wakalazimika kukubali kuwa wafanyakazi nao ni binadamu wana haki zao.
Lakini Uislamu tangu karne ya saba ulizitambua haki hizi za mfanyakazi wakati wazungu miaka mingi baadae wakimuona mfanyakazi ni kama mtumwa.
Uislamu bila ya shinikizo za migomo na maandamano kabla mwanaadamu hajajua kuunda vyama vya wafanyakazi ulimpa mfanyakazi haki ambazo ni za kimaumbile kwa hakika, ili kumpa mfanyakazi maisha mazuri na ya heshima yeye na familia yake akiwa hai na baada ya kufa.
Kama ambavyo Uislamu umewataka waajiri kuamiliana vizuri na wafanyakazi wao muamala wa kibinadamu na wa heshima, na kuwaonea huruma na kuwatendea wema na kutowapa kazi nyingi juu ya uwezo wao na haki nyingi nyingine ambazo hatuwezi kuzitaja zote.
Ni lazima utambue kuwa hawa ni watu muhimu kwako kwa sababu lau watagoma kazi zao hutaweza kuzifanya na utapata hasara kubwa.
Zifuatazo ni baadhi ya haki za mfanyakazi
1-Haki ya malipo:
Ni haki ya msingi kabisa ya mfanyakazi kulipwa malipo yake bila kupungua,kwani malipo yake ndiyo yatakayomfanya aishi maisha ya heshima bila kuomba,iwapo mtu atafanya kazi lakini asilipwe ujira wake itakuwa ni dhulma kubwa na ni kinyume na falsafa ya kufanya kazi,mtu afanya kazi ili aweze kujikimu na wanawe kutokana na kazi yake. Bali Mtume wa Uislamu amekwenda mbali zaidi ya hapo,siyo tu umlipe mfanyakazi wako bali umlipe kabla jasho halijakauka bila kumcheleweshea malipo yake.
Kama baadhi ya watu wanavyofanya,mtu ametekeleza wajibu wake lakini anamzungusha katika malipo yake,njoo kesho, sijakwenda benki njoo usiku, huu ni udhalilishaji na ni kinyume na haki za mfanyakazi, wanasheria wana kauli yao maarufu a justice delayed is ajustice denied (haki iliyocheleweshwa ni haki iliyokataliwa) kuchelewesha haki ni sawa na kuikataa.
Vile vile kumpa mtu kazi kabla ya kupatana naye malipo, ni muhimu muelewane kabla ya kuanza kazi ili isitokee kutokuelewana baadae.
2-Kupewa haki alizoahidiwa na mfanyiwakazi:
Ni lazima kwa mfanyiwakazi kumpa mfanyakazi haki zote alizomuahidi bila ya kupunguza chochote, kufanya hivyo ni dhulma yenye adhabu kali kisheria.
Hairuhusiwi kwa hali yoyote ile kupunguza kitu katika mambo mliyoahidiana, ama kwa kumuona ni mnyonge hawezi kukufanya kitu, au kwa kumuona ni mjinga hajui sheria, kufanya hivyo ni vibaya na ni kutangaza vita na Mungu wako alo kuumba.
3-Kutompa kazi zaidi ya uwezo wake:
Ni wajibu kwa kumfanyiwa kazi kutomchosha mfanyakazi kwa kumpa kazi zitakazomchosha au kumdhuru afya yake, na ikiwa kazi fulani yahitajia vifaa maalum vya usalama ni wajibu wa mfanyiwakazi kumpatia vifaa hivyo.
4-Kumheshimu mfanyakazi:
Ni wajibu kwa mfanyiwakazi kumheshimu mfanyakazi wake kwani yeye si mtumwa ni binadamu kama yeye, asimdhalilishe kwa kumpiga au kumtukana kama kumwambia kuwa njaa ndiyo iliyokuleta hapa, kufanya hivyo ni vibaya sana.
5-Kutekeleza matakwa ya Mungu:
Ni wajibu wa mfanyiwakazi kumpa nafasi mfanyakazi wake kutekeleza matakwa ya Mungu wake kama vile kusali nk. Baadhi ya mabosi wanadhani kuwa wafanyakazi wanaoswali huwatia hasara kwa kuwa muda wa swala wao wanakwenda kuswali,si sawa. Ni lazima ujuwe kuwa sifa muhimu kwa mfanyakazi ni uaminifu na mfanyakazi muaminifu kwa Mwenyeezi Mungu atakuwa ni muaminifu kwako pia.
Pili wadhani wewe kuwa kazi zako zitafanikiwa iwapo wewe ni katika wale waliokhiyari maisha ya dunia juu ya akhera na wanaozuia watu na njia ya Mwenyeezi Mungu?
6-Haki ya kufungua mashitaka:
Kwa kuwa mfanyakazi si mtumwa ana haki ya kumshitaki muajiri wake akiona kuwa amemdhulumu au amemtendea kinyume na haki yake.
7-Haki ya fidia:
Mfanyakazi ana haki ya kulipwa fidia iwapo atafanyiwa jambo la kumdhuru mwili wake, nafsi yake au madhara ya namna yoyote yale. Hizi ni baadhi tu ya haki za Mfanyakazi ambazo tumekunjukiwa na nafasi ya kuzieleza hapa.
Kama tulivyosema kufuatana na msingi wa mbadilishano wa haki (reciprocity of rights) haki hizi atazistahiki mfanyakazi pale tu atakapotimiza wajibu wake,kwa sababu mfanyiwakazi naye ana haki zake.
Huwezi kustahiki na kudai malipo kamili iwapo wewe umefanya kazi nusu, huwezi kudai malipo ya mwezi mzima hali ya kuwa umefanya kazi ya siku kumi na tano, kwa kufanya hivyo ni makosa kisheria.