Tangu mimba inatungwa na kipindi chote cha ujauzito ni wakati muhimu mno kwa mjamzito, lakini wakati muhimu zaidi ni wakati wa kujifungua.
Yapo mambo muhimu ambayo yanapaswa kufanyika mara mama mjamzito anapofikishwa kwenye chumba cha kujifungulia.
Jina la kituo lazima liandikwe kwenye sehemu yake kwenye kadi ya kliniki.
Tarehe na muda alioanza kupata uchungu na kulazwa, chupa kupasuka au hapana. Umri wa mimba na kimo chake kwa wiki, mlalo na kitangulizi cha mtoto pamoja na upimaji wa nyonga ni baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia.
Upimaji sahihi wa nyonga hutoa taswira ya mwelekeo wa kujifungua kwa kulinganisha na makadirio ya ukubwa wa mtoto.
Ndani ya chumba cha kujifungulia ni lazima viashiria vyote vya hatari wakati wa ujauzito vijulikane kwa anayemhudumia mama wakati wa kumlaza kwa ajili ya kujifungua.
Viashiria hivi ni kidokezo A au B katika ujauzito, chupa kupasuka bila uchungu, uchungu kabla ya wiki 34, saa 12 kupita tangu uchungu kuanza, damu kutoka, mapigo ya moyo ya mtoto kuwa juu ya 160 au chini ya 120 kwa dakika pamoja na kubadilika badilika, kifafa cha mimba au presha kuwa zaidi ya 140/90 na upungufu wa damu chini ya gramu 8.5 kwa desilita na homa juu ya kiwango cha 38 sentigredi.
Mambo haya yanapogundulika kwenye kituo kidogo cha afya, mhudumu anapaswa kumpeleka kituo kikubwa au hospitali na daktari kupewa taarifa mara moja.
Ndani ya chumba cha kujifungulia, maendeleo ya uchungu husimamiwa kwa grafu maalumu (partogram). Matumizi sahihi ya grafu hii ni njia mojawapo ya kupata matokeo mazuri kwa uzazi salama kwani huonyesha kama mama anaendelea vizuri au kuna viashiria vya hatari vinajitokeza, hivyo kutoa nafasi kwa mhudumu kuchukua hatua mapema kabla madhara hayajatokea.
Grafu hii huratibu mambo makuu matano amabyo ni mapigo ya moyo wa mtoto aliyeko tumboni, kufunguka kwa njia ya uzazi sehemu ya shingo (cervix) ili kuruhusu mtoto kupita, kushuka kwa mtoto hadi kutoka, kiwango cha maumivu ya uchungu kila baada ya dakika 10 na hali ya afya ya mama kwa ujumla.
Uratibu wa mambo haya makuu hufanywa kwa pamoja au kwa mpangilio kutegemea na hali ya kujifungua aliyokuja nayo mzazi mtarajiwa.
Mzazi anaweza kupokelewa wakati uchungu haujakazana wala njia kufunguka au uchungu umekolea na njia kufunguka zaidi ya sentimita tatu.