Kitendo cha kuahirishwa mara kwa mara kwa vikao vya Bunge la Katiba kimewakera baadhi ya wakazi wa Mji wa Dodoma ambao sasa wanapendekeza chombo hicho kivunjwe.
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema kuwa vurugu za bungeni zimewachosha na kuwafanya wakose hamu ya kuangalia au kusikiliza mijadala.
Katibu wa uchumi wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) mkoani Dodoma, Mary Chihoma alisema kwa hali ilivyo sasa, haya ni matumizi mabaya ya fedha za wananchi.
“Hatuwezi kusema ni mtu mmoja ndiye ambaye anastahili kubeba lawama hizo.
Hawa wote wanatakiwa kulaumiwa moja kwa moja kwani wanakula kwa wasichokifanyia kazi,” alisema Chihoma.
Mwanasiasa huyo alitoa wito kwa wajumbe hao kumwogopa Mungu na kurudi kwenye mjadala wa msingi wa kutunga Katiba.
Mkazi mwingine, Kayumbo Kabutali alitaja chanzo cha vurugu hizo kuwa ni wajumbe kuacha misingi bora ya hayati Julius Nyerere na Shekhe Abeid Karume.
Kabutali alisema Wajumbe wa Bunge hilo wameacha kabisa misingi hiyo na kujikita katika masilahi binafsi jambo ambalo linaweza kuigharimu nchi yetu kwa ujumla.