Kuwa na mafanikio makubwa na hatimaye kuwa tajiri ni kitu ambacho kinaonekana kuwa kigumu kwa wengi ama hakiwezekani kabisa. Hii yote inatokana na wengi kutokujua njia au mambo muhimu ya kufanya hadi kufikia mafanikio makubwa.
Kutokana na hili wengi wamekuwa wakijiuliza wafanye nini au kitu gani kitakachowafanikisha katika maisha yao. Kiuhalisia, katika maisha kuna vitu ambavyo ukifanya iwe kwa kukusudia au bahati ni lazima uwe tajiri na pia kuna vitu ambavyo ukifanya, sahau mafanikio katika maisha yako.
Vitu hivi vinaweza kuwa tabia zetu au mienendo tuliyonayo ambayo inakuwa inaathari kubwa kwetu na hii ndiyo naweza sema ni siri kubwa iliyofichika kati ya watu wenye mafanikio na ambao hawana. Watu wenye mafanikio wamemudu kwa kiasi kikubwa kufanya mambo yanayowafanya wawe matajiri, huku maskini wakiwa hawajui hilo na kuendelea kufanya vitu vinavyowafanya kuwa maskini.
Kwa wewe kulijua hilo tu, tayari una nafasi kubwa ya kufanikiwa na kufanya mambo makubwa katika maisha yako. Kama kweli umechoshwa na umaskini, na umedhamiria kweli kuwa tajiri hakikisha unafanya mambo haya:
1. Hakikisha unajiwekea mipango na malengo makubwa.
Kama kweli unataka kufanikiwa na kuwa tajiri ni lazima ufanye hili. Huwezi kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kama una tabia ya kujiwekea malengo kidogo.
Watu wote wenye mafanikio huwa ni watu wa kujiwekea malengo makubwa na ambayo huanza kuyafatilia kila siku na kuhakikisha mpaka yanatimia. Acha kujidharau au kujiona hufai eti kwa sababu huna pesa na ukashindwa kujiwekea mlengo yako.
Panga mipango yako vizuri, kama ni pesa zitakuja zenyewe wakati unaendelea kutekeleza mambo mengine. Ukiwa na malengo makubwa hii itakusaidia kufanya kazi kwa bidii kubwa na hautaweza kukata tamaa mapema. Chukua tabia hii muhimu ikusaidie kukufanikisha.
2. Hakikisha unatumia muda wako vizuri.
Muda ni kitu muhimu sana katika maisha yetu. Kama wewe ni mtunzaji mzuri wa muda na haupotezi muda hovyo, elewa kabisa kufanikiwa kwako ni lazima. Watu wengi kutokana na kutokujua ama mazoea ambayo wanayo toka mwanzo, ni watu wa kupoteza muda sana.
Kama tabia hii ndiyo unayo, kufanikiwa na kupiga hatua mbele itakuwa ngumu katika maisha yako. Jifunze kutunza muda utaona mafanikio makubwa sana ambayo hukufikiri hapo mwanzo.
3. Hakikisha unajifunza vitu vipya kila siku.
Tatizo kubwa walilonalo watu wengi ni kutopenda kujifunza vitu vipya. Wengi ni wavivu wa kusoma hali ambayo hupelekea kukosa vitu vizuri vyenye uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yao. Kama unataka mafanikio makubwa katika maisha yako, ni lazima uwe msomaji mzuri pia. Hii itakusaidia wewe kupambana na changamoto kwa kujua wengine waliweza kukabiliana nazo vipi. Ni lazima ujenge utaratibu wa kujisomea vitu vitakavyobadili maisha yako.
4. Usiwe mtu wa kulaumu tu.
Wapo watu ambao siku zote ni watu wa kulalamika tu na kulaumu wengine ndio waliopelekea wao kuwa hivyo. Hawa ni watu ambao mara nyingi hufikiri kuwa wao wamekuwa maskini pengine kutokana na wazazi hawa kuwasaidia au hawakusoma na visingizio vingi tu. Hii ni tabia ambayo haiwezi kukufikisha popote, zaidi ya kukurudisha nyuma. Kama nia yako kubwa ni mafanikio achana na visingizio, chukua hatua za kusonga mbele.
Vipo vitu vingi vya kufanya na ukaondokana na kulaumu kwako. (Unaweza ukasoma pia Huu Ndio utajiri mkubwa utakaoupata kama utaamua kufanya biashara hii)
5. Hakikisha unaye ‘mentor’ wa kukuongoza kwenye mafanikio yako.
Asilimia kubwa ya matajiri wote walioko duniani wanao watu waliowaongoza katika maisha yao hadi kufanikiwa. Ni muhimu hata kwako wewe kuwa na ‘mentor’ au mtu ambaye atakuongoza kwenye mafanikio yako.
Mara nyingi huwa hatujui kila kitu katika maisha yetu. Kama katika kitu ulichochagua kufanya yupo mtu ambaye tayari amefanikiwa katika hilo eneo ni vizuri ukamtumia ili akakuongoza ili usije ukapotea kiurahisi na kufanya makosa ambayo pengine hukustahili kuyafanya.
6. Hakikisha unaepuka madeni yasiyo ya lazima.
Kama umekopa mkopo benki, hakikisha huo mkopo unakusaidia kuongeza kipato chako. Acha kukopa mkopo halafu unaamua kujengea nyumba au kununua gari, na matokeo yake pesa zote unazipoteza unaanza kuhangaika namna ya kulilipa deni hilo.
Kati ya vitu ambavyo vimewafanya wengi kujuta na kujilaumu katika maisha yao ni mikopo. Kama umeamua kukopa, uwe mwangalifu ili usije ukaumia baadae wakati unarudisha hilo deni. Kikubwa jifunze kutumia mkopo vizuri.
7. Hakikisha unaweka akiba ya kutosha.
Kila pesa unayopata hakikisha unajiwekea akiba yako. Wataalamu wengi wa masuala ya mafanikio wanashauri angalau asilimia kumi ya kile unachokipata iweke kama akiba yako. Pesa hii inapokuwa nyingi itakusaidia wewe kuwekeza katika miradi yako mbalimbali. Hakikisha pesa hii unaiwekeza na usiitumie katika matumizi mengine yasiyo ya lazima.
Kama ukifanya hivi kwa pesa hii utakuwa upo kwenye nafasi ya kupata mafanikio makubwa katika maisha yako.Kwa kufanya mambo hayo unao uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yako kwa jinsi unavyotaka na kuwa tajiri.
Kumbuka hukuzaliwa maskini au mlalahoi kama unavyodhani, kikubwa jifunze kuwa na fikra sahihi zitakazo badili maisha yako na kisha chukua hatua sahihi kuelekea malengo yako uliyojiwekea.
Hakuna kinachoshindikana kila kitu kinawezekana endapo tu ukiamua.Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea Mutalemwa Blog na ujifunze mambo mengi na mazuri zaidi.
Kwa habari za Matukio Kitaifa, Kimataifa, Michezo na Burudani, Ungana nami kupitia Link zifuatazo hapo chini.
In order you follow me just click one of the Icon Button above.