JUMA NYOSSO anaendelea kutumikia adhabu yake ya ‘kikatili’-kutokucheza soka kwa miaka miwili kwa kosa la kumshika sehemu ya makalio nahodha wa Azam FC, John Bocco na bahati mbaya zaidi rufaa yake ‘imewekwa kapuni’ kwa mwaka mmoja sasa.
Najiuliza sana, ‘hivi ni kweli soka ni mchezo wa kiungwana?’ Katika nchi zilizoendelea wanaamini soka ni mchezo wa kiungwana ndio maana matukio yote yanayojiri katika mchezo huu huchukulia ni ya kiungwana.
Soka lina kanuni/sheria zake ambazo zinaufanya mchezo huu kuwa na maana ya fair play. Kama, Nyosso alipewa adhabu kubwa vile, ni kwanini basi, Agrey Morris anaendelea kuwaumiza wachezaji wenzake na hachukuliwi hatua za kinidhamu?
Jumatano ya wiki iliyopita mlinzi huyo wa Azam FC alimchezea faulo mbaya mshambulizi wa Stand United, Mnigeria, Chidiebere Abasirim na kumvunja taya.
Hakuna aliyekemea hilo. Labda ni kwasababu ya urafiki ama uoga. Aggrey ni ‘mkatili’ kuliko Nyosso ndiyo maana alifanya jaribio lingine la kutaka kumvunja mshambulizi wa Yanga SC, Mzambia, Obrey Chirwa katika pambano la jana Azam FC 0-0 Yanga SC.
Misimu miwili iliyopita mlinzi huyo wa kati wa timu ya Taifa ya Zanzibar alimchezea rafu mbaya aliyekuwa mshambuliaji wa Simba SC, Emmanuel Okwi kiasi ambacho watazamaji wote wa mechi ile walihamaki na kudhani labda Okwi atakuwa ameumizwa vibaya.
Agrey si muungwana na licha ya kwenda kumjulia hali, Chidiebere siku moja baada ya kumuumiza kwa makusudi mchezaji huyo alikuwa tayari kumuumiza pia Chirwa.
Uungwana ni vitendo wala si maneno matupu na katika hili la Aggrey dhidi ya Chidiebere TFF inapaswa kuchunguza kisha kuchukua hatua ya kumfungia mchezaji huyo wa Azam FC ili kumuonya vinginevyo atakuja kuua mchezaji mwenzake uwanjani.
Jamaa anacheza vibaya sana na nashangaa anaendelea kupata mashabiki, labda kwa vile matukio yake yote ya kutisha ameyafanya kwa wachezaji wa kigeni.
Kumfungia Nyosso miaka miwili na kushabikia vitendo vya kihuni kupitiliza vinavyofanywa na Aggrey si haki.
Ombi langu kwa TFF ni kulichunguza tukio la kuumizwa kwa Chidiebere na kutafuta tukio lile la Agrey dhidi ya Okwi kisha kutazama mechi ya jana ya Azam v Yanga ili kupata kujiridhisha zaidi kuhusu tabia mbaya kiuchezaji ya mlinzi huyo wa Azam FC.
Kama Nyosso alifungiwa kwa kumshika Bocco sehemu ya makalio na kumuacha Agrey na ukatili wake akiendelea kuwaumiza wenzake si haki. Kumfungia Nyosso na kushabikia ‘ukatili’ wa Aggrey Moris si haki, TFF ifanye uchunguzi.
Usikose kuangalia Movies mbalimbali kutoka kila kona ya dunia, bofya kwenye picha iliyopo hapo chini kuona izo muvies