Dar es Salaam. Pambano la bondia Francis Miyeyusho na Ronald Pontillas wa Ufilipino lililokuwa lifanyike leo limeahirishwa hadi Aprili 12, kutokana na sababu ambazo ziko juu ya uwezo wa waandaaji.
Katibu Mkuu wa Chama cha Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), Anthony Lutha, alisema pambano la Miyeyusho limeahirishwa kutokana na sababu ambazo ziko juu ya uwezo wao.
Promota wa pambano hilo, Mussa Kova alisema, pambano la Miyeyusho na Pontillas limeahirishwa baada ya kocha wa bondia huyo kupewa taarifa tofauti kutoka hapa nchini.
“Pontillas aliambiwa pambano halitakuwepo na kiongozi wa ngumi (alimtaja jina) na alimwambia kuwa Miyeyusho ana pambano Aprili 26, hivyo hawezi kucheza Aprili 5 na kweli walipoangalia kwenye mtandao boxrec wakaliona hilo pambano hivyo wakaghairi kuja,” alisema Kova.
Alisema pambano hilo limesogezwa mbele hadi Jumamosi ijayo ambapo sasa Miyeyusho atapigana na bondia mwingine wa Ufilipino, Angelito Merin.