Kuna kila dalili kwamba Mita Mpya za LUKU, zinazosambazwa kwa sasa na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kwa wateja wake nchini, zinaweza kuwa na harufu ya ufisadi baada ya wateja walio wengi waliofungiwa luku hizo kulalamikia ubora wake zikilinganishwa na Mita za Luku za zamani zilizokuwa zikitumiwa na wateja hao.
Malalamiko hayo ya wateja wapya wa Tanesco, hasa wa jijini Dar es Salaam, kuhusu ubora wa LUKU mpya hizo, yamekuja katika kipindi ambacho Serikali imewasimamisha kazi kwa muda vigogo watano wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), kutokana na kukabiliwa na tuhuma zenye harufu ya ufisadi wa kuagiza nje ya nchi mabehewa mabovu ya abiria na mizigo kwa ajili ya treni ya reli ya kati, inayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam-Kigoma na Dar es Salaam-Mwanza.
Hivi karibuni, Serikali, kupitia kwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ilitangaza kumsimamisha kazi kwa muda Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu na watumishi wenzake wanne baada ya ripoti ya uchunguzi kuwahusisha na sakata la ununuzi wa mabehewa mabovu 274 ulioisababishia shirika hilo na Serikali kwa ujumla wake hasara ya Sh bilioni 230.
Mbali na Kisamfu, watendaji wengine waliosimamishwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao ni Mkurugenzi Mkuu wa Ndani wa TRL, Jasper Kisiraga, Meneja Mkuu wa Manunuzi, Fedinarnd Soka, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa na Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles.
Inadaiwa kwamba Machi 21, 2013, watendaji wakuu hao wa TRL waliingia mkataba wa kununua mabehewa hayo aina ya Ballist Hopper Bogie (BHB) kutoka kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industrial Limited ya India, wenye thamani ya Sh bilioni 431.6 kwa ajili ya kutumika katika uimarishaji wa njia za Reli ya Kati, kabla ya mabehewa hayo kuwasili nchini Julai mwaka 2014.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba baada ya mabehewa hayo kuanza kazi yalilalamikiwa na wadau wengi wa shirika hilo yakidaiwa kutokuwa na ubora unaotakiwa, hali iliyomlazimu aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi wa wakati, Dk Harrison Mwakyembe kuunda kamati kwa ajili ya kuchunguza, pamoja na mambo mengine mazingira yaliyotawala katika zabuni hiyo iliyopelekea kuingizwa nchini kwa idadi kubwa hiyo ya mabehewa yakiwa mabovu huku mzabuni akiwa tayari amelipwa gaharama zake zote kwa mujibu wa mkataba.
Wakati Watanzania wakiwa bado wanatafakari kuhusu tuhuma hizo ndani ya TRL na hatua hizo zilizochukuliwa na Serikali kupitia kwa Wizara inayohusika na uchukuzi, wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam waliofungiwa mita mpya za luku na Tanesco, wametilia shaka ubora wa luku mpya hizo kwa kile wanachodai kwamba umeme unapopungua nguvu wakati wa jioni au asubuhi kutokana na ongezeko la matumizi ya umeme majumbani, mashine hizo mpya za luku hupoteza nguvu ya kuwasha umeme na wakati mwingine kuzimika kabisa.
Kutokana na kasoro hiyo inayodaiwa kutokana na uduni wa ubora wa LUKU hizo, wateja hao wa Tanesco ambao wengi wao ni wapya, wamelitaka shirika hilo kuziondoa mita zao mpya hizo na badala yake wawafungie LUKU za zamani ambazo wanasema zina ubora zaidi usiotiliwa shaka yoyote katika mazingira yoyote ya upatikanaji wa umeme kuliko luku mpya hizo.
Kwa mujibu wa wateja hao wa Tanesco, LUKU hizo mpya zinazolalamikiwa zina umbo dogo tofauti na zile za zamani, ingawa wanasema kimuonekano na kiumbo, LUKU hizo ni nzuri, bali tatizo liko kwenye ubora wake hasa katika nyakati ambazo matumizi ya umeme majumbani yanaongezeka, ambapo mara nyingi unakuwa ni wakati wa jioni ya saa moja hadi usiku wa saa nne na asubuhi kati ya saa 12 na saa mbili.
