Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 na katika makala haya nitachambua aina zote za likizo zinazoonyeshwa katika sheria.
Likizo ni haki ya mfanyakazi yeyote, mwajiri na mfanyakazi wanatakiwa kukaa meza moja na kukubaliana muda wa likizo kwa kila mfanyakazi bila kuathiri haki hii ya msingi kwa mfanyakazi mwenyewe na bila kuathiri shughuli za mwajiri.
Kama nilivyosema hapo juu kuna aina nyingi za likizo ambazo kwa mujibu wa sheria hii (niliyotaja hapo juu) mfanyakazi anastahili kulingana na mazingira mbalimbali katika maisha ya binadamu.
Likizo ya mwakaLikizo ya mwaka inapaswa kutolewa kwa mfanyakazi aliyefanya kazi kwa muda maalumu na siyo chini ya miezi sita katika mwaka, ikiwa ni pamoja na wale wa msimu, kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 29 na 31 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.
Sheria inaagiza mfanyakazi apatiwe likizo ya mwaka ya angalau siku 28 mfululizo. Neno mfululizo hapa lina maana sawa na kusema siku 28 hizo zikiwa ni pamoja na siku za mapumziko na siku za sikukuu zitakazoangukia katika kipindi hicho. Wafanyakazi wengi wamekuwa na tabia ya kuuza likizo zao, yaani inapofikia wakati wa likizo yeye haendi ila anafanya kazi na kulipwa mara mbili.
Hili ni jukumu la mwajiri. Mwajiri ni lazima atoe likizo kwa wafanyakazi, ambao nao ni lazima wachukue likizo hizo za mwaka na hazitakiwi kuuzwa au kubadilishwa kwa malipo ya aina yoyote ile, isipokuwa kwa kibali kilichotolewa na Waziri wa Kazi kwa mujibu wa kifungu cha 100 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.
Hata hivyo kifungu cha 31(6) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini 2004, kimekataza kabisa kwa wafanyakazi kufanya au kufanyishwa kazi wakati wa likizo ya mwaka. Likizo ya ugonjwaUkisoma kifungu cha 2 cha sheria hii, utagundua kuwa sheria hii inatumika kwa wafanyakazi wote wakiwemo wale wanaofanya kazi katika utumishi wa umma.
Cha kusikitisha hapa ni jinsi waajiri wengi hasa katika mashirika binafsi wanavyopuuzia sheria hii kwa makusudi kabisa ama kwa kutokujua. Hili huonekana hasa pale mfanyakazi anapougua au anapopata ulemavu katika mazingira ya kazi. Ninachotaka kumaanisha hapa ni kwamba, mfanyakazi atastahili kupewa siku 126 za likizo ya ugonjwa akiugua ndani ya kipindi cha kila miaka mitatu.
Kwa mujibu wa sheria, siku 63 za mwanzo kati ya hizo 126, mfanyakazi anayeugua anastahili kulipwa mshahara kamili na siku 63 zilizobaki, atalipwa nusu mshahara, kama inavyofafanuliwa katika kifungu cha 32(2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini 2004.
Hata hivyo, mwajiri habanwi au halazimishwi kumpa likizo hii mfanyakazi iwapo kama hakupewa uthibitisho wa cheti cha daktari au iwapo kama mfanyakazi huyo anastahili likizo ya ugonjwa kwa malipo kwa mujibu wa sheria nyingine yoyote, au utaratibu mwingine wa hifadhi ya jamii kama vile bima, makubaliano ya pamoja. Hii inaelezwa katika kifungu cha 32(3) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004.
Likizo ya uzazi kwa wanawakeKwa mujibu wa matakwa ya kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004, mfanyakazi mwanamke anapaswa kutoa taarifa (ya miezi mitatu kabla ya tarehe anayotegemea kujifungua), kwa mwajiri wake (ikiambatana na cheti cha daktari) juu ya nia yake ya kuanza likizo ya uzazi.
Hivyo basi, ni sawa na kusema kwamba, mfanyakazi huyo ni lazima apewe likizo ya uzazi ya malipo kwa siku 84 ndani ya mzunguko wa likizo wa miaka mitatu, lakini pia likizo hiyo itaongezwa na kufikia siku 100 iwapo kama atajifungua mtoto zaidi ya mmoja, kama ilivyoelekezwa na kifungu cha 33(6) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004.
Kwa upande mwingine endapo mtoto aliyezaliwa atafariki ndani ya kipindi cha mwaka wa kwanza tangu kuzaliwa kwake, mfanyakazi huyo (yaani mama), atastahili siku nyingine 84 ndani ya mzunguko uleule aliopewa siku za mwanzo, kama inavyoelekezwa na kifungu cha 33 (7) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004.
Mfanyakazi husika atatakiwa kurudi kazini pindi tu anapomaliza likizo yake ya uzazi, ambapo katika kipindi cha kunyonyesha, hatakiwi kupewa kazi ambazo ni hatarishi kwa afya ya mtoto. Vilevile, kifungu cha 33 (10) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004 kinampa mfanyakazi huyo muda usiozidi saa mbili za kunyonyesha mtoto wakati wa saa za kazi, kwa kila siku.
Hivyo wakina mama ulizieni juu ya haki zenu hizi. Hata hivyo, kwa sasa sheria bado imenyamaza kimya kuhusu kipindi cha mwisho cha mfanyakazi kupewa muda wa kunyonyesha mtoto wakati wa saa za kazi.
Kwa mantiki hiyo, uzoefu, busara na makubaliano ya haki ni lazima yatumike kufikia muafaka wa muda huo, baina ya mwajiri na mfanyakazi au wafanyakazi wake.