Mmoja wa wateja wa Tanesco anayekabiliwa na adha hiyo ya usumbufu wa luku mpya hizo, aliyejitambulisha kwa jina la Hussein Mtega, ameiambia FikraPevu kwamba mbali na kukabiliwa na adha hiyo ya usumbufu huo wa kukatika kwa umeme katika kipindi hicho cha upungufu wa umeme kunakotokana na ongezeko la matumizi makubwa ya umeme majumbani, kila wanapotoa taarifa Tanesco kupitia vituo vyao vya kutolea huduma kwa wateja, huwa hawapati msaada wowote wala majibu ya kuridhisha juu ya tatizo la mita hizo, hali inayowafanya muda mwingi kukaa gizani.
Sikuweza kumpata mtaalam wa kiufundi wa masuala ya LUKU ndani ya Tanesco ili kutolea ufafanuzi malalamiko hayo ya wananchi ambao wengi wao ni wateja wa shirika hilo, hata hivyo uchunguzi binafsi uliofanywa na timu ya waandishi wetu umebaini kuwa kabla mita za LUKU zinazoagizwa nje hazijaingizwa nchini (zinatakiwa kufanyiwa majaribio ya kihandisi) ambayo kitaalam huitwa Factory Acceptance Test (FAT) huko huko kiwandani zinakotengenezwa.
Kwa mujibu wa uchunguzi wetu huo kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani ya shirika hilo pekee la umeme nchini, mita nyingi za LUKU za Tanesco huagizwa na kuingizwa nchini bila kufanyiwa majaribio hayo ya kihandisi kwa kuwango kinachotakiwa kutokana na maelezo kwamba shirika hilo halina kiwanda wala nchi maalum kwa ajili ya kutengenezewa mashine hizo za luku, bali huwa linaziagiza kutoka nchi mbalimbali duniani, zikiwemo China na Afrika Kusini.
Ofisa mmoja mwandamizi wa Tanesco, ambaye hakupenda jina lake litajwe kutokana na sababu za usalama wa ajira yake, amekiri kuwepo kwa kasoro za kiufundi katika mita hizo mpya za LUKU, hasa katika maeneo nchini yenye umeme mdogo (low voltage), hali inayosababishwa na matumizi makubwa ya umeme.
Kwa mujibu wa Ofisa huyo wa Tanesco, kwa kawaida umeme unaotakiwa kuingia kwenye mita hizo mpya za LUKU, hivyo kuiwezesha zifanye kazi vizuri unatakiwa uwe na nguvu kati voti 200 na 230 kwa umeme wa njia moja, lakini nguvu hiyo inaposhuka chini ya voti 200 hadi 170, LUKU hizo hushindwa kufanya kazi na hatimaye kukata umeme kabisa.
“Umeme unaposhuka au kuongezeka kuliko kiwango cha kawaida kinachotakiwa, yote mawili hayo yanaweza kusababisha hatari ya uharibifu wa vifaa vinavyotumia umeme, wakati mwingine huweza kuunguza hata nyumba,” anatahadharisha Ofisa huyo.
Msemaji wa Shirika la Tanesco, Adrian Severin, alipoulizwa juu ya malalamiko hayo ya wateja wao kuhusu uduni wa mita hizo mpya za LUKU, amekiri kuyafahamu malalamiko hayo.
Anasema kwa sasa, ili kukabiliana na tatizo hilo la LUKU mpya hizo, shirika hilo limejipanga kuongeza transfoma mpya katika maeneo yaliyobainika kukabiliwa na tatizo la umeme mdogo unaosababisha luku hizo zishindwe kufanya kazi vizuri.
Alipotakiwa kueleza nchi ambako mita hizo mpya za luku ziliagizwa pamoja na kampuni iliyopewa kazi hiyo ya kusambaza luku hizo kwa Tanesco, Severin alisema:
“Tuna LUKU za aina nyingi. Zipo zilizotengenezwa Korea, Thailand, China, Afrika Kusini na kadhalika,”Kwa siku za karibuni Tanesco, imekuwa ikiwafungia wateja wake wapya mita mpya za LUKU, zenye muonekano tofauti na zile za zamani, huku mita mpya hizo za LUKU zikidaiwa kuwa bora zaidi ya zile za mwanzo, lakini pia zikielezwa kuwa rahisi kuhamishika kuliko mita za LUKU za zamani.
Habari hii ni Kwa hisani ya Fikra Pevu.
Kwa habari za Matukio Kitaifa, Kimataifa, Michezo na Burudani, Ungana nami kupitia Link zifuatazo hapo chini.
In order you follow me just click one of the Icon Button above